Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Shukrani zangu ziambatane na pongezi za kukupongeza wewe binafsi, kwamba unawatia moyo wazazi wengi ambao wamewekeza kwa watoto wa kike. Wanawaambia wasome kwa bidii ili siku moja wawe ma-lecturer kama wewe; wanawaambia wasome kwa bidii ili siku moja wawe Wanasheria kama wewe; wawe wanasiasa kama wewe na ikiwekezekana waweze kushika Mhimili kama wewe ulivyo. Kwa hiyo, unatutia moyo sana mabinti wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kabisa kwa kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. Kwa dhati ya moyo wangu kama mwakilishi wa wana-Momba, naishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Hassan Suluhu kwa miradi yote ya maendeleo ambayo tumepewa ndani ya Jimbo la Momba. Ingekuwa naruhusiwa kupiga magoti hapa, ningepiga goti la heshima la kuonesha shukrani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu leo utajielekeza kwenye kuwasemea vijana wa Kitanzania, hususan kwenye suala la ajira. Ajira kwa vijana ni suala la usalama kama ambavyo tunavyoangalia usalama wa afya zetu na usalama wa chakula. Vijana ambao wanaajiriwa katika kipindi hiki, miaka 20 ijayo ndio viongozi wakubwa wa mhimili kama wewe, ndio atapatikana Mheshimiwa Rais hapo, Baraza la Mawaziri, na Wabunge kama sisi. Kwa hiyo, ni usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ajira nchini kwetu, lakini changamoto ya ajira siyo issue, ila ni namna ambavyo ajira hizi zinagawanywa; ni

namna ambavyo ajira hizi zinaenda zikiwa na usawa sawia, especially kwa sisi ambao tunatoka vijijini ambako hakuna fursa nyingi za biashara, hakuna makampuni binafsi ambayo tunajua kwamba watu wanaweza wakaajiriwa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba changamoto ya ajira inawezekana inasababishwa na jambo fulani. Kwenye uchumi kuna kitu kinaitwa demand and supply. Supply inapokuwa low au inapokuwa limited, demand ikiwa high inapelekea bei kupanda kwa kitu husika. Kwa hiyo, mahitaji yanapoongezeka, bei inapokuwa juu, lakini vitu hivi huwa vinaboreshwa, kwa sababu watu wanalipia gharama kubwa kupata hicho kitu.

Mheshimiwa Spika, sasa tuangalie kwenye ajira zetu, inawezekana changamoto ya ajira imetokana na kuwepo kwa teknolojia na kuongezeka sana. Teknolojia imechukua ajira nyingi za vijana, lakini pia nchi yetu imepiga hatua kwenye kuboresha elimu. Wasomi wameongezeka ukilinganisha na nyuma, lakini mambo yalivyoendelea sana, kwa mfano mambo ya artificial intelligence mambo ya Web3, mambo ya Blockchain, yamechukuwa ajira za vijana, lakini tunaongelea hicho kidogo ambacho kinapatikana chenye thamani, kinatakiwa kipatikanaje? Changamoto ndiyo inaanzia hapo.

Mheshimiwa Spika, mimi naona kwamba ipo misingi ya utawala bora iliachwa kwa namna ambavyo ajira hizi zinagawiwa. Kwenye misingi ya utawala bora, kuna vitu ambavyo unaambatana navyo. Lazima kuwe kuna uwazi, namna ambavyo ajira hizi zinapatikana, ni kwa uwazi? Zinagawiwa kwa uwazi? Ushirikishwaji; ajira hizi zinapokuwa zinagawanywa kunakuwa na ushirikishwaji kila mtu aweze kuona? Kuwajibika; watu wanawajibika wanapogawa hizi ajira kwenye Halmashauri zote na kwenye maeneo yote, na kwa watu ambao hawana watu wa wakuwasemea? Ufanisi; kuna ufanisi kwenye jambo hili? Je, kuna usawa na ujumuishi?

Je, watu ambao hawana watu wa kuwasemea, hawana ndugu zao viongozi, usawa umefanyika? Je, makubaliano yanayoelezeka, yapo makubaliano ambayo yakionekana kwamba hapa palifeli tukubaliane ili wakati mwingine iweje? Je, usikivu wa karibu wa Serikali, jambo hilo linafanyika? Lingine ni kufuata utawala wa sheria.

Mheshimiwa Spika, jambo hili likapelekea jamii kuanza kukosa Imani. Siyo kwamba labda inakosa imani na Rais wao, lakini inakosa imani na wale ambao watu Rais amewaamini, mamlaka zimewaamini, ambapo wao ndio wanachakata hizo ajira ziweze kuwafikia watu wote. Kwa nini wananchi wakapoteza imani? Kwa nini wananchi waache kuamini mfumo ambao unachakata ajira, waanze kutufuata sisi Wabunge? Kila Mbunge anafuatwa ili aweze kumsaidia mwananchi kuweza kupata ajira? Mimi mwenyewe kwenye simu yangu nini meseji zaidi ya 300; kila mtu ananiambia wewe ni mtu mkubwa. Mimi ni mtu mkubwa kuanzia lini? Mimi kazi yangu ni kuwasemea wananchi, kuyaleta mahitaji yao hapa kwa Serikali. Kwa nini wananchi wapoteze imani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi watakapopoteza imani kwa vyombo ambavyo vinachakata ajira zetu, tutatengeneza jamii ambayo itakuwa na matabaka sana. Miaka 20 au 30 inayokuja tutakuwa na watu ambao wanaamimi kila mtu aliyeko madarakani ni mtoto wa kigogo, kitu ambacho siyo kweli. Sisi wengine ni watoto wa wakulima, mbona tuko hapa ndani! Kwa hiyo, ni lazima ajira hizi ziwe jumuishi, ajira hizi zizingatie utawala bora ili kila mtu aweze kupata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini imani ni kitu cha muhimu? Hebu tuangalie, mimi kwa imani yangu kama Mkristo, tunaamini kwamba hata Mungu wakati anaumba ulimwengu, aliumba kwa imani. Nisome kwa Waraka wa Waebrania Sura ya 11 mstari wa kwanza mpaka wa tatu.

Biblia Takatifu, inasema hivi: “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasionekana. Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa. Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa na kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Biblia yenyewe inasema kwamba imani ni kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Kwa hiyo, wananchi wakianza kuamini kwamba sisi hatuwezi kutendewa haki, mbele tunaweza kutengeneza kizazi ambacho ni cha waasi. Mbele tukatengeneza watu ambao hawatawaamini tena viongozi walioko madarakani, kwa sababu watakuwa wanamwona kila aliye Spika ni kwa sababu alikuwa ni mtoto wa kigogo. Jaji Mkuu labda wa Mahakama, ni mtoto wa kigogo. Ni lazima tuweze ku-balance kama ambavyo wazee wetu wa zamani, kila mahali ambapo nchi hii ilitoka, alitoka kiongozi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiangalia Kanda ya Ziwa, alitoka Rais wa kwanza; tukiangalia sijui Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete, ametoka Pwani; tukiangalia sijui Mtwara kule, alitoka Rais. Pia nchi hii, wako Viongozi kama akina Kawawa, walitoka sehemu za kawaida. Kwa hiyo, ni lazima ajira hizi ziwa-spot vijana kutoka maeneo yote. Ni lazima Serikali ifike hatua itengeneze imani kwa Watanzania kwamba ajira hizi zinapotokea, wakikaa chini huko sirini ambapo sisi hatuoni, wawaaminishe Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni nini? Ushauri wangu ni mambo yafuatayo: Wapo vijana wengi wa Kitanzania ambao ni ma-programmer wazuri sana. Mimi mwenyewe by professional ni programmer. Tunaomba vijana hawa wa Kitanzania waitwe, wawasaidie kutengeneza system ambayo mtakapokuwa mkikaa sirini, mkiwaita vijana; kwa mfano, kama nafasi zilizotolewa ni 21, kama 100,000 wana sifa, system ile iwe ya wazi. Tuweze kuona kwamba kama watu 100,000 wana sifa, system iweze kuwachakata tuone. System yenyewe iwa-terminate kulingana na system ilivyo. Hii itafanya tusindelee kuona kwamba Serikali ni bias. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imani hiyo hiyo kwa Watanzania ambayo imejengeka kwamba nafasi ambazo zinatolewa, zinatolewa kwa kujuana; mwaka 2022 ulivyotupeleka sisi Jeshini, kuna nafasi za Watendaji zilitolewa kwenye Halmashauri yangu. Kule ambapo nafasi zilikuwa zimetangazwa kulikuwa na watoto wengi ambao wanajitolea kwenye Halmashauri ya Momba. Yule mtu aliyetoka Tume, cha kushangaza, sisi hakuna hata mtoto mmoja aliyetoka Momba. Sasa kwa sababu tumejenga imani ya kwamba nafasi hizi zinatolewa kwa madili na janja janja na mbambamba nyingi, hata mimi mwenyewe Mbunge naamini yule mtu aliyetoka kule Tume alikuja na majina yake mfukoni, ndiyo maana hakutaka kuwapa nafasi watoto ambao walitoka kwenye Halmashauri ya Momba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halafu jambo hili liliteta uchungu kwenye Jimbo la Momba…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, jambo hili liliumiza sana wazazi wa Momba kwamba ilikuwaje kwamba watoto hawa ambao Halmashauri ilikuwa imewaamini, wanajitolea na wanakusanya mapato TAMISEMI, halafu leo walipoingia kuhojiwa, eti watoto wao hawakuwa na sifa. Ni kitu ambacho hakiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye misingi ya utawala bora inasema, lazima kuwe na usawa na ujumuishi. Sasa hiyo usawa na utawala bora ulikuwepo wapi ambapo sisi hatukufanyiwa usawa na hatukujumuishwa? Hivyo naomba, hata kwenye ajira hizi ambazo zimetolewa, watoto wote wa Kitanzania, misingi ya utawala bora ifuatwe wakati watakapokuwa wanapewa ajira. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: …bila ya kujali ni mtoto wa kigogo, bila ya kujali ni mtoto wa nani, tunatamani kuona hata watoto wa masikini na wakulima wakishika nafasi kubwa kwenye nchi hii kama ilivyo kwenye viongozi wetu wa zamani. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, naunga mkoni hoja. (Makofi)