Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia katika mjadala wetu huu muhimu wa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwanza kwa kuwapongeza Watendaji wa Wizara hii kwa kuanza na Mheshimiwa Waziri ambaye kwanza amepewa majukumu haya kwa muda mfupi uliopita, nadhani haizidi hata mwenzi mmoja lakini anaonekana kuyamudu vizuri majukumu yake na hata hotuba yake ilikuwa nzuri pamoja na Naibu wake pia ni kijana mwenzetu tuna imani naye, kwa hiyo tunawatakia kila la kheri kwenye utendaji wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Katibu Mkuu wa Wizara naye ni kijana mwenzetu, tunaamini kwamba kwa upya wao huo, tunatarajia mambo mengi mazuri yanaenda kutekelezeka kwa maana ya kwamba utakuwa ni utumishi usiozingatia mazoea, siyo utumishi unaofanya kazi kwa mazoea, tunataka creativity tunataka tunaone mambo mapya tunayoyazungumza hapa yanafanyiwa kazi na tunataka tuone mabadiliko, waboreshe utumishi, waboreshe utendaji katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo kubwa moja ambalo lilikuwa kwenye moyo wangu kuhusu mafao kwa wastaafu hasa hasa kwenye eneo la kikokotoo. Ninamshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambae aliridhia kikokotoo hiki kutoka kwenye asilimia 25 kwenda kwenye asilimia 33. Jambo hili bado lina manung’uniko kwenye eneo la utekelezaji, watumishi hasa wastaafu bado wana malalamiko kwenye kiwango wanachopewa cha mafao lakini pia kumekuwa na usumbufu mkubwa baada ya kuunganisha ile mifuko ya jamii liliyokuwa mitano kwenda kwenye mfuko mmoja uliobaki, hivi sasa kumekuwa na malalamiko mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi anakwenda pale ile filling system ya taarifa zake ni mbovu, anaambiwa wewe ulikuwa LAPF sisi PSSF hatuna taarifa zako, anakwenda anaambiwa nenda rudi, hivi na ni watu wazima wazee tunaotarajia waheshimike na wahudumiwe ipasavyo, ninaomba tuhakikishe tunaboresha huduma kwa wastaafu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kile kiwango ambacho kiliridhiwa walipokaa waajiri, Serikali pamoja na kile Chama cha Wafanyakazi kwamba iwe asilimia 33 bado jambo hili watumishi hawajaridhika nalo walio wengi. Naomba niwe very sincere nizungumze kile kulichopo moyoni mwangu na sisi tuko kwa wananchi, tunaishi na wananchi hawa wanaostaafu ndiyo wanarudi wanakuwa wapigakura wetu na tuna watarajia waje watupigie kura 2025 watampigia kura Mheshimiwa Samia watatupia kura na sisi wote tulioko hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana jambo lirudiwe tena liende kwenye majadiliano liangaliwe upya, yale malalamiko mapungufu taliyopo yakafanyiwe kazi, wastaafu wanapata taabu, naomba lifanyiwe kazi mapungufu yaliyopo yatatuliwe ili wastaafu hawa nao waweze kunufaika na waweze kuishi vizuri maisha yao ya ustaafu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili jambo la ajira ambalo tumekuwa tukulizungumza sana hapa Bungeni ambao ni mjadala mkubwa hivi sasa. Kwenye eneo la ajira hapa tuna wataalam bobezi hapa, wakiwemo walimu wetu waliotufundisha vyuo vikuu, walitufundisha kuajiri kwa kuzingatia sifa kwa kuondokana mambo ya nepotism, tuzingatie bureaucratic systems, kwa kuajiri kupitia nepotism mambo ya udugu, kufahamiana huyu ni mtoto wa fulani, huu ni ushamba, huu ni utumishi wa kishamba, mtu mshamba ambae hajastaarabika ataenda kumuangalia ndugu yake badala ya kuzingatia sifa. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakemea kabisa wale wanaoajiri watu kwa kuangalia nyuso badala ya kuangalia sifa walizonazo, hili tutaliepuka endapo tutaenda kuondokana na kufanya interview kwa face to face huu utaratibu uliopo hivi sasa wa kuwakusanya Watanzania kutoka Mtwara, kutoka Katavi kutoka Mwanza huko Kagera, kutoka sijui wapi Ukerewe, kuwalete Dodoma kuja kufanya interview ni mambo ya kishamba haya (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende sasa kwenye kuzingatia TEHAMA, sasa hivi wenzetu wanaajiri kwa kutumia kompyuta. Kama watoto walienda Vyuo Vikuu kwa ku-apply kwenye kompyuta huko vijijini mwao, kwa nini wasifanye hizi interview au wasi-apply kazi kwa kupitia kompyuta hukohuko waliko kwenye maeneo yao tuepuke gharama, tuepuke usumbufu, tuwasaidie Watanzania hawa masikini wanaotaka kujikomboa kwa kutumia vyeti vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu utaratibu wa kuajiri hivi sasa naomba tuzingatie kompyuta, tu-computerize mifumo yetu. Tunaweza kufanya interview kwenye Mikoa yetu ukawa ni utaratibu ambao uko fair, ukam-accommodate kila mtu, tena kwa kuzingatia sifa zao. Kama tuliwaita vyuoni kwa kutumia kompyuta tena hukohuko kwenye vijiji wanakotoka kwa nini leo tunapotaka kuwaajiri tunashindwa kutumia kompyuta, kwa nini hatuaminiani shida iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye eneo la ajira hizi kelele hazitaisha endapo tutaendelea na ule ukale wa utaratibu tunaoutumia kwenye ajira. Malalamiko yataendela kuwepo, tutaendela kulaumiana bila sababu. Kwa hiyo, ninashauri hapa pamoja na kutumia hizi TEHAMA pia tuunde timu ya kushauri. Tunao wataalam, tunao watu bobezi Maprofesa wasomi wazuri, kwa nini hatutaki kutumia watu hawa watushauri ipasavyo ili tuweze kuboresha utumishi, tuweze kupata watumishi wazuri wanaoweza kwenda kukutumikia ipasavyo kwenye utumishi wetu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine..
MWENYEKITI: Mheshimiwa...
MHE. ABEI R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu watumishi. Tuna vijana wanatembea na bahasha mitaani mpaka wanachoka, viatu yaani wanatembea kama vile vichaa, hata nguo wanashindwa kufua, hawana sabuni hawana nini, lakini tunalalamika tunao upungufu wa watumishi tatizo liko wapi? Kwa nini tunashindwa kuajiri watumishi wanaotosha wakatumikia watu wetu kule vijijini?
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ramadhani Ighondo muda wako umekwisha.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja ninaomba tuajiri watu wakatumikie nchi, vijana wasomi wapo. (Makofi)