Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Bunda na kwa bahati nzuri nina Kata saba, kwa hiyo, niwashukuru wapiga kura wa Nyamang’uta, Nyamswa, Salama, Mihingo, Mgeta na Hunyali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Wabunge wote nikiwemo mimi mwenyewe, hatua ya kufika hapa ni ndefu sana. Kwa kweli, Mwenyezi Mungu ametusaidia tumefika hapa wote, jambo la kwanza naomba tupendane, hii habari ya kushabikia vyama na kunyoosheana vidole itakuwepo, lakini iwe kwa wastani, kwa sababu wote tunaishi kama binadamu na tukifa au tukifiwa tunaenda kupeana pole, kwa hiyo tunapokuwa humu ndani naomba tupendane.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba Wabunge wa CCM wajue kwamba, nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumekabidhiwa sisi, hawa jamaa zetu wapo tu kwa kupinga na kupiga kelele. Kwa hiyo, tunatakiwa tufanye kila la maana kuwatendea haki Watanzania ili tunapofika 2020 hawa watakwenda kuuliza, tuliwaambia CCM hamuwezi sasa mnaona mmefanya nini? Kwa hiyo, tufanye kila la maana ili nchi yetu iweze kupata maendeleo ikifika 2020 tuwaoneshe kwamba tumefanya nini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais, sijui huwa najiuliza mara mbili mbili hivi kuna nini? Kwa sababu kabla ya mambo yote tunasema nchi inaliwa, nchi mbovu, hali mbaya, tunalia kila mahali, leo tumepata jembe, tingatinga anapiga kila upande bado watu wananung’unika nini? Hivi nchi hii tusipopata Rais nje ya Magufuli tunapata Rais wa aina gani? Kilichobaki ni kusahihishana tu pale na hapa mambo yanakwenda sawa, lakini Rais anafanya kazi nzuri sana.nn(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye utawala bora. Katika utawala bora naangalia mafunzo ya Halmashauri za Vijiji, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata. Tumekuwa na tabia ya kuchagua viongozi halafu hatuwapi mafunzo, hata humu ndani Wabunge tumo tu, hatukupata mafunzo bora, juzi nilikuwa namuuliza mwenzangu hapa, hivi maana ya mshahara wa Waziri ni nini? Ananiambia na mimi sijui! Unashika mshahara wa Waziri, mshahara uko benki wewe unaushikaje? Anasema sijui. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulitakiwa kuelezwa kwamba hivi vitu vinakwendaje, kuna Vote, kuna sub-vote, kuna program tulitakiwa tupewe mafunzo. Mafunzo kwa Watendaji wa Vijiji ni jambo la msingi sana, lakini imezungumzwa hapa habari ya Wenyeviti wa Vijiji kulipwa mshahara au kupewa posho. Serikali za Halmashauri au Halmashauri za Wilaya haziwezi kutoa posho, hilo tukubaliane!
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote tumetokea maeneo hayo, tumetoka kwenye vijiji, tumetoka kwenye Kata tunakuwaje hatuwatetei watu hawa wapate posho nzuri? Tunapaswa kufanya kila namna Watendaji wa Halmashauri za Vijiji, Wenyeviti wa Vijiji wapate posho nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo nizungumzie habari ya migogoro ya mipaka. Kuna migogoro ya mipaka ya Wilaya na Wilaya, kuna migogoro ya mipaka kati ya Kata na Kata, kuna migogoro ya mipaka kati ya Vijiji na Vijiji na ni mingi sana, kwenye Jimbo langu ipo katika kila eneo. Tunaomba Wizara zinazohusika na maeneo hayo, TAMISEMI na Ardhi washirikiane kumaliza migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Shule za Msingi, jambo ambalo Bunge la Kumi na Moja tutafanya na tutapata heshima ni kupata madawati ya watoto, madawati ya wananfunzi katika shule za msingi. Ukienda shule ya msingi ukiingia darasani watoto wanaamka wanakusalimia shikamoo mzazi, unasema marahaba, halafu unawaambia kaeni chini au unafanyaje? Wanakaa kwenye vumbi! Huwa najiuliza, naomba Waziri Mkuu afanye kazi mmoja, tufanye kazi moja au kazi mbili tu na nitoe njia. Kwanza, tukubaliane kwamba Bunge hili Bajeti yoyote kutoka Wizara mbalimbali ikatwe tupate bilioni 150 za kuweka madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepiga hesabu hapa yamepungua madawati 1,500,000 kama milioni nne, kwa hiyo, tukipata bilioni 160 au 170 maana yake madawati nchi nzima yanakuwepo. Waheshimiwa Wabunge tukitoka hapa tutakwenda kupambana na tatizo la madawati hamtakwepa, saa hizi kuna meseji zinazotoka kwa DED ooh! Mheshimiwa Mbunge hela yako ya Mfuko natengenezea madawati, nani kakutuma utengeneze madawati mimi sijafika huko?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tukubaliane kwamba madawati ni jambo la kwanza katika Bunge hili. Tutoke humu tujue kwamba tunakwenda kupata madawati nchi nzima, tukisema hii ya Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa tumetofautiana kipato katika Mikoa. Dar es salaam watatengeneza, Arusha watatengeneza, Bunda je, ambayo ni Wilaya ya maskini? hawawezi kutengeneza madawati! Kwa hiyo, nafikiri kwamba jambo la msingi sana kufanya mambo kama haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kama hatuwezi kuweka bajeti bilioni 160 kutoka Wizara mbalimbali, tukubaliane na Waziri Mkuu aunde Kamati ihusishe Kambi zote, Kamati itafanya kazi moja ya kujua idadi ya madawati nchi nzima, lakini kujua mashirika mbalimbali. Kwa mfano, tukasema hivi ukiweka shilingi tano katika Makampuni ya Simu, ukiweka shilingi tano kwa Makampuni ya Mafuta, ukiweka taasisi mbalimbali tulizonazo, hatuwezi kupata bilioni 160? Inawezekana! Waziri Mkuu aunde Kamati ili tuweze kupata watu, wafanye tathmini, watuletee hapa, wote tuchange.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Bunge letu limechanga, tumechanga bilioni sita au uwongo jamani?
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, tumechanga bilioni sita kutokea Bungeni humu ndani, tunataka Mashirika mengine yote na Taasisi zingine zichange.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yangu kwa leo yalikuwa hayo, naomba kuunga mkono hoja.