Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii, leo Mheshimiwa Rais, nimeshamshukuru kwa niaba ya watumishi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. Leo niwapongeze Mheshimiwa Simbachawene kwa kuaminiwa kuwa mdau wa Utumishi wa Umma nchini, nikupongeze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilivyokuwa naangalia sifa zao wote ni Wanasheria, kwa hiyo kuna makusudi na sababu kuwapeleka Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Waende wakarekebishe sheria, wakaangalie Kanuni na wakaangalie miongozo iliyopitwa na wakati ndani ya utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nampongeza Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete nilimwambia hivi, kuna sheria ambazo zilitungwa kabla yeye hajazaliwa lakini bado ziko kwenye utumishi wa umma, tumezifanya nazo kama ni imani ya Dini kama ni Biblia na Qurani ambavyo huwa havibadiliki. Niwaombe wakazibadilishe. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, nasema hivyo kwa sababu gani? Kuna standing order inayosema kwenda na nyaraka ya Serikali nje ya ofisi ni makosa, lakini leo hii tunatumiana hata kwenye vishikwambi hizo nyaraka za Serikali. Leo hii tunatumiana kwenye e-mai,l je, ukiambiwa umefanya kosa utatokea wapi? Wakati kuna standing order inayosema hivyo, ndiyo maana ya sheria ninazosema wakaziangalie ni za aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitaongelea ajira kazi kubwa ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma ni ajira, ni kuajiri watumishi ndani nchini, lakini leo TAMISEMI anaajiri, tukikaa Wizara ya Afya itaajiri, hizo ajira tunazi–control vipi? Huko nyuma tulishafanya, Wizara zikapewa mamlaka na idara za Serikali kuajiri. Shida tuliyopata Serikali ikaamua kuunda Sekretarieti ya Ajira na Katibu wake wa kwanza akiwa ni Daudi Xavier ambaye sasa hivi ni Naibu Katibu Mkuu, Utumishi wa Umma, ni kwa sababu waliona haiwezekani, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ndiyo iangalie ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya matatizo tunayopata kwamba wameajiri kwa upendeleo wamefanya nini? Ni kwa sababu hakuna ambaye ndiye anayesimamia. Kwa mfano Mama Jenista Mhagama akiwa Waziri wa Utumishi alituambia amefungua kanzidata tukakupongeza, hivi kama hiyo kanzidata ingekuwa inatunzwa na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na wao ndiyo wanaajiri, leo hii kulikwa na sababu ya kutangaza kazi hizi tulizotangaza? Tungerudi kwenye kanzidata tukaangalia wale walioomba, nafasi zikawa kidogo wakabaki ndio wangeajiriwa, kwa sababu tayari walikuwa wameshafanya interview. Hii ingepunguza gharama ya Serikali za kurudia tena kwenye kuajiri. Hilo niwaombe Wanasheria wangu wawili hapo wakaliangalie upya, wasimame kwenye instrument yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna miundo inayokinzana, leo hii ukiangalia kwa RAS pale ndiyo anasimamia Halmashauri lakini niongelee kada ya sheria tu iwe mfano. Mwanasheria aliyeko kwa RAS ambaye kazi yake ni kusimamia wanasheria walio kwenye Halmashauri, yeye anaitwa Afisa Mkuu na analipwa mshahara wa kimadaraka lakini wenzake walio kwenye Halmashauri ni Wakuu wa Vitengo na wanalipwa mshahara wa kimadaraka siyo wa kimuundo, huyu analipwa kimuundo hawa kimadaraka. Sasa mtu anayelipwa mshahara wa kimuundo wa Afisa Mkuu atamsimamia ambaye ni Mkuu wa Kitengo analipwa marupurupu yote? Kazi tunaitegemea ipatikane sawa? Ndiyo maana mikataba mingine inapita ya kiajabu ajabu kwa sababu huyu mmeshamdogosha hawezi kumsimamia mtu ambaye anamzidi mshahara na cheo, hilo nalo mkaliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee faragha ya Viongozi. Viongozi wetu tunasema Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na ninyi Waheshimiwa Wabunge. Kwa nini inaonekana labda viongozi wa sasa hivi hawana maadili mazuri? Ni kwa sababu tumewaondolea haki yao ya faragha. Viongozi wetu, kuwa Waziri Mheshimiwa Jenista hakukutoi kwenye raha zako zingine. Zamani mlikuwa na faragha, mlikuwa na Leaders Club, mlikuwa na Mikoani sehemu za kukaa viongozi wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo, pale ukikaa hata ukiburudika na bia moja ukadondoka wanakubeba viongozi wenzako na hautalisikia mtaani. Leo hamna pa kukaa mkafanya faragha zenu na hilo limeonekana kama hakuna maadili, lakini maadili ni yale yale, watu ni wale wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Leaders Club ikarudi Menejimenti ya Utumishi wa Umma, hapa Dodoma mjenge Leaders Club ya Viongozi kwenda kupumzika baada ya saa za kazi, na hii inasababisha hata document za Serikali ku- leak. Kwa sababu zamani, ukienda Leaders Club unampelekea Katibu Mkuu document au Waziri aliyepo pemebeni ni Waziri mwenzake au Katibu Mkuu mwenzake, lakini leo tukikuletea Morena kuna simu zingine zina mita 200 zinavuta document unaikuta magazetini. Turudishe hizo faragha.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ndugu zangu niongelee Vyuo vyetu vilivyo chini ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Hivi vyuo kila chuo kilianzishwa kwa maana yake. Chuo cha Uhazili Tabora kilikuwa ni kutoa Masekretari mahiri, wenye stenography, leo tunao? Kwa sababu chuo kile sasa tumekibadilisha, kumekuwa na miundo mingi pale, masomo mengi pale kimekuwa ni cha kibiashara. Pia iko wapi IDM Mzumbe ambapo watu walikuwa wakishakuwa Maafisa Wakuu mnapelekwa pale kufundishwa uongozi, kufundishwa uzalendo, kufundishwa maadili. Leo iko wapi? ndiyo maana tunaona maadili hayapo, watu wanateliwa hawajapelekwa mahali popopte kupikwa. IDM imebadilika leo ukitafuta historia yake iliyoianzisha haipo tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Chuo cha Utumishi wa Umma, Magogoni kilikuwa ni chuo cha ku-refresh watumishi waliokazini! Leo hii tumeweka wanafunzi wanaotoka shuleni moja kwa moja, yale maadili yake yameondoka. Niwaombe muende mviangalie vyuo hivyo. Leo hii hatuna wa kuzalisha hata ma-stenographer wa kuja hapa Bungeni wa kwenda Mahakamani wa kwenda kwenye Taasisi za nje zinazokuja hapa. Hawapo hawazalishwi kwa sababu tayari vyuo tumeshavichanganya.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja mkono.(Makofi)