Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kwa mchana huu nianze kuchangia kwenye Wizara hii, Fungu 67; lakini kabla nitoe pongezi sana kwa hotuba nzuri iliyowasilishwa na kaka yangu Simbachawene. Najua ni kwa msaada mzuri wa mdogo wangu Ridhiwani Kikwete, na ninatambua bila shaka watendaji kwenye Wizara hii ya Ofisi ya Rais Utumishi wako vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu najua ni kumi nimeziweka hapa ili yale ambayo ninayoweza kujaliwa kuyatimiza. Kabla, hii dakika moja lazima niseme vizuri juu ya kazi kubwa ambayo inafanywa na Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kila mmoja anayesimama hapa anajaribu kueleza ni jinsi gani Mheshimiwa Rais anafanya kazi, hatuwezi kumaliza kwa dakika moja. Nakumbuka, na ninawasilisha leo; wananchi wangu wa Jimbo la Kibamba, yupo mzee mmoja mstaafu wiki moja iliyopita aliniandikia barua, akaniambia naomba peleka wazo langu Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama anafanya kazi kubwa, ndiye Rais wetu wa kwanza mwanamke, kwa nini tusifikie sarafu yetu ya nchi ikabeba sura ya Mama Samia Suluhu Hassan? Najua tuliwekeana utaratibu na marais wetu huyu ni wa sita, marais wawili tu ndio wanaoonekana, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi. Tufikie maamuzi Rais wetu wa kwanza mwanamke kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye aingie kwenye sarafu ya fedha zetu, haya si maneno yangu ni maneno ya wananchi wangu toka jimbo la Kibamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitachangia maeneo mawili mpaka matatu muda ukiniruhusu kwa haraka. Eneo la kwanza ni eneo ambalo linahusu utumishi kwa ujumla wake lakini katika idara nataka nizungumze kidogo idara ya uhasibu pamoja na fedha. Kumekuwa na changamoto sana, na nimewahi kuuliza swali la msingi hapa kama mwaka na nusu uliopita juu ya idara hii. Inaonekana idara ya fedha na uhasibu ndicho kiini cha hati safi na hati chafu. Wakuu wa ofisi, kwa maana ya accounting officers wanapopata hati safi wanasifiwa lakini inapopatikana chafu hawa ndio wanaoshikwa; hawa wahasibu na wakaguzi wa fedha walioandaa hesabu, lakini kuna jambo huku ambalo ndilo linasababisha ambalo leo likieleweka tena inawezekana ikalisaidia Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, idara hii mara nyingi katika sekritarieti za mikoa na wizara zetu na hizi tunaita idara zinazojitegemea, zote hizi zina wahasibu wakuu; lakini pia kuna vitengo. Sasa wakuu wa vitengo wana changamoto sana. Kwanza wanakuwa hawawi involved vizuri kwenye menejimenti, hilo la kwanza; lakini la pili hawa wote wanakuwa ni ma chief accountants. Ukiwa na tofauti na wakuu wa idara, kwa mfano idara ya rasilimali watu, tuna wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu lakini ziada wana wasaidizi, mkurugenzi utawala, mkurugenzi rasilimali watu, wamegawanyika wawili, wasaidizi hao, lakini unaenda mipango, Mkurugenzi wa Mipango ana wasaidizi, mkurugenzi upande fulani, mkurugenzi upande fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokwenda kwa uhasibu unakuta mhasibu mkuu peke yake; anahangaika na mambo ya malipo, kama payment anahangaika na mambo ya revenue kama mapato, ni jambo gumu na kubwa sana. Mkumbuke tulikotoka tulikuwa tunatumia manual hata kwenye kufunga hesabu, lakini leo unapofunga hesabu Tanzania ndivyo wanavyofunga hesabu Marekani na Uingereza, kwa standard moja. Sasa kwa nini tunaona kazi zao hizi ni ndogo? Kwa hiyo ni vizuri tupandishe hadhi kwenye hizi ziwe idara, muwape wawe wakurugenzi wa fedha na utawala lakini pia wawe na wakurugenzi wasaidizi upande wa fedha na upande wa utawala. Kwa kufanya hivyo tutapunguza sana na kwa kiwango kikubwa hoja za ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mhasibu mkuu yupo peke yake na anafanya kazi peke yake, niliona hilo niliweke hivyo. Na, hata kama hatutaki kwenda kuibadilisha kuwa idara basi mhasibu mkuu kimuundo awe na wasaidiizi. Kuwe na mhasibu mkuu msaidizi kimuundo kwenye upande mmoja wa mapato na upande mmoja wa matumizi. Ikiwa hivyo tutasaidiwa sana kwenye kufunga hesabu vizuri na kuondoa hoja ya ukaguzi. Niliona hilo niliweke katika sura hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu ajira portal, limesemwa na wengine. Mimi mwanzo nilikuwa na mawazo, tuliko toka zamani ilikuwa kila taasisi accounting officer anaweza kuajiri lakini tukaja kwenye huu mfumo mzuri tukajua utatusaidia. Hata hivyo nje kuna manung’uniko mengi sana juu ya jambo ambalo mimi nilijua garbage inn garbage out; kwamba tunachokiingiza process mle iwe ni fair na nje pia tutakutana na jambo zuri, lakini leo mambo ya hovyo tu bado yanatokea kaka yangu Simbachawene. Tunaitegemea ajira portal lakini ukiichungulia, amesema Engineer Chiwelesa, unaona kabila limesimama pale, unaliona kabisa. Si hivyo tu unaona ukanda, na inatokea kwenye ajira portal tunayoiamini lakini ziada inatokea sura za viongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unamwona Mheshimiwa Simbachawene moja kwa moja kwenye matokeo ya wale wanaoajiriwa, unamwona Mheshimiwa Kikwete moja kwa moja, natolea mifano tu. Hii haiwezi kusaidia. Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wakurugenzi ndio sura ya ajira inayotembea. Mimi sitaki tuondoke kwenye ajira portal bali tui-strengthen. Waheshimiwa Wabunge wengi wametoa ushauri, na mimi ni mmoja wapo, kwamba ikibidi twende kwenye majimbo ili mimi wale wanaonitumia message na kadhalika niwaone. Hata kama wataenda kufanya kazi Mbeya, Sumbawanga lakini hawa wanatokea Wilaya ya Ubungo, hiyo itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa haraka. Nimeona hapa, liko jambo la idara ya kumbukumbu na nyaraka za Taifa, nimesoma nikafurahi sana. Humu ndani wenzetu wanatuambia ni kama mradi na fedha walizozipata wamejaribu kutafuta nyaraka kwa kuhoji familia na watu, walimu, waasisi wetu, wanatamkwa waasisi wawili humu. Anatamkwa mhasisi wetu Karume kwa upande wa Zanzibar na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa ujumla ndio waasisi wetu. Lakini changamoto ya humu maandishi yanaonesha historia zao zimetafutwa hata kabla ya uhuru tangu wanasoma na Sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vizazi vya mwisho vya kujua historia ya nchi yetu ni sisi. Tukiondoka sisi wajukuu na watoto wetu hawatajua tena kwenye hili, na ndiyo maana wanaenda kwa kuchoka, watajua watu wawili lakini sio kweli. Uhuru wanchi hii umepatikana na wazee wetu tunawajua. Nakutajia na majukumu yao, Kasela Bantu hakuna mtu asiye mjua. Huyu ndiye mwaka 1954 aliyeshawishi kikao cha TANU kifanyike ili kuanzishwa kutoka Tanganyika African Association TAA, iliyoanzishwa 1929-1954. Kuna Abulwahid Sykes tangu mwaka 1929 alikuwa na TAA hadi 1954. Yeye ndiye aliachia kiti akamwachia Mwalimu Julius Nyerere tangu TAA kuanzishwa hadi TANU. Kuna Alhaj Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu katibu Mkuu wa Kwanza wa TANU, kwa nini tunaacha haya? Vilevile kuna mzee Dothan Azizi, Waheshimiwa Wabunge lazima niwaambie, huyu ndiye aliyetoa land rover yake ikatembea kwa ajili ya kutafuta kura za TANU. Si hivyo tu, pia kuna akina Mzee Rupia, Bibi Titi Mohammed; na juzi nilimfurahia sana Mheshimiwa Mchengerwa, na akina mama mmeanza kukubali na kukumbuka kwamba huyu ndiye mama wa Taifa sasa, lakini walisahaulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri ukija utuambie, hizi nyaraka zenu juu ya wengine wote ambao walisababisha hao wakafahamika. Mimi nataka niwaambie tu wala si success story kama ndugu yangu Chief Kunambi anavyosema, lakini nikikumbuka sana, Mwalimu Nyerere anatoka Pugu alikaa pale mnaita Aggrey kwenye nyumba ya Mwinshehe Manga Mtemvu, babu huyo, akiwa anakunywa kahawa na kadhalika, kwenda Kariakoo Shimoni. Hii nchi lazima watu hawa wafahamike na kutambulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti,lakini mwisho sana kwa umuhimu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Watumishi mmewafurahisha, mmeanzisha PEPMIS na PIPMIS, mifumo miwili; ya watumishi na ya public institutions itawasaidia sasa hivi kuna hali mbaya sana. Mimi huwa sipendi kuongelea kwingine kwenye nchi hii. Wilaya ya Ubungo tunayotokea leo kunawazuia sana watumishi ndiyo maana mmeziona issue za mkaguzi wa nje, mambo ya hovyo sana; lakini maana yake kuna watu wameishi mle muda mrefu. Nendeni mkaangalie muone walio overstay muwatoe, si lazima niwataje majina kama Wabunge wengine wanavyofanya hapa, sihitaji kutaja jina la mtu mle ndani kwenye taasisi mimi ninayoiongoza, Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo. Nendeni mkaone shida iko wapi ili muweze kutusafishia mazingira hayo Mheshimiwa Simbachawene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi naunga mkono hoja iliyopo mezani, ahsante. (Makofi)