Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Furaha Ntengo Matondo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia katika Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya njema lakini kunipa ridhaa na kibali cha kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nikushukuru wewe mwenyewe kwa kazi yako nzuri ya weledi ya kuliendesha Bunge hili lakini nimshukuru Mheshimiwa Waziri kaka yangu Simbachawene, nimshukuru pia Naibu Waziri kaka yangu kwa kazi kubwa ambazo anazifanya. Katibu Mkuu na timu yao nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwa wananchi wa Tanzania kuhakikisha wananchi wako salama na wanafanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuagiza watumishi wote walioondolewa kwenye utumishi wa umma kuweza kupata mafao yao. Ni jambo ambalo ni zuri sana kwa watumishi wetu ambao waliachishwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nipende kumshukuru Mheshimiwa Rais kuagiza watumishi ambao walikaa zaidi ya miaka mitano bila kupandishwa madaraja kuweza kupandishwa madaraja. Ninamshukuru sana sana kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea tena kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa juzi tu kutangaza ajira nyingi, ajira 21,200 kwa vijana wetu wa Tanzania. Kwa kweli ni jambo kubwa kwa sababu ni muda mrefu ajira zilikuwa hazijatangazwa. Ajira hii ni kada ya afya na kada ya elimu. Ajira 13,130 kwa kada ya elimu, lakini tuna ajira 8,070 kwa kada ya afya. Ni jambo kubwa na ni jambo la kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda niongelee katika Mkoa wangu wa Mwanza. Katika Mkoa wangu wa Mwanza, walimu wa shule ya msingi tunauhitaji wa walimu 19,842. Walimu waliopo ni 12,529, tuna uhitaji wa walimu 7,313.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuajiri lakini tunaona ni jinsi gani changamoto ya ajira ilivyokuwa kubwa katika nchi yetu. Huu ni Mkoa tu mmoja wa Mwanza ambao shule za msingi tuna uhitaji wa walimu 7,313. Unaona ni jinsi gani hata weledi wa watoto wetu kupata elimu inakuwa ni changamoto kwa sababu ya walimu ambao bado ni wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, walimu wetu wa sekondari kwa maana ya sayansi tunao wachache sana. Kwa Mkoa wangu wa Mwanza uhitaji ni 3,750 lakini walimu tulionao ni 1,731. Upungufu tuna 2,019. Unaona ni jinsi gani changamoto ya walimu wetu wa sayansi katika Mkoa ilivyo ni kubwa. Hii inaonyesha wazi tutakuja kukosa vijana wetu madaktari lakini pia tutakosa ma-engineer, hata watu ambao wanatusaidia kwa maana ya kada muhimu kama hii kuweza kuwa na shida. Kwa hiyo, nizidi kuiomba Serikali yangu tukufu pamoja na kwamba ajira zimetolewa lakini ione changamoto hii tunaweza kwenda kuitatua vipi kwa kuongeza watumishi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Mwanza tuna changamoto kubwa sana tena kwa watu wa afya. Watumishi tulionao, waliopo ni 3,411; wanaohitajika ni 10,136 lakini upungufu tuna watumishi 6,975. Huo ni mkoa mmoja tu na tumeajiri 8,070. Utaona ni jinsi gani tuna mahitaji makubwa ya wataalam wetu, madaktari wetu. Tunajenga vituo vya afya lakini tunajenga zahanati. Bila kupata wataalam hawa tutakwenda kufanya kazi gani katika hizo zahanati zetu na vituo vya afya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizidi kuiomba Serikali yangu tukufu iweze kuliona hili changamoto ni kubwa. Tusije tukajenga majengo yakaja kuishia kwenye popo tu. Bila kupata wataalam hatuwezi kufanya kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali yangu iendelee na mkakati huu maalum ambao wanao wa kuweza kuendeleza wataalamu wetu ili angalau tuweze kuendana na kasi ya wananchi wetu tuliopo huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongee kidogo kuhusu suala la wastaafu wetu. Wafanyakazi wetu wanaajiriwa. Anaajiriwa mtu akiwa na miaka 20, anaajiriwa kwenye Mfumo wa LAWSON wote wanajua wanaingia mle lakini hata kabla hajastaafu, ndani ya miezi sita anaandika barua ya kustaafu lakini inakuja kufika kipindi anatakiwa kustaafu, anaanza kuambiwa mfumo wako hauonekani vizuri, mara barua zako hazionekani. Tuliwezaje kumlipa huyu mtu mshahara wakati anafanya kazi kama barua zake hazikuwemo kwenye mfumo? Tuliwezaje kuwa na huyu mtu miaka 20,30 kazini kama tulikuwa tunajua ana matatizo? Wazee wetu wamehangaika sana. Walipata changamoto kubwa sana, walimu shule zilikuwa ni mbali, mtu anatembea kwa baiskeli kwa mwendo mrefu saa 10 usiku anaamka. Inakuja kufika mwisho ameishiwa nguvu anaanza kuambiwa barua zako hazionekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inaumiza sana, tuone ni jinsi gani tutaendelea kuwasaidia wazee wetu waliotufikisha hapa kuweza kuwaachia maisha yao ya baadaye yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali yangu kwa kuleta Mfumo mzuri wa TASAF kwa ajili ya kupunguza umasikini kwenye kaya zetu. Mfumo wa TASAF ni mzuri sana na ninaupongeza sana lakini changamoto iliyopo kwa wananchi wetu ni kukosa elimu.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali yangu tukufu kuona kuna haja sasa ya kuwapelekea wananchi wetu elimu, waweze kujua nini maana ya TASAF? Pia waweze kujua TASAF ina malengo gani kwao?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. FURAHA N. MATONDO: ...Waweze kutambua taratibu zake zikoje kwa wananchi na walengwa ni watu wa namna gani?

SPIKA: Mheshimiwa Furaha Matondo kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Waziri wa Nchi.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge ya kukubaliana naye kwamba Mfumo ama program ya Mradi wa TASAF ni mradi muhimu sana na unahitaji elimu na jambo hili lilithibitishwa pia na Diwani wa Chama cha CHADEMA katika Kata moja ya Masasi Mjini alipokuwa anaishukuru Serikali kwa kazi nzuri iliyofanywa na Program ya TASAF katika kata yake ya CHADEMA pale Masasi Mjini na akaomba elimu itolewe nchi nzima, Watanzania wote ikiwemo vyama vyote vya siasa waelewe mradi huu wa TASAF ulivyo mzuri na unavyosaidia wananchi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Tunza Malapo unamfahamu huyo Diwani jina lake ili Mheshimiwa Waziri…

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

SPIKA: Mheshimiwa ngoja, subiri. Mheshimiwa Tunza Malapo unalifahamu jina la huyo Diwani?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, hapana simfahamu.

SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Furaha Matondo unaipokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Waziri?

MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ninaipokea kwa sababu TASAF wanafanya kazi nzuri, changamoto ilikuwa ni elimu tu kama alivyosema. Kwa hiyo, niombe wananchi wetu waweze kupata elimu waweze kujua nini misingi ya TASAF lakini taratibu zake zikoje kwa wananchi na walengwa ni watu wa namna gani?

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kweli mikutano inaitishwa na watu wanaitwa lakini wengine hawawezi kuhudhuria maana hawaelewi nini maana ya TASAF. Licha ya hivyo, kuna wazee wengine ambao familia zao vijana na watu wanaowazunguka wanauwezo wa kufanya kazi. Kwa hiyo, wananchi wengi hawajui ni kitu gani kinatakiwa kwa wale baba zetu na ndugu zetu walioko kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo naomba niseme kidogo tena kwenye changamoto iliyopo kwenye ajira zetu. Kuna nyumba watu wako wanne, ameanza kuomba ajira wa kwanza huu ni mwaka wa tano mpaka wa sita lakini mpaka na wadogo zake wamekuja kusoma wamekuwa watu wanne wanasomeshwa kwa shida lakini mpaka leo hawajapata ajira. Kila wakiingia kwenye mfumo kuomba ajira, ajira zikitoka hawamo. Inaumiza, ni kweli Wabunge tuliomba humu wote wala siyo wachache, simu zetu zimejaa kuombwa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wabunge unajua kabisa ni jinsi gani hatuwezi kuajiri lakini tunajua mfumo wetu ni mfumo ambao unatenda haki. Basi ukatende haki kwa wananchi wetu. Kama ambavyo tumesema changamoto kubwa iliyoko hata kwenye Mkoa wangu wa Mwanza, tuna vijana wengi ambao hawajaajiriwa. Wamemaliza wana zaidi ya miaka mitano, miaka sita wanahitaji ajira lakini mpaka leo ajira hazijapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuombe sasa haki ikatendeke, vijana wetu waweze kupata ajira. Changamoto iliyopo iweze kupatikana. Mkate tunaoupata tuweze kugawana wote ratio sawa. Mikoa mingi tuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)