Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Kasalali Emmanuel Mageni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya. Pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia nafasi za ajiri zaidi ya 21,000 ni jambo jema na ni jambo la kupewa heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene kwa nafasi hii aliyopewa na kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika Wizara mbalimbali alizopita na ninaamini Wizara hii imepata mtu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Naibu wa Waziri Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, amekuwa ni msaada na kiongozi wa kujituma. Hongera sana Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wengine walivyotangulia kumpongeza Mheshimiwa Jenista Mhagama, Seneta, Waziri mzoefu, mwenye heshima, na anayejituma kufanya kazi yake vizuri; Mheshimiwa Waziri, hongera sana kwa njia uliyoiacha kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kabla sijaenda mbali, naunga mkono bajeti, kwa sababu naamini watu ninaoenda kuwashauri, watanisikiliza na watafanyia kazi ushauri wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, nataka nitoe takwimu halisi za upungufu wa watumishi kwenye Jimbo la Sumve. Jimbo la Sumve hivi ninavyozungumza ni moja ya majimbo ambayo yako vijijini kwa asilimia mia moja. Ni majimbo ambayo yanakumbana na watumishi kupangiwa kazi na kuanza kuomba uhamisho siku wameanza kazi. Majimbo haya yanatakiwa yaangaliwe kwa jicho la pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Sumve ninavyozungumza sasa hivi, tuna upungufu wa walimu wa shule za msingi zaidi ya 1,311, lakini walimu wa shule za sekondari zaidi ya 318. Kwenye Jimbo la Sumve, kuna shule kama Nyang’ingi, shule nzima ina walimu watano. Kuna shule kama Bukala, shule nzima ina walimu saba. Hali ya upatikanaji ya watumishi ni mbaya kwenye maeneo ya vijijini. Serikali bado ina kazi kubwa ya kufanya kwenye sekta hii ya utumishi. Bado tuna upungufu mkubwa wa watumishi, kwa hiyo tunaomba Wizara iliangalie hili kwa jicho la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie kama ambavyo wengi wamesema kuhusu mfumo wetu wa ajira. Niliwahi kusema hapa na wengine wamesema. Tunalo tatizo kubwa sasa hivi kwenye nchi yetu la wananchi kupoteza imani na mfumo wetu wa ajira Serikalini; na Wabunge wote wamesema humu. Tunazo meseji mpaka zimejaa kwenye simu, za watu kuomba tuwasaidie kupata kazi Serikalini. Watu wamehamisha imani kwa Wabunge, wameondoa imani kwenye Mfumo wa Serikali wa Ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi tunaowaongoza, wana akili na wanajiongeza. Wanajiongeza kutokana na wanayoyaona. Mfumo wetu wa ajira umekuwa ni mfumo wenye usiri mkubwa sana. Watu wanaomba kwenye Tume ya Ajira; sijui kuna kitu kinaitwa sijui kanzidata na story nyingine nyingi. Watu wanamwambia mtu ameomba, aliyekosa amewekwa kwenye kanzidata, mwingine amepewa ajira. Baadaye tena ajira ile ile hawatumii tena kanzidata kumpa ajira huyu waliyemweka, wanatangaza tena ajira nyingine kwenye jambo lile lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamefika wakati wamegundua kwamba mfumo wa ajira ni wa dili. Sasa kama kweli mfumo wa ajira ni wa dili, ni hatari sana. Tutakuwa tunapokea Ripoti za CAG hapa, watu wametushangaza, kwa sababu wameingia kwa dili. Kwa hiyo, lazima mfumo huu wa ajira tuuangalie kwa namna nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatari kubwa sasa hivi, leo naongea kwa Wizara ya Utumishi, lakini imani ya wananchi mpaka kwenye mfumo wa ajira kwenye majeshi ni ndogo sana. Yaani wananchi wanatupa ujumbe kwamba huko tuna askari wa dili. Sasa nchi kama tunataka hivi ni lazima tujifikirie, yaani kuna kitu kwenye mfumo wa ajira wananchi wameshaondoa imani. Serikali lazima ijitazame na ijiangalie mara mbili. Wananchi bado hawatuamini. Sasa tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kushauri hapa, ajira zikishushwa chini ni rahisi zaidi watu kuwa na imani. Maana watu wamesema hapa, hata ajira hizi kuna maeneo, mimi Mbunge wa Sumve nikikwambia ni wangapi wameajiriwa Sumve, siwezi kusema, maana sijui. Kwa sababu mambo haya yanafanyika juu juu tu. Sasa lazima ifike wakati uwazi uongezeke ili kuwe na mambo yanayoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira hii siyo kwamba tunafanyia tu siasa. Mfano, leo tunasema kuna mfumo ambao TAMISEMI wamesema hapa, ajira wataangalia watu wa 2015, wengine hawawaangalii. Mtu wa 2015 leo ana miaka minane hafanyi kazi yoyote. Hawana database ya watu wanaojitolea. Watu wanaojitolea wanachukuliwa kama vile hamna wanachokifanya. Sasa kama Serikali yetu haina database ya watu wanaofundisha watoto wetu, inafanya kazi gani? Yaani sisi tumepeleka watoto shuleni, ninyi hamjui wanafundishwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanajitolea huko, wanajiandikisha Walimu Wakuu, kila mwezi wanapeleka ripoti ya watu walioko kwenye shule, kwamba nina walimu kiasi kadhaa. Kumbe tunafanya formality, ni mazoea tu, mambo ya kishikaji. Lazima tufike wakati vitu vya msingi tulivyokubaliana vifuatwe. Watu wamejitolea na mnawajua, taarifa za watu wanaojitolea zinajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali, hizi nafasi zilizotolewa 21,000 tusiwe na haraka nazo sana, ni nyingi sana, tuzitengenezee mfumo mzuri ili watu wote wapate wanaostahili na zije kuwa na tija. Kwani tuna haraka gani? Kwani lazima tuajiri sasa hivi, si Rais ameshatupa. Hebu tulieni, tusikilizeni tuwaambie, kwamba watu wanaojitolea wanajulikana. Story ya kwamba hawajulikani, ni kuidhalilisha Serikali. Walimu Wakuu wanajua hawa watu, na ripoti za kila mwezi kwa Maafisa Elimu zinapelekwa. Leo mnasimama hapa mnatuambia hamuwajui, mnafanya kazi gani sasa hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike wakati tusimamishe hii ajira ya watu 21,000, tushauriane humu, wote ni watu wazima, tumetumwa na wananchi, tukubaliane nani anaajiriwa, na kwa sifa ipi? Kwa sababu tukiendelea na utaratibu huu, tutaendelea kuwa na watu tu tunaajiri, tunaajiri kwa ajili ya kujifurahisha, lakini watu bora tunawaacha nje, lakini na wananchi wanakosa imani na mfumo wetu wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nishauri jambo lingine. Kuna jambo hapa linaitwa kikotoo. Serikali iwape watu fedha zao. Mtu amefanya kazi kwa muda mrefu, amepokea mshahara wake, mlikuwa hamumtunzii, ilikuwa hamhusiki chochote na mshahara wake, leo anastaafu zinakuja story kwamba hawezi kutunza hela yake. Wapeni watu hela zao. Wapeni watu hela zao wapambane nazo huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya huko. Kweli kabisa! Humu tunaweza tukakaa tukawa tunafikiri hali ni nzuri; kuhusu wastaafu, wastaafu masikini ni wazee wetu, nasi ni wastaafu watarajiwa, hawariziki na hela yao kutunziwa. Wakitunziwa, hatujui mtu kesho na keshokutwa hayupo, inalipwaje? Tufike wakati mtu apewa hela yake, amefanya kazi kwa heshima kwenye nchi hii, aende akafanye kazi yake vizuri. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kasalali Mageni, kuna taarifa kutoka kwa Waziri, Mheshimiwa Profesa Ndalichako.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilikuwa naomba nimpe taarifa kaka yangu, Mheshimiwa Kasalali Mageni ambaye ninamheshimu sana, na anachangia mchango mzuri, lakini naomba tu hili jambo lisije likapotoshwa kwamba Serikali inaona watu hawawezi kutunza fedha zao. Fedha ambazo mtu analipwa za mkupuo; na nilishafanya semina hata kwa Wabunge; anapata fedha nyingi kuliko hata zile ambazo amechangia katika miaka yake yote ya utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokizungumzia mafao ya mkupuo, ni ile pensheni ambayo mtu anaipata ambayo makisio ya umri wa kuishi baada ya kustaafu tumekadiria ni miaka 12 na nusu. Kwa hiyo, tunafanya makisio ya fedha yote ta mtu kustaafu halafu katika fedha ile ndiyo tunampa mkupuo wa asilimia 33. Ni tofauti na kile ambacho mtu anakuwa amechangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona tu kaka yangu amechangia vizuri, nimpe hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri kwa taarifa, na muda wa mchangiaji umekwisha.

Ninakuongezea dakika moja na nusu ili uweze kuhitimisha hoja yako Mheshimiwa.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri,

Mwalimu wangu, nimepokea taarifa yako. Ila nataka tu kusema, hao wanaolalamika siyo kwamba vichwa vyao vimekatwa, wanaona kwamba jambo hili siyo sawa. Nasi kazi yetu ni kuwaambia kwamba wale wastaafu wanalalamika. Wanapolalamika, ni kwetu. Sasa kama mtu anapewa hela nyingi zaidi halafu bado analalamika, sijui, labda wastaafu wetu wana hali ngumu sana za kufikiri; lakini kama ni kweli zile walizotutumikia mpaka nchi yetu imefika hapa, ukweli ni kwamba wanalalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuone namna ya kuwapa hela zao wachukue wakapambane nazo. Tusiwakadirie umri wa kuishi, kila mmoja Mungu ndio anakadiria umri wetu wa kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninamshukuru Mwalimu wangu wa Measurement and Evaluation, Profesa, nakuheshimu sana, lakini wananchi wanasema kwamba hawaridhiki, wanaomba mbadilishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Kicheko/Makofi)