Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujalia zawadi hii ya uhai na kuweza kuiona siku hii ya leo. Pili nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendela kuwa na imani na mimi kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi yake Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa kumsaidia Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki hapa TAMISEMI, ni imani kubwa sana, ni imani kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Chamwino hapa Mkoani Dodoma, kwa imani yao ambayo wanayo kwangu mimi kama Mbunge wao na niwaahidi tu wanachamwino kuendelea kuwatumikia kama vile ambavyo wanatarajia kutoka kwa Mbunge wao na tutaendelea kushirikiana kila siku katika changamoto mbalimbali za Jimbo letu la Chamwino.
Mheshimiwa Spika, nikienda moja kwa moja kwenye hoja mbalimbali ambazo Wabunge walizizungumza humu ndani, karibia kila Mbunge aliyesimama humu alizungumzia suala la barabara kupitia TARURA. Waheshimiwa Wabunge, wengi mlisifu sana jitihada ambazo zimefanyika na taasisi ya TARURA nchini ya Engineer Seif, niwatoe mashaka Waheshimiwa Wabunge, ninyi mmekuwa ni mashahidi kwamba ndani ya mwaka mmoja TARURA imefanya kazi kubwa sana kwenye Majimbo yetu, kuhakikisha barabara zinapitika kwa kuhakikisha madaraja yanapitika.
Mheshimiwa Spika, mtakumbuka mwaka mmoja na nusu ama miwili iliyopita kabla ya Serikali hii ya Awamu ya Sita kuingia madarakani, TARURA walikuwa na bajeti ya Bilioni 257 tu, lakini ni utashi wake Rais wetu Dokta Samia Suluhu Hassan, aliona namna ifanyike kuweza kuongezea TARURA fedha. Fedha ile imekwenda kuleta mabadiliko makubwa ambayo huenda tungeyasubiri kwa miaka mingine 10 au 15 kuweza kufikia utengenezaji wa barabara kama tulivyofikia sasa.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wote mmesema fedha TARURA haitoshi, niwatoe mashaka katika mwaka huu wa fedha bajeti imeachwa vilevile kama ilivyokuwa mwaka jana na tunakwenda kutekeleza miradi yenye thamani ya Bilioni 838 kwa fedha za ndani na fedha za nje kutoka TARURA. Hii ina maana kila mmoja wetu humu kwenye Jimbo lake na kwenye Mkoa wake anaenda kufikiwa na taasisi yetu ya TARURA.
Mheshimiwa Spika, Watanzania mamilioni na mamilioni wanaenda kufikiwa na TARURA na ninaamini mwakani tukirudi hapa kama ambavyo walikuwa wakimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TARURA na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Waheshimiwa Wabunge hapa mtazidi kutoa pongezi hizo katika bajeti ambayo inafuata.
Mheshimiwa Spika, kitu ambacho naweza nikasema kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni kutoa commitment yetu ya usimamizi wa miradi hii. Tutahakikisha hakuna ubadhilifu, tutahakikisha inaenda kukamilika kwa wakati, vilevile tutahakikisha value for money inakuwepo katika miradi hii yote ya barabara ambayo ipo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la elimu, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia, nakumbuka Mheshimiwa Vedastus Manyinyi Mathayo Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini alizungumzia suala la madawati, madarasa yamejengwa mengi
sana, lakini tukumbuke katika mwaka wa 2021/2022 katika madarasa ya UVIKO tayari madawati 794,000 yaliweza kutengenezwa kuendana na madarasa yale yaliyojengwa na UVIKO-19 katika shule za sekondari. Pia madawati 45,000 kwa shule za msingi.
Mheshimiwa Spika, ni commitment ya Serikali, ni commitment ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kuhakikisjha kwamba utengenezaji wa madawati unaendana na madarasa yaliyopo. Ninyi ni mashahidi hivi sasa kila eneo la nchi yetu limeguswa na madarasa mapya katika sekondari, katika mradi wa BOOST ambao unaenda kuanza hivi karibuni na Waheshimiwa Wabunge wote, Mheshimiwa Waziri wangu Angellah Jasmine Kairuki amewapa barua ya kuonesha mradi wa BOOST unapoenda kugusa katika Majimbo yenu. Tutahakikisha yale madarasa yanayojengwa vilevile yanaenda kuwa na madawati ya kutosha, kwa hiyo niwatoe mashaka Mheshimiwa Vedastus Manyinyi Mathayo na Waheshimiwa Wabunge wengi mliozungumzia suala zima la madawati.
Mheshimiwa Spika, katika miradi hii ambayo pia imekuwa ikitekelezwa ya madarasa yale ya Milioni 470 katika Majimbo na Wilaya zetu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tunaenda kuisimamia kikamilifu ikamilike na watoto walio dhamiriwa kuingia kwenye Shule zile waweze kuingia kwa wakati. Kuna wengi wenu hapa ni mashahidi shule zile zimeshaanza kupokea wanafunzi, kuna zingine ambazo ziko mwishoni kwenye ukamilishaji. Sisi kama timu ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI tutahakikisha shule zile zinaenda kukamilika vizuri, awamu inayokuja vilevile tutahakikisha changamoto zilizojitokeza katika awamu hii ya kwanza basi haziendi kujitokeza zile ambazo zinakuja kwa kila Halmashauri shule za Milioni 470.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ni kwenye shule hizi za wasichana za A-Level ambazo zimeshajengwa 10 za kwanza katika Mikoa Kumi ya mwanzo, awamu ya pili tunaenda kwenye Mikoa Mitano halafu tutakuja kumalizia kwenye Mikoa iliyobaki. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tunakwenda kuhakikisha sasa fedha zinapofika kule zinatumika mara moja hakuna ucheleweshaji kama maeneo mengine ambavyo yalikuwa yamejitokeza, vilevile tunaenda kuhakikisha zile changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza ya hizi shule Kumi ambazo Bilioni 30 imekwenda kila Mkoa Bilioni Tatu changamoto zile hazijitokezi tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kumaliza kwa kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)