Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niwapongeze Mheshimiwa Waziri na msaidizi wake kwa hotuba nzuri waliyoitoa. Lakini pia nimpongeze mtangulizi wake aliyekuwepo, Mheshimiwa Jenista, kwa kuyachukua mengi tuliyoyachangia katika Bunge la Bajeti lililopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yako baadhi ambayo hayajafanyiwa kazi. Sasa nilitaka kipindi tunaendelea kwanza nipongeze nafasi nyingi sana za ajira ambazo zimetoka, hasa hizi nafasi 21,200. Tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa nafasi hizo, walau zinapunguza joto ingawa joto bado ni kubwa, lakini at least zinapunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana wakati nachangia bajeti hii ya Utumishi specifically niliongelea

jambo moja linalohusu watoto waliomaliza katika vyuo vya maliasili lakini wakanyimwa ajira kwa sababu umri wao umevuka miaka 25. Nililisema hapa na ninaomba nilirudie kwa sababu ni kama halikufanyiwa kazi na bado halijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunapewa majibu humu ndani tuliambiwa sheria za Jeshi haziruhusu kuajiri mtu aliyevuka miaka 25. Nikasema sawa. Lakini vijana hawa wengi ambao tunasema wametoka kwenye vyuo vyao wamekuwa trained Kijeshi na tayari wanavyo vyeti. Sasa unaposema huwezi kumuajiri wakati ana cheti na umem-train Kijeshi na yuko mtaani, sidhani kama ni fair. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe, kwa sababu vyuo hivi ni vya Serikali, wazazi wamelipia kuwapeleka watoto wao wakaenda kusoma pale, tunaomba Serikali itumie busara ione vijana hawa ambao hawakuajiriwa kati ya 2015 mpaka 2022 waone jinsi ya kusaidiwa ili na wao jasho lao walilolitoa kujifunza mafunzo haya ya Kijeshi waone kwamba kuna sehemu wanakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuendelea kuwaacha mtaani ni kuwaonea. Maana mtu amesomeshwa na mzazi kwa ada ya milioni nne mpaka nane, leo anamaliza pale unamwacha mtaani unamwambia umri umevuka, na hakukataa kujiajiri, ni kwa sababu hatukuwa na nafasi za kuwaajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini huku tunapotoka kila siku tunalalamika tembo wanatoka wanajeruhi wananchi, wanafanya nini. Hawa vijana wako mtaani, tuone jinsi ya kuwachukua kwa sababu bado nafasi za kuwaajiri zipo; hilo ndiyo ninaomba. Mlichukue hivyo, Serikali ilione ili iweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu wa mwaka jana niliongelea pia habari ya nafasi zinazotoka kwa kigezo cha JKT. Wote ni mashahidi; kambi zetu tulizonazo za ku-hold watoto katika JKT hazitoshi wala haziwezi kuenea watoto wote walio mtaani. Lakini inashangaza kwamba nafasi bado zinatoka kwa kigezo cha kwamba mtu awe amepita JKT. Na humu ndani tulisema na Serikali ikasema imesikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninao mfano; nafasi za Uhamiaji zilizotoka ilikuwa ni miaka 18 mpaka 25 kigezo cha kwanza, kinachofuata, awe amehitimu JKT. Lakini ni vijana wangapi wamekuwa denied nafasi ya kwenda JKT? Unamnyima kwenda JKT, wakati wa kutafuta ajira umetangaza ajira unamwambia awe ametoka JKT. Inaumiza kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili naomba niliseme kwa niaba ya vijana walioko mtaani. Tumeona habari za Uhamiaji, tumeona nafasi za Magereza. Leo nilikuwa nasoma kwenye website ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi ambalo tunasema kwamba labda ndiyo basic; hakuna hiyo condition ya kwamba mtu awe ametoka JKT. Wameandika tu miaka 18 mpaka 25, awe Mtanzania aliyemaliza kidato cha nne, wao hawaweki kigezo cha JKT.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaomba haya Majeshi mengine ambayo yanafuata hapa wajaribu kuona, mpe nafasi huyu Mtanzania aje kwenye interview. Kama anafeli afeli kwa kigezo hicho cha kufeli baadaye mrudishe nyumbani, kuliko kum-deny kabisa hata nafasi ya kufanya interview. Watoto hawa wanaonewa, naomba hilo liangaliwe ili tuweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala lingine ambalo nataka niliongelee. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, jana ametutolea ufafanuzi mzuri sana hapa kuhusu hizi ajira, maana simu zimeelemewa huku; meseji ni nyingi, watu bado wanaendelea kutuma, pamoja na ufafanuzi wako wa jana meseji zinaendelea; wazazi, watoto na kila mmoja anaendelea kutuma. Lakini ninaomba nitoe suggestion moja; kuna mtu aliyeongea jana hapa kuhusu allocation ya hizi nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, wote hapa tulikwenda kuomba kura kwa wananchi. Wakati tunaomba kura kwa wananchi tuliinadi Ilani ya CCM. Ilani ya CCM imeweka specific kabisa kwamba tunataka kutengeneza ajira milioni nane. Ni aibu kwa Mbunge ninayesimama hapa leo, sijui hata watu ambao katika hizo nafasi 21,000 zilizotoka, leo hata jimboni kwangu naulizwa wametoka watu wangapi, sijui. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni Mbunge mwenzetu, unawawakilisha wananchi, na humu ndani hakuna mtu anayegombea kwamba hizi nafasi anazipeleka kwenye familia yake. Lakini tunachoomba ni kwamba pale tunaposhauri mawazo yetu ni mawazo ya wananchi, tunawasikiliza wananchi huko mtaani wanavyosema. Wanatoa mawazo kwamba kwa nini hata hizi nafasi zisigawanywe kwa kila jimbo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnatugawia pesa sawa ya miradi ya barabara, mnatugawia pesa sawa miradi ya maji, mbona kwenye ajira kunakuwa na kigugumizi? Tukigusia tu ajira mnaanza kusema ubaguzi. Tunachotaka ni kwamba nafasi zimetoka 21,200, hatutaki kumpangia Waziri nafasi zile amuweke nani au afanye nini, tunachotaka iwekwe equality. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepiga hesabu, nafasi 21,200, ukigawanya kwa halmashauri 184 za nchi hii wote wako sawa, kila halmashauri iko sawa, hakuna halmashauri kubwa wala ndogo hapa. Nawawakilisha wananchi na Wabunge wenzangu wanawakilisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukigawanya maana yake kila halmashauri itapewa nafasi 115 katika ajira hizi. Twende kwenye ile system yetu, system si unai-feed tu? Iwe ni system ya JAVA au kama ni C++ programming, unai-feed information, ielekeze, kwamba choose watu 140 kutoka wilaya hii itakupa, choose watu 140 kutoka wilaya nyingine watakuwepo pale, mkabidhi Waziri wa TAMISEMI mwambie watu wako 21,200 hawa hapa. Yeye awapange anavyotaka, lakini ajira hizi zisambae nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani sisi tunakaa hapa tunawawakilisha wananchi unatoka hapa wananchi kila mtu anatuma meseji, wewe unakuwa unamwambia mfumo. Wakati unaomba kura ulimwambia tutawasaidia kupata ajira, tutaleta maendeleo, leo unamwambia mfumo. Hiyo haikubaliki, tusaidiane. Najua bado deadline haijafika, mnaweza kwenda kwenye mfumo – Utumishi mko hapa – tukakubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri zaidi tunaye Mheshimiwa Bashe ni mfano tosha hapa kwenye Mradi wa BBT. Waliomba nchi nzima lakini kila wilaya imepata, tumeona, na yakatoka matangazo. Hakuna malalamiko tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanaouliza tunawaambia kwamba nafasi ya pili ya BBT inakuja, subiri. Iko wazi inaonekana. Ajira hazipo lakini zikitoka chache tukawaambia wilayani kwetu tumepata ajira 50, subirini raundi ijayo, wananchi wanaelewa na wanaelewa hali ilivyo. Kuliko unakwenda sehemu mtu anakuuliza huna hata jibu la kumpa. Ninaomba hilo tulizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuna kitu nimekuwa najiuliza. Ajira tunazoziona hapa; ualimu, huduma ya afya, hivi ajira za TRA huwa mnazitangazia wapi; ajira za BoT mnazitangazia wapi? We want to see them. Ajira za TANESCO mnazitangazia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka hata zile ajira kubwa tuone watoto wa maskini wakienda huko kwa sababu wamesoma. Kelele zilizoko huko ni kwamba wanahisi zile ajira ni za watoto wa viongozi, siyo za kwao. Tuone zikitangazwa wazi, huo mfumo uwekwe kwa uwazi kama ni kugawanya tugawanye equally, nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatutaki tuone watu wa TRA ukienda unakuta watu wa kabila fulani tu na watu wa eneo fulani. Tunataka uende ukute Muha, Mhaya, Mchagga, ukute nchi nzima tumeenea kule, that is what we want. Kwa sababu hii ni keki ya Taifa, tuigawane equally ili kila mmoja aweze kupata haki ya kutumika katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa kumalizia, ninachoomba, taasisi hii ya Sekretarieti ya Ajira, tulikuwa tunaomba kama inawezekana ajira zote zipitie huko, tui- empower hii Sekretarieti ya Ajira. Kwa sababu ndiyo usalama wa Taifa letu wenyewe ulipo, tuwaajiri watu tunaowajua watachujwa kwa vigezo wataonekana kwa merits na qualifications zao ili iweze kutusaidia hata kuulinda usalama wa nchi hii. Siyo sasa kila taasisi inaachiwa inaajiri yenyewe tukitoka hapo baadaye tunakuja tunataja mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nishukuru sana kwa nafasi. Lakini pia tuzidi kuangalia, tuzidi kumuomba Mheshimiwa Rais atusaidie ajira nyingine ziweze kuongezeka kwa sababu kweli kiuhalisia madarasa ni mengi, vituo vya afya ni vingi, watumishi wanahitajika na bado wengi wako mtaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunisikiliza, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)