Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mchango wangu utajielekeza kwenye maeneo mawili. Upande wa utawala bora na upande wa masilahi ya watumishi.

Mheshimiwa Spika, kwenye utawala bora, nina ushauri mmoja kwa TAKUKURU, kwa sababu kuna masuala mengine yako wazi kabisa lakini michakato yake inachukua muda mrefu sana. Nakumbuka mwaka 2017/2018 kuna mchakato ulianzishwa pale Jijini Arusha, wenzetu wa boda boda wakaweza kuchangisha fedha kiasi cha shilingi milioni 400 ambazo baadaye zilikuja kuibiwa na baadhi ya watu.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni kwamba, mnamo tarehe 18 Juni, 2021, katika Tawi la NMB Mbagala kuna Mtu anaitwa Maulid, mwingine anaitwa Makongoro, Mwingine anaitwa John F. Fungameza, walikwenda kuchukua fedha kwenye akaunti kiasi cha shilingi 39,500,000. Mnamo tarehe 8 Julai, 2021, kuna mtu mwingine tena ambaye anaitwa John na mwingine anaitwa Edwin, walikwenda kwenye Akaunti na kuchukua fedha kiasi cha shilingi 43,500,000. Mnamo tarehe 31 Agosti, 2021, kwenye Tawi la Kariakoo wakachukua tena Fedha kiasi cha shilingi 43,800,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tena mnamo tarehe 25 Novemba, 2020, kupitia NIDA namba ya T100027912657 walikwenda kuchukua shilingi 15,000,000. Orodha ndefu na inaendelea. Hoja yangu hapa ni kwamba hawa watu wa bodaboda fedha zao zimeibiwa na walioiba fedha wanajulikana, wameenda benki wamechukua fedha na wametoa vitambulisho vya NIDA na wamechukua kwa majina yako. Hata hivyo, toka mwaka 2020 mpaka leo suala hili halijapelekwa Mahakamani na wahusika hawajakamatwa, badala yake inatolewa fursa kwa baadhi ya watu kuanza kuchafua majina ya watu ambao hwahusiki kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Spika, ombi langu, tuwaombe TAKUKURU, najua wanafanya kazi kubwa na wanafanya kazi nzuri. Kama wezi wanajulikana na ushahidi upo, kigugumizi ni cha nini kuhusu kuwakamata na kuwapeleka mahakamani ili kuweza kuondoa changamoto hii kwenye maeneo mengine?

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili, maana hapa ukiangalia fedha zilizochukuliwa ni kiasi cha shilingi 214,500,000. Hizi ni fedha nyingi sana kama zingepatikana zingewasaidia vijana wa bodaboda kuendelea kukopeshana kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili ni kuhusiana na madai ya watumishi. Ukiangalia Jiji la Arusha ulifanyika uhakiki mwaka 2017 wa kuangalia ni watumishi gani ambao walikuwa wanadai masilahi yao. Ukiangalia mfano, kwenye upande shule ya msingi na shule ya sekondari kwenye uhakiki huo, kwenye upande wa likizo kwa upande wa shule za msingi zinadaiwa shilingi 105,000,000; Kwenye upande wa sekondari ni shilingi 94,000,000; jumla ni shilingi milioni 200.141.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa waliokwenda masomoni kwenye shule ya msingi shilingi 2,800,000 na shule za sekondari shilingi 600,000, jumla ni shilingi 3,400,000; Ukienda kwenye matibabu jumla ni shilingi 14,775,000; Ukienda kwenye uhamisho wa watumishi ni shilingi 56,757,000; Ukienda kwenye fedha za kujikimu ni shilingi 2,211,000; Ukienda kwa waliostaafu yaani kuna watu waliostaafu kabla ya mwaka 2017, wamelipwa stahiki zao zote, lakini mpaka leo hawajalipwa fedha za kusafirisha mizigo yao ambazo ni kiasi cha shilingi 26,837,013.94; Kuna ambao walifiwa mpaka leo wanadai shilingi 3,150,000; Kuna ambao wanadai hela zao za mizigo shilingi 12,000,000; Kuna nauli pia kwa ajili ya ajira mpya, mtu ameajiriwa nauli yake ya kumpeleka kituoni hajapewa na asingeenda kituoni pengine angepewa adhabu ya kutokuwa kazini. Wanadai na wenyewe kiasi cha shilingi 998,000 tu; na ukiangalia stahiki za Wakuu wa Idara zenyewe ni shilingi 38,050,000. Kwa hiyo jumla yake ni shilingi 358,420,582.89.

Mheshimiwa Spika, ndio maana tunapoona kwenye Jiji la Arusha kuna ufisadi na wizi tunapiga kelele kwa sababu tunaamini tukidhibiti ule wizi, zile fedha zitakuja kuwasaidia hawa wanyonge ambao wanasaidia kufanya kazi mbalimbali kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni ombi langu, si lazima kila kitu tuchukue fedha kutoka Hazina. Zile halmashauri ambazo zina mapato makubwa kama vile Arusha, Ilala, Mwanza zile za majiji zote, wangepewa maelekezo na utaratibu hela ndogo kama hizi milioni 358 wangezilipa wao wenyewe ili kuwaondolea wananchi wetu kero pamoja na masuala mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia fedha hizi katika ufisadi uliofanyika Arusha zile risiti fake peke yake tu milioni 699 peke yake zingeweza kulipa deni hili na change ingebaki na masuala mengine pia yangeweza kuendelea.

Mheshimiwa Spika, suala lingine pia ambalo ningependa kulizungumzia kuhusiana na watumishi wetu ni kuhusiana na kupanda madaraja kwa watumishi. Kwenye suala la kupanda madaraja, katika hili naomba niipongeze Serikali kwa sababu kwa kweli kuna kazi kubwa imefanyika. Kwa sababu kwanza nafahamu kuna mwongozo wa Serikali ulitoka wa tarehe 27 Machi, 2018 ambao ulielekeza kwamba ukurasa wa pili, kifungu cha 3(b) ulikuwa unasema, kufuta barua za awali za kuwapandisha vyeo na badala yake barua za vyeo hivyo zionyeshe kuwa vyeo vya watumishi hao vinaanza tarehe 1 Aprili, 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tafsiri yake ni kwamba walikuwa wamenyimwa miaka miwili ya kupandishwa mishahara yao. Hata hivyo, bahati nzuri kwa sababu ya usikivu wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeona mwaka huu 2023 tarehe 23 Desemba, umetoka mwongozo wa Serikali ambao umeelekeza watumishi walioathirika na zoezi la uhakiki katika upandishaji vyeo mwaka 2016 ambao walipandishwa kwa makundi mawili ya mwezi Novemba, 2017 na Mwezi Aprili, 2018 na kupanda vyeo walivyonavyo sasa mwezi Mei, 2022, lengo la hatua hii ni kuwezesha uwepo wa msawazisho wa vyeo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni imani yangu kwamba wenzetu Wizara ya Utumishi watahakikisha kwamba wafanyakazi wote hawa kama Serikali ilivyoelekeza, wanaingizwa kwenye utaratibu na wanapata haki zao kama ambavyo Serikali imeelekeza.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kulikuwa na changamoto za jumla, Serikali siku za nyuma imekuwa inapandisha mishahara kutokana na uwezo wake wa kibajeti. Kwa hiyo, sisi ombi letu ni kwamba wasiangalie uwezo wa kibajeti, waangalie kama miaka mitatu imefika watumishi wote wajue mwaka huu wanatakiwa wapandishwe, wapandishwe wote. Kwa sababu, mwaka huu ukipandisha nusu halafu mwakani ukapandisha wengine watakuwa wanatofautiana vyeo na mishahara wakati walianza kazi siku moja na sifa kwa ujumla wake zinafanana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MRISHO M. GAMBO. Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)