Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pia, naendelea kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kujali huu utumishi wa Umma, maana mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Tumeona jinsi ambavyo Serikali imeendelea – japo kuwa ana keki ndogo – lakini imeendelea kujali utumishi wa Umma ukilinganisha na ambavyo ilikuwa hapo nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mawaziri wetu, Mheshimiwa Simbachawene, pamoja na Mheshimiwa Ridhiwani. Nampongeza pia Mheshimiwa Jenista Mhagama, wakati tunajadili bajeti yetu hiii tulishirikiana naye vizuri kwa sababu wakati huo yeye ndio alikuwa Waziri wa Wizara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Wizara imeendelea kufanya kazi zake ambazo ni za msingi kwa maana ya kusimamia utumishi wa Umma, utendaji kazi bora, pia kuhakikisha stahiki za wafanyakazi zinasimamiwa sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii ni Wizara ambayo ina- deal na rasilimali watu, rasilimali watu ukiisimamia vizuri ndiyo inaweza kusimamia rasilimali nyingine; rasilimali ardhi, madini, maji n.k. Na haya malalamiko yote ambayo tunayaona, kama kuna usimamizi mzuri wa rasilimali watu hatutakuja kuyaona. Ubadhirifu hatutakuja kuuona. Kwa hiyo, ni muhimu sana kusimamia rasilimali watu, kwa hiyo Wizara hii inafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo; nikienda kwenye Fungu 32. Fungu hili limekuja na mifumo mingi, mifumo hii ndiyo kwanza inaanza, kuna mfumo ambao tunauita wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma. Mfumo huu ni kama ule ambao ulikuwa OPRAS siku za nyuma. Ule ulikuwa unaamua, mnakaa watumishi mnajikusanya mnajijazia. Na mwajiri anakuwa anakutazama unafananaje anakujazia. Lakini sasa hivi kuna mfumo huu umekuja unasimamia utendaji kazi wa utumishi wa Umma na mwingine unasimamia utendaji kazi wa taasisi za Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu mpaka sasa hivi umefanya majaribio kwenye taasisi 11 za Umma na umefanya kazi nzuri sana. Na sasa hivi mfumo huu utakuwa unaangalia ubora na wingi (workload). Kwa hiyo, automatically inakwenda kwenye mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati unamjazia mtumishi utapunguza upendeleo na unyanyasaji, whether unampenda au humpendi lakini zile grades zimekuja kwenye mfumo. Kwa hiyo, hii itatoa moyo kwa watumishi sasa hivi, watakuwa na ari. Kwa hiyo, itakuwa na usimamizi mzuri na wafanyakazi watafanya kazi kwa moyo na hakutakuwa na uonevu kama ambavyo nimesema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri mifumo hii ndiyo kwanza inaanza, ina nia njema, naomba mamlaka mtandao iongezewe bajeti kuwe na fedha za kutosha kuhakikisha usimamizi wa mfumo huu. Ni mwema, lakini kama hautasimamiwa vizuri, hautakuwa na ulinzi, ina maana ile tija haitaonekana; ndiyo ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mfumo mwingine unaitwa wa Taarifa za Utumishi na Mishahara. Mfumo huu ni mzuri sana kwa sababu tunakumbuka zamani, mchakato wa mshahara ulikuwa unachukua hata siku 14, lakini sasa hivi mchakato wa mshahara siku moja tu umesambaa kote, umefika kwa siku moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza kuona mifumo hii ina nia njema ya kuboresha maslahi ya watumishi ili wafanye kazi kwa bidi ili kulinda utumishi katika sehemu nyingine mbalimbali, kutoa tija. Ukimpa mtumishi mshahara wake kwa wakati unamtia morali, unamtia moyo, anafanya kazi kwa ufanisi. Kwa hiyo, mifumo hii tusiidharau. Nimeijadili kwa sababu imeanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mfumo mpaka sasa hivi umeshaunganishwa kwenye taasisi 433 kati ya taasisi 522 tulizonazo kwenye utumishi wa Umma. Kwa hiyo, unaweza ukaona jinsi ambavyo Serikali inakazana. Nashauri kwamba mifumo hii isimamiwe kwa udhibiti mkubwa sana na pesa ziongezwe, iimarishwe, isambazwe kote. Huu mfumo pia, kwa mfano…

TAARIFA

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa anayechangia. Hapo awali tulishauri Bunge hili kwa habari ya kuondokana na Mfumo wa OPRAS, na Serikali sikivu ya Awamu ya Sita ilisikia, ikaenda kwenye mifumo hii mipya, PEPMIS na iLMIS ambayo kimsingi imeanza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kumuunga mkono mzungumzaji, anazungumza jambo jema sana kwa Taifa letu. Ninashauri ni muhimu sasa Wizara ya Utumishi ianzishe kitengo maalum kitakachoratibu uendeshaji wa mifumo hii nchi nzima. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kaijage, taarifa.

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kueleza jinsi ambavyo Mfumo huu wa Taarifa za Utumishi na Mishahara unavyofanya kazi vizuri. Sasa hivi ulivyoanza kufanya kazi kwenye taasisi hizi ambazo zimeshaunganishwa ukifika umri wako wa kustaafu automatically mfumo huu unatoa jina lako kwenye mshahara, unalihamishia kwenye mifuko ya pensheni. Kwa hiyo, itapunguza zile taratibu za mtu kuendelea kulipwa mshahara wakati alishatoka kwenye umri wa kustahili mshahara, na itapunguza udanganyaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu umeunganishwa na taasisi mbalimbali; NIDA, RITA na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii. Kwa hiyo, umeanza sasa hivi, tutaona baadaye effect yake. Sasa hivi ukifika muda wako wa kustaafu, umri wa kustaafu, kwa sababu RITA imeunganishwa na mfumo huu, automatically jina lako linahama, hupati tena mshahara, linahamia kwenye pensheni kwa hiyo, nipongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuomba kwamba mifumo hii iwezeshwe ili iweze kufanya kazi kwa tija na izalishe vizuri na watu waweze kuona umuhimu wake na hivyo, watumishi wakifanya kazi wawe wanajua kwamba mwisho wa siku watakuwa na utulivu na watakuwa hawana wasiwasi juu ya mafao yao na stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mfumo mwingine unaoitwa wa Tathmini ya Mahitaji ya Watumishi wa Umma. Sasa huu ni mfumo muhimu sana kwa sababu ndiyo ambao utakuwa unaonesha watumishi wako wangapi, wako sehemu gani, kuna upungufu wa watumishi kiasi gani, kuna wingi wa watumishi kiasi gani. Kwa hiyo, utakuwa unarahisisha Serikali kufahamu kwamba yamkini vituo viko sawa, vina level sawa, kwa mfano labda vya hospitali, kituo fulani kinahitaji watumishi 500, kingine watumishi 500.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukija kuangalia kwenye workload na idadi ya mtu ambaye ameona mgonjwa unagundua kwamba katika kituo fulani, japo kinafanana na kingine, lakini wana madaktari 50, wengine wana 100 lakini hawa wana wagonjwa wachache, kwa hiyo, kutakuwa kuna urahisi wa kuhamisha watumishi kutoka sehemu fulani kwenda sehemu nyingine kulingana na jinsi ambavyo mfumo unaonesha idadi, uwezo na ubora na workload anayotumia yule mtu kutibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mfumo huu utapunguza malalamiko mengi ambayo Wabunge wengi wamechangia. Unakuta sehemu fulani kuna watumishi wengi, sehemu nyingine kuna watumishi wachache lakini vituo vinafanana. Lakini ukiangalia katika uhaliasia workload aliyonayo mtumishi mmoja na yule mwingine ni tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mfumo huu ni mzuri sana, utabaini idadi ya uhalisia wa uhitaji wa wafanyakazi, utakuwa bayana. Nimeona niseme hivi vitu; nimeshazungumzia mambo mengi kuhusu wafanyakazi na kuwatetea, lakini naomba niwaoneshe, kwa sababu niko kwenye Kamati hii, mambo yanayokuja mbeleni yatakuwa mazuri. Ila tunachokiomba; Serikali iongeze bajeti ya e- Government ili mifumo hii isimamiwe vizuri iweze kuwa na tija baadaye. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)