Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nikupongeze sana kwa kuweza kusimamia Bunge letu kikamilifu kabisa. Pia nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa Manyoni sisi ametuletea fedha nyingi sana. Vilevile nimshukuru Waziri Kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, lakini vile vile Naibu Waziri Ndugu yangu, Mheshimiwa Ridhiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nina maeneo matatu ningependa kuchangia. Eneo la kwanza linahusu upungufu wa Maaskari na hali ya usalama Manyoni, eneo la pili linahusu upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na muda ukiniruhusu nitachangia kuhusu Standing Orders (Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma).

Mheshimiwa Spika, tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi hususani Maaskari katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na katika Wilaya ya Manyoni. Vile vile, sanjali na hilo, Manyoni kumekuwa na matukio mengi sana ya uhalifu. Tangu 2017 kumekuwa na matukio ya aina tatu ya uhalifu. La kwanza, kumekuwa na matukio ya mauaji, watu wanauawa wanatupwa pale Manyoni Mjini. Pili, kumekuwa na tabia ya kufukua makaburi na kuchukua viungo na vitu mbalimbali. Hali hii imekithiri tangu 2017 tumekuwa na haya matukio.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana RPC wa Mkoa wa Singida na Mkuu wa Mkoa wa Singida, lakini vile vile niishukuru Serikali, hivi karibuni imetuletea Mkuu wa Wilaya mpya Mheshimiwa Kemilembe. Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani amefanya mabadiliko pale Manyoni, ametuletea OCD mpya na amefanya mabadiliko ya Mpelelezi wa Wilaya.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba, tunahitaji sasa Serikali ituongezee watumishi wa Polisi lakini vile vile iangalie kwa ukaribu hali ya usalama wa Manyoni. Wastani kila mwezi mtu mmoja anaokotwa amekufa pale Manyoni Mjini, lakini watu wanafukua makaburi. Siku hizi wananchi wa Manyoni wanalinda makaburi, tukishazika inabidi uweke mlinzi kwa sababu ndani ya siku tatu unakuta makaburi yameshafukuliwa. Kwa hiyo, naomba tuliwezeshe Jeshi la Polisi, wana upungufu wa magari, hawana pikipiki na wana upungufu wa zaidi ya watumishi 10 pale Manyoni. Pia niombe wapeleke timu ikachunguze yale mauaji, kwa nini yale mauaji yanatokea pale Manyoni?

Mheshimiwa Spika, suala la pili, ni suala la upungufu wa watumishi pale Manyoni. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi. Upande wa Afya mahitaji ni watumishi 642, lakini waliopo ni 289 na upungufu ni 353. Mgao wa mwaka jana tulipata watumishi wa afya 33 tu. TAMISEMI wametoa tangazo la kuajiri watumishi, tunaomba na kwa kupitia Waziri wa Utumishi, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni tuangaliwe.

Mheshimiwa Spika, upande wa Walimu mahitaji upande wa sekondari ni 460, waliopo ni 268, upungufu ni takribani 138. Vivyo hivyo hata upande wa shule za msingi. Vilevile kwenye kada zingine, upande wa Uhasibu tuna upungufu mkubwa sana pale tuna Wahasibu watatu tu. Kati ya hao ni Mweka Hazina tu ndio ana CPA, lakini wengine wote hawana CPA. Nimeona hilo nalo niliombe na nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene na Mheshimiwa Naibu Waziri watusaidie tupate watumishi pale Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

Mheshimiwa Spika, upande wa Walimu, mahitaji upande wa Sekondari ni 460 lakini vilevile waliopo ni 268 upungufu ni takribani 138. Vivyo hivyo hata upande wa shule za msingi. Vilevile kada zingine upande wa Uhasibu tuna upungufu mkubwa sana pale, tuna Wahasibu Watatu tu na kati ya hao ni Mwekahazina tu ndiyo ana CPA lakini wengine wote hawana CPA, nimeona hilo nalo niliombe na nimuombe Kaka yangu Simbachawene na Mheshimiwa Naibu Waziri mtusaidie tupate watumishi pale Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la wanaokaimu. Halmashuri ya Wilya ya Manyoni haina Mkurugenzi tangu mwaka jana mwezi wa Nane, tunae anaekaimu. Nilisikia wenzangu wakichangia hapa kanuni ya kukaimu, mtu anakaimu zaidi ya miezi Saba miezi Nane, kwa hiyo niliona nalo hilo tulione pia Wakuu wengi wa Vitengo wanakaimu, kwa hiyo hilo nalo niliona nilichangie.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho naomba nichangie upande wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma. Katika Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma kuna maeneo matatu ningependa kuchangia. Eneo la kwanza kuhusu wazazi tunapofiwa sisi na wazazi watumishi wa umma, wazazi hawawi considered kwenye suala la mazishi, lakini mnajua msiba unapotokea wa mzazi tegemeo kubwa ni kwa mtumishi. Ningeomba Mheshimiwa Waziri hebu liangalieni hili, wazazi wawe considered kwenye suala la kuwahudumia kwenye mazishi, baba, mama anapofariki. Kwa kweli, huwa watumishi wetu wanapata shida sana inapotokea msiba wa mzazi, anaanza kuhangaika kukopa na kadhalika, kwa hiyo hili ni eneo la kwanza ambalo nilidhani ni eneo ambalo tunahitaji kubadilisha zile standing order zetu tuweze kuwa- accommodate wazazi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la mtu kuwa Mkuu wa Idara, taarifa ya CAG inaonesha kwamba maeneo mengi Wakuu wa Idara wanakaimu, wanakaimu kwa sababu ya vigezo vyetu vya mtu kuwa Mkuu wa Idara. Ili mtu awe Mkuu wa Idara anatakiwa awe Afisa Mwandamizi, sasa hicho ni kigezo cha juu sana, lakini huko nyuma tulikaa muda mrefu watu hawajapata promotion.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni nini? nadhani tungeangalia maeneo kwa mfano, kuna kada ambazo ni ngumu sana kupata watu wenye kuwa Waandamizi kwa mfano TEHAMA, Sheria, Manunuzi, hawa watu tuwachukue hata wale wa Grade One ili angalau wawe Wakuu wa Idara nadhani hilo litasaidia sana kuhakikisha kwamba tunakuwa na Wakuu wa Idara ambao wanakidhi vigezo lakini vilevile tutajibu ile hoja ya CAG.

Mheshimiwa Spika, lingine suala la likizo ya uzazi. Katika likizo ya uzazi kuna mambo matatu ningependa kuchangia, kwanza ni pale mama anapojifungua halafu bahati mbaya mtoto akafariki. Standing order inampa siku 42 za kupumzika, lakini jamani siku 42 ni siku chache sana, mama anapojifungua mtoto akafariki bado anakuwa na machungu mengi, mnataka ndani ya siku 42 arudi tena kazini, mimi ningeshauri hata wale mama ambao wanajifungua mtoto anafariki wapewe zilezile siku 84 kwa sababu anakuwa bado anapitia mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu ni kuhusu wanaume, mama amejifungua standing order inasema inampa siku tatu, mama amejifungua kwa operation, siku tatu mwanaume ndiyo anatakiwa amhudumie then aendelee na kazi zingine, nadhani hapa kuna tatizo vilevile kwa hiyo nishauri na yenyewe muiangalie na ningependekeza angalau basi na baba apewe angalau siku Saba ili apate muda mzuri wa ku- take care mke wake wakati huo anauguza vidonda vya operation. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la mamlaka ya nidhamu katika Halmashauri zetu kuna mkanganyiko. Kanuni zilizorekebishwa zinasema mamlaka ya nidhamu ni Mkurugenzi lakini sheria inasema mamlaka ya nidhamu ni Baraza la Madiwani. Sasa hapa ningeshauri iangaliwe hii kama tumeamua mamlaka ya nidhamu katika Halmashauri zetu awe Mkurugenzi kote isomeke Mkurugenzi, lakini kama tunasema mamlaka ya nidhamu katika Halmashauri zetu wawe Madiwani basi kote kuwe Madiwani.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nakushukuru sana na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)