Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. PROFESA KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, na kwa kweli nianze mchango wangu kwa kukupongeza, unaendesha kikao vizuri sana. Upo vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kwa kweli kupongeza sana hatua ya Serikali na Mheshimiwa Rais kutoa kibali cha ajira 21,000. Jambo hili siyo la kupongeza tu kwa maana ya utaratibu wa kawaida. Katika kipindi ambacho dunia nzima ina changamoto ya kiuchumi, katika kipindi ambacho kuna nchi tunavyozungumza leo zimeshindwa kulipa mishahara ya watumishi, katika nchi ambazo zimeshindwa kulipa mishahara ya Waheshimiwa Wabunge, lakini sisi siyo kwamba tunalipa tu mishahara, tunaajiri watumishi wapya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili haliwezi kupita bila kuzungumziwa vizuri. Ni jambo kubwa, na ni jambo jema. Tunatambua kwamba idadi ya ajira hizi siyo kwamba zinakidhi, lakini lazima kila hatua tuone kwamba ni hatua na sisi kama Wabunge lazima tupongeze na kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tukishashukuru tunajenga hoja ya kuongezewa zaidi kwa hiyo hilo ni jambo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika hoja hiyohiyo, viongozi hufanya mambo manne; hujenga, huboresha, hufanya mambo mapya na hurekebisha pale ambapo walipoishia wenzao hapakukaa vizuri. Namimi nataka nichukue nafasi hii, hata hili la kuajiri ni hatua kubwa ya Mheshimiwa Rais ya kurekebisha kwa sababu miaka mitano, sita, saba nchi hii ilikuwa haiajari watumishi. Hawa waliyotoka vyuo vikuu wanafahamu, miaka ya tisini, miaka kumi Serikali iliacha kuajiri watumishi hasa katika vyuo vikuu kwa kitendo hiki ni hatua nzuri ya kurekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika muktadha huohuo nataka niombe Serikali warekebishe mambo mengine mengi lakini hasa matatu katika utumishi wa umma, na nataka kuzungumzia utumishi katika vyuo vikuu; kwa sababu pia kwenye Jimbo la Ubungo pale kuna Chuo Kikuu cha Kwanza Tanzania (Chuo Kikuu cha Dar es salaam) ambapo nimewahi kupata bahati ya kukitumikia; kwa sababu kufanya kazi chuo kikuu kama Profesa ni bahati kubwa na mshukuru Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa chuo kikuu kwa walimu ni uhuru wa kitaaluma (academic freedom). Yaani mwalimu chuo kikuu lazima anapokaa pale awe na uhuru wa kufundisha na kufanya utafiti na kusambaza maarifa bila woga wa kufikili kwamba hataingiliwa, ataonewa, atashughulikiwa, atabaguliwa au atanyanyaswa; huu ni msingi ambao unaongoza vyuo Vikuu Vyote Duniani. Ni kwa sababu vyuo vikuu duniani vinakuwa na sheria zake; na sisi tungekuwa na sheria ya vyuo vikuu, kila chuo kingekuwa na sheria yake. Hata hivyo mwaka 2005 Bunge likatunga Sheria linaitwa Universities Act, Sheria Na. 07 ya Mwaka 2005, lengo ni kulinda uhuru wa kitaaluma katika vyuo vikuu. Na vyuo vikuu vimeanzisha vyombo vyao vya kujiendesha na kujitawala. Kwa hiyo kazi kubwa ya Serikali imekuwa ni kutoa sera na muelekeo na kutoa rasilimali lakini uendeshaji wa vyuo vikuu unakuwa ndani ya vyuo vikuu vyenyewe. Kwa hiyo kuna vyombo viwili vikubwa; Kuna Baraza la Chuo Kikuu na kuna Senate, Senate ni kama Bunge hili. Hili ni jambo la msingi sana ambalo lazima tulielewe, na hivyo hivyo duniani. Sasa hizi nyenzo zimewekwa ili vyuo vikuu vijiendeshe na vilinde uhuru wa kitaaluma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo moja la msingi sana ambalo lazima tulirekebishe ni kuepusha urasimu wa kawaida kuuingiza vyuo vikuu, bureaucracy ya kiserikali. Kwa mfano vyuo vikuu duniani na hapa Tanzania siku zote huwa vinaajiri watumishi wake; na ndiyo maana kwenye sheria yetu ambayo nimeisoma function namba 05 ya mabaraza ya vyuo vikuu is to appoint officers of the institutions. Maana yake waajiri wa vyuo vikuu ni mabaraza ya vyuo vikuu, na ajira za chuo kikuu ni za chuo husika. Ndivyo ilivyo duniani, ndiyo maana inaitwa university, yaani universal from the word universal). Kwamba misingi ya vyuo vikuu ambayo inafanana duniani kote. Sasa nataka niulize, na mtusaidie kulirekebisha jambo hili. Katika miaka ya hivi karibuni, nadhani kuanzia Mwaka 2015, 2016, tumeamua ajira za vyuo vyuo vikuu zinaendeshwa na Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira. Hili jambo ni peculiar kwa Tanzania, halipo vyuo vikuu vyovyote duniani. Yaani huwezi; na naona mmeanza kuhamisha walimu kutoka chuo kimoja kwenda chuo kingine. Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Oxford akitaka kwenda Cambridge ana- apply, anaomba aajiriwe na Cambridge; lakini huwezi kukuta Serikali ina muamisha huyo mtu kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge kwenda Oxford, hiyo Duniani haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili jambo lazima mliangalie, muachie vyombo ambavyo tumeunda kisheria kufanya ajira. Hata hizi ajira za walimu ambazo tunalizungumza hapa, tunaona kama jambo la kawaida, kwamba wanaajiri Ofisi ya Rais – TAMISEMI lakini sheria haisemi hivyo. Sheria ya Ajira za Walimu ipo katika Tanzania Teacher’s Service Commission, na ipo very clear. Moja ya majukumu ya Commission TSC jukumu namba 03 is to appoint, promote and discipline teachers. Kwa hiyo Waziri ana jukumu la kurebisha hapa; na Mheshimiwa Rais moja ya ajenda yake nikufanya maboresho na marekebisho tumsaidie kurekebisha. Moja ya marekebisho ni kwamba Utumishi waache vyombo vya kisheria vifanye kazi zake. (Makofi)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Taarifa Mwenyekiti.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere taarifa.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa maelezo ya mzungumzaji, kwamba kuna Sheria ya Kuajiri Walimu kupitia Tume ya Walimu tunaomba ajira inayoendelea sasa hivi ifutwe tufate sheria iliyopo sasa hivi. (Makofi/Vicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kitila Mkumbo, unapokea Taarifa?

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Nimeipokea ni muhimu Serikali ikafanya marekebisho na maboresho. Kama sheria hizi ambazo tunatunga mnaona hazifanyi kazi leteni tufanye mabadiliko, ni jambo la msingi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambalo linaendana na hilo, na nataka niweke msisitizo kabisa kabisa; mnaanza kuhamisha walimu kutoka vyuo vikuu kwenda chuo kikuu kingine; hili nimeisha lisema siyo sahihi. Ajira za walimu ni za chuo husika. Kitila Mkumbo akita kwenda chuo kikuu cha UDOM ana apply. Sasa nyie mmehamisha walimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam; kwa mfano a rarely professor environmental economics mmemtoa pale mkaenda kumtupa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia ambacho hakina wanafunzi, yupo pale hana wanafunzi. This is a professor ambayo alikuwa anafanya kazi vizuri sana pale chou kikuu. Mmemuamisha mwalimu ametoka PHD resource assessment ana uchungu wa kufanya kazi amekaa siku mbili tatu ana hamishwa kwenye Chuo cha Maji, kufanya nini? Kwa hiyo kaka yangu Ndugu yangu Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kitila Mkumbo, nakuongeza dakika nne ili uweze kumalizia hoja yako. (Makofi)

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ubarikiwe sana, uko vizuri. Hilo nadhani limeeleweka; Mheshimiwa George Simbachawene tunakuheshimu, umefanya kazi nzuri naomba hili jambo ulifanyie kazi ulirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni ajira za mikataba kwa maprofesa wa vyuo vikuu. Tulikuwa na utaratibu mzuri sana, Profesa akisha ku–retire chuo kikuu, vyuo vikuu vinamfanyia tathimini. Akiwa bado ana nguvu na anafanya kazi zake kitaaluma vizuri anapewa mkataba wa miaka miwili miwili mpaka pale tutakapoona kwamba afya yake ya mwili na kiakili imechoka. Jambo hili tukaliondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ipo hivi; profesa si kama wana michezo, ambaye kadri umri unavyokwenda anazidi kuchoka. Uprofesa ni kama wine. Wine inavyokaa muda mrefu ndivyo inavyozidi kunoga, profesa unavyozidi kukaa muda mrefu anazidi kubobea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na maprofesa wengi, wanafahamu Profesa Ndalichako, maprofesa wengi wanapata uprofesa late 50’s na wameongezewa hadi 60’s. Sisi wengine tuliopata tukiwa na miaka 40 tulibahatisha tu, lakini Maprofesa wengi wanapata Uprofesa miaka 50 na kuendelea. Sasa amemaliza tu profesa ndiyo anaanza kubobea mnamuondoa. Kwa hiyo tunaomba utaratibu wa zamani ambapo Profesa akishakustaafu anapewa mkataba uendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo madhara yake ni nini? Vyuo vikuu vya umma kwa sasa vinaanza kubaki na junior staff. Kwa sababu Maprofesa wote ambao wana– retire Chuo Kikuu cha Dar es salaam wanakwenda kwenye private universities; tunamsaidia nani? Kwa hiyo naomba hili pia Mheshimiwa Waziri aliangalie na alirekebishe lirudishwe kwenye utaratibu ambao ulikuwepo. Kwa sababu tunasema if it is not broken don’t fixed it, kwa sababu ni kitu kizuri kilisaidia nchi yetu, kilisaidia vyuo vikuu vyetu. Utaratibu huu kwa nini uliondolewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuwaombea. Wametufata maprofesa wa siku nyingi ambao waliajiriwa kabla ya mwaka 1978 kabla ya PPF kuanzishwa; hawa watu hawakuwa kwenye mfumo wa pension, waliwekwa katika mfumo wa bima, wanalipwa kitu kinaitwa SSSS (Serious Staff Superannuation Scheme). Hawa maprofesa wameondoka chou kikuu anapata milioni 10, milioni 20. Baadhi yao wameniambia hata ukitaja majina yetu ni sawa tu. Sasa wamebaki maprofesa 180, hawana pension, wapo tu. Jambo hili limieshawasilishwa mara nyingi, Serikali imelipokea, hivyo tunaomba Mheshimiwa George Simbachawene kupitia kiti chako jambo hili ulimalizie ili tutunze heshima ya watu ambao wametumikia katika nchi hili miaka 30, miaka 40 katika utumishi wa vyuo vikuu, ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kusema hayo nimalizie tena kukushukuru na kukupongeza kwa mchango wako naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)