Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Omar Issa Kombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wingwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia na mimi nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Ofisi ya Rais. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia mpaka muda huu nikiwa bado nina neema yake ya uhai na afya njema. Vilevile nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yao yote Wizarani kwa kuandaa hotuba nzuri kabisa na kuiwasilisha kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Jemadari Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya maendeleo anayoendelea kuifanya katika Taifa letu. Mama ameonesha uwezo mkubwa sana na kwa kweli anastahili pongezi. Tunapompongeza, hatumpongezi kwa bahati mbaya, ni kwa mazuri na makubwa tunayoyaona katika nchi yetu ambayo anaendelea kuyatekeleza mama huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia hotuba hii kwenye taasisi ya TASAF. Nitagusia kidogo tu. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuutekeleza mradi huu kwenye jamii yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali kuendeleza mradi huu. Tunafahamu kwamba mradi huu umeanza awamu kwa awamu, ulianza na Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa, wakaja viongozi wengine wakauendeleza. Sasa kitendo cha Mheshimiwa Rais Samia kukubali kuuendeleza mradi huu, kwa kweli, anastahili pongezi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, naipongeza TASAF, imekuwa ikifanya kazi nzuri sana. Pia kuna maeneo naomba niishauri Serikali ili iangalie katika program hii ya TASAF. Kwa mfano, kwenye vigezo vya kuwatambua wanufaika; malalamiko yamekuwa mengi kwa wananchi wetu kwamba, kuna baadhi ya wananchi wana sifa za kuingia kwenye mpango huu, lakini kwa kweli bado wanaendelea kuachwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iangalie vigezo. Kwa mfano, tunapoangalia kigezo cha umasikini, tukiangalia kwamba mtu akipata nyumba tayari eti anaonekana kwamba, sio masikini. Tuangalie hiyo nyumba ameipataje? Kuna mazingira tofauti ya kuipata nyumba. Wakati mwingine mtu anajengewa na wahisani. Hatuwezi kusema kwamba huyu siyo masikini tena. Au wakati mwingine familia ilikuwa na baba, baba amefariki, anapofariki familia hii inarudi katika ukwasi wa maisha. Kwa hiyo, kigezo cha nyumba hakiwezi kutumika kama ni kigezo cha mtu kutoingizwa kwenye Mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tuangalie vilevile ruzuku inayotolewa. Naipongeza TASAF imeandaa program za kutoa ajira za muda. Lengo la ajira hizi ni kuwawezesha wananchi kujimudu katika vile vipindi vigumu. Pia tuangalie: Je, unapokwenda kumlipa mtu Shilingi 3,000/= kwa siku, hivi jamani kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ni njema na malengo ni mema, lakini kulingana na kupanda kwa gharama za tuangalie namna ya kuboresha. Shilingi 3,000 sasa hivi kumpa mtu kwa kweli haiwezi kwenda kumsaidia kama vile ambavyo Mheshimiwa Rais amekusudia kuwasaidia wananchi wake. Kwa hiyo, tuangalie ikiwezekana tuongeze angalau iwe shilingi 5,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile muda wanaoutumia katika hizi ajira za muda. Wanakwenda wanufaika wanaanza saa 01:00 mpaka saa 09:00, analipwa shilingi 3,000, kulingana na ukubwa wa kazi na muda anaoutumia. Muda huo anaoutumia ina maana tayari hapa hatumsaidii. Ni vema tukaweka muda mchache ili aweze kufanya kazi nyingine za kumwingizia kipato. Nadhani hii itakuwa ni njia sahihi ya kuweza kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile miradi ambayo tutakwenda kuifanyia kazi, tuwachagulie zile kazi nyepesi. Kama tunavyofahamu kwamba, wanufaika wengi wa TASAF hali zao ni duni, wengi wao ni akina mama. Kwa mfano, katika jimbo langu tunakwenda kutekeleza mradi huu wa ajira za muda kwenye masuala ya zege. Mama unambebesha saruji, wengine wanaangukanayo, ni jambo ambalo kwa kweli Mheshimiwa Waziri, ni lazima tuliangalie kwa kina. Ni vyema tukawatafutia zile kazi nyepesi ambazo wanazimudu, lakini vilevile muda wanaoutumia uwe mchache ili waweze kwenda kufanya shughuli nyingine za kujiingizia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikwazo kingine ni suala la vitambulisho vya NIDA. Mara nyingi Wabunge tumekuwa tukipiga kelele kuhusu tatizo la vitambulisho vya NIDA. Tokea Wizara hii iko kwenye Kamati ya USEMI tumekuwa tukishauri mara kwa mara kwamba, Wizara ikutane na Wizara ya Mambo ya Ndani, wakae kwa pamoja waangalie namna ya kutatua au kama haiwezekani basi, kigezo cha kitambulisho cha NIDA kiondolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Masheha, akishathibitishwa na Sheha basi aweze kuingizwa kwenye Mpango, lakini suala la kuweka kitambulisho cha NIDA kama ni kigezo, na huku tayari kuna vikwazo vya kupata hicho kitambulisho cha NIDA, hapa itakuwa hatuwatendei haki wananchi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akutane na Wizara inayohusika ili tuangalie namna ya kutatua changamoto hii ya vitambulisho vya NIDA ili wananchi waweze kupata haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa haraka kulingana na muda, nije kwenye program ya kuendeleza miundombinu ya miradi ya kijamii. Tumeelezwa hapa kwamba kuna miradi 550 tayari iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji. Naomba kuwe na utaratibu mzuri wa kugawanya miradi hii, kwa sababu kuna baadhi ya Shehia, mfano kwenye jimbo langu Shehia ya Mjini Wingwi, Mapofu, wamepeleka barua za maombi ya miradi kama hii, lakini hadi leo ukiangalia, miradi inapelekwa sehemu moja au sehemu chache, wakati wananchi wanaohitaji miradi hii ni wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili mkalifanyie kazi. Kwa zile Shehia ambazo tayari wameshapeleka barua zao za maombi basi na huko kuangaliwe namna ya kufanyiwa kazi. Wananchi wote tunahitaji hizi huduma, keki hii ya Taifa tuweze kuifaidi sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nije kwenye upelekaji kwenye rufaa. Tumeelezwa kwamba, bado kuna malalamiko ya rufaa yanaendelea kufanyiwa kazi na ni muda sasa. Kwenye majimbo yetu wananchi wanakuwa wakitulalamikia kwamba rufaa imekuwa ni muda mrefu, watu wanatolewa bila utaratibu. Hebu niombe hizi rufaa ziende kwa haraka ili kama anastahili kuingizwa kwenye mpango aendelezwe kwenye mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha zaidi ni kwamba kuna wananchi tayari wameshafanya kazi karibu miezi miwili, lakini wanafikia mahali wanaondolewa kwenye mpango na kile walichofanyia kazi bado hawajalipwa. Niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi iende ikafanyie kazi hizi rufaa. Hawa wananchi kama wanastahili kupata hizi haki waendelee kuzipata, lakini kama hawastahili vilevile kuandaliwe utaratibu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vikundi, kutolewa elimu kwa wanufaika. Tumeambiwa kuna vikundi kadhaa vimeundwa, lakini ukifuatilia kwa kweli bado wananchi hawa elimu ya kuibua miradi ni ndogo. Tutumie maafisa wetu wa huduma za jamii, lakini vilevile tutumie wataalam wetu ili waweze kuwasaidia wanufaika hawa waweze kuibua miradi kulingana na mazingira wanayoishi ili mradi huu wa TASAF uweze kukidhi yale malengo ambayo Mheshimiwa Rais ameyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, nishukuru sana, naunga mkono hotuba hii. Ahsante sana. (Makofi)