Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpa hongera sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa weledi mkubwa. Pamoja na kwamba Serikali imeendelea kuboresha huduma mbalimbali kwenye Jimbo langu la Ngorongoro ikiwepo elimu na afya bado kuna changamoto kubwa sana katika nyanja mbalimbali za kijamii.

Mheshimiwa Spika, nianze na afya; kata nyingi hazina huduma za afya kwa maana ya kutokuwa na zahanati wala kituo cha afya, hivyo wanakosa huduma hizo na kupelekea kupoteza maisha wakiwa njiani kufuata huduma za afya sehemu za mbali ambayo ni wastani wa kilometa 60 hadi 100.

Mheshimiwa Spika, wananchi wameendelea kujitolea na kuanza ujenzi wa majengo mbalimbali kwa ajili ya uhitaji wa huduma za afya; ombi langu naomba Wizara itenge fedha kwa ajili ya umaliziaji wa vituo vya afya vifuatavyo ambavyo vimejengwa kwa nguvu wananchi: -

(i) Kituo cha Afya Arash - wananchi wamejenga majengo matano na yote yamepauliwa kwa nguvu zao wenyewe, Serikali ikitupatia shilingi 300,000,000 wananchi watapata huduma ukaribu sana.

(ii) Kituo cha Afya Samunge - wananchi wamejenga majengo saba na yote yamepauliwa, Serikali inatakiwa kutenga fedha kwa ajili kukamilisha ujenzi wa kituo hiki cha afya ili wananchi wapate huduma kwa ukaribu.

Mheshimiwa Spika, kata ambazo hazina vituo vya afya ni pamoja na Kata ya Kirangi, Kata ya Piyaya, Kata ya Maaloni, Kata ya Engusero Sambu, Kata ya Oldonyosambu, Kata ya Ololosokwan, Kata ya Ngaresero, Kata ya Pinyinyi, Kata ya Soitsambu na Kata ya Digodigo.

Mheshimiwa Spika, wananchi kutoka kwenye kata nilizozitaja hapo juu hufuata huduma za afya kwa wastani wa kilometa 60 hadi -100 jambo ambalo linahatarisha maisha yao. Hivyo, naomba Wizara itenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu elimu; bado suala la elimu kwa Wilaya yangu ya Ngorongoro ni duni sana, shule nyingi za msingi zimechakaa sana na zinahatarisha maisha ya wanafunzi wanaosoma kwenye madarasa chakavu. Hivyo, basi naiomba Serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati wa majengo chakavu na ujenzi wa madarasa mapya pamoja shule mpya kwenye vijiji vya Kirtalo (Losirwa) Kijiji cha Soitsambu (Esilalei).

Kwa upande wa elimu ya sekondari; Wilaya ya Ngorongoro ina shule 11 tu Serikali kati ya kata 28. Hivyo, niiombe Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari kwenye Kata za Pinyinyi, Arash, Soitsambu, Enguserosambu, Oloirien Magaiduru, Digodigo na Kata ya Maaloni.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ugawaji wa maeneo ya utawala, naomba Wizara itusaidie kuongeza maeneo ya utawala hasa kwenye kata ambazo zina kijiji kimoja badala ya vijiji zaidi ya kimoja ambapo Kata ya Ngaresero ina kijiji kimoja; Kata ya Sale ina kijiji kimoja; Kata ya Digodigo ina kijiji kimoja; Kata ya Pinyinyi na Kata ya Piyaya ina kijiji kimoja.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Wizara itusaidie kugawa baadhi ya kata zifuatazo ambazo utoaji wa huduma kwa wananchi imekuwa ngumu sana; kata hizo ni Enguserosambu, Soitsambu, Ololosokwan, Malambo, Oldonyosambu na Oloirien Magaiduru.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara, Wilaya ya Ngorongoro ina mtandao wa barabara wa kilometa 934, hivyo naomba tuongezewe fedha za kutosheleza kutengeneza barabara zote ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.