Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote kwa vile Wizara hii iko chini ya Ofisi ya Rais mwenyewe, nichukue nafasi hii kumpongeza sana na kumshukuru kwa ajili ya kazi kubwa, mageuzi makubwa yanayofanyika katika sekta hii ya utumishi na hata sekta ya utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna anayebisha kwamba yako mageuzi makubwa ambayo yamefanyika ndani ya muda mfupi katika maeneo hayo yote mawili. Watanzania wanaona na hata dunia nzima inaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Waheshimiwa hawa nikianza na Mheshimiwa George Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete kwa kuaminiwa kuongoza Wizara hii nyeti. Ni wanasheria na mawakili wabobezi lakini nakwepa kuwaita wasomi kwa sababu historia inaonyesha kwamba suala hili la wanasheria kuitwa wasomi ilitengenezwa kwa ajili ya mahakamani ili kutawala zile nyongo zao na nini na kuheshimiana wakati mambo yanapokuwa makali kwenye mabishano. Sasa mnapotuita wasomi huku nje kuna kaujanja hapa mnataka kututenga na mambo fulani fulani mazuri, tumeshtuka tunaanza kukataa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la utumishi changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezizungumza katika maeneo yao pia zipo katika Jimbo letu la Mwanga hasa katika sekta ya elimu na afya. Upungufu ni mkubwa na changamoto zote zilizozungumzwa zipo. Naungana na wale ambao wameshauri kwamba pamoja na vigezo vizuri ambavyo TAMISEMI imeviweka katika kuajiri kama vilivyozungumzwa na Mheshimiwa Waziri katika Bunge hili, bado kile kigezo cha wanaojitolea ni kigezo cha muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, unaweza ukakuta hizi kazi za ualimu hasa ualimu na afya pamoja na kwamba ni kazi za mshahara lakini ni kazi za wito. Mtu anaweza akawa alimaliza 2015 akaomba ajira, alipoikosa akaenda kufanya shughuli zake. Leo 2022 nafasi zimetoka anaomba, tunasema kwa vile ni wa 2015 tumpe lakini yuko mwingine ambaye amehitimu 2018 akakosa ajira lakini akajitolea mpaka leo. Kwangu mimi huyu ndiye mwalimu au mhudumu wa afya mwenye wito kwa hiyo apewe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liko suala la ATCL ambalo nimeona kwamba kamati imeshauri kwamba Serikali iiondolee mzigo Wakala wa Ndege za Serikali mzigo wa kumiliki hizi ndege za biashara ambazo zinaendeshwa na ATCL. Wazo hilo ni zuri lakini naamini kabisa kwamba utekelezaji wake ni wa kiufundi sana ambao unahitaji makamati makubwa makubwa ya wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali. Nachangia kwenye eneo hilo kama kuchochea tu kufikiri ili Serikali ione umuhimu wa kulikabili jambo hili kwa utaalamu wa hali ya juu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama kumbukumbu zangu ziko sawa, nikikumubuka Hotuba ya aliyekuwa Waziri wa sekta hiyo, Dkt. Harrison Mwakyembe kipindi fulani ambapo aliwashambulia sana watu walioingiza fedha kwenye akaunti ya ATCL ilihali wakijua kwamba kuna madeni. Nadhani utaratibu huu wa kuzinunua hizi ndege kupitia wakala wa ndege za Serikali umesaidia katika kutibu hili jambo kwamba ATCL imepata muda wa kupumua kuweka mambo yake sawa kabla haijaingia kwenye biashara hii nyeti ya kumiliki na kuendesha ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa jambo hili limetuokoa katika madeni ya ATCL hasa yale ya ndani kwa sababu sheria yetu hairuhusu kukamata mali za Serikali katika kutekeleza hukumu.

Mheshimiwa Spika, sasa katika madeni haya ya nje hasa yanayotokana na maamuzi ya mahakama za kimataifa imeonekana kwamba sasa ndiyo tumeizamisha huko ndiyo maana baadhi ya ndege zetu kwa taarifa zinazokuja ni kwamba zimekamatwa na pia hatujui kwamba na hizi ambazo hazijakamatwa ziko salama au ziko namna gani kwa sababu suala la kushtakiwa na kuwa na hukumu ambazo ni dhidi yetu ni suala la kawaida tu kwa sababu kama nchi inakuwa inaingia kwenye mikataba inafanya mambo makubwa haiwezekani ikakaa tu bila kukabiliana na majanga kama hayo ya kesi. Kwa hiyo, hatuwezi kukwepa, dawa yake ni kuangalia jinsi ya kulinda mali zetu katika matatizo kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tufanye nini? Mimi ushauri wangu, muundo wa ATCL mpango wake wa uwekezaji pamoja na masuala ya madeni yapitiwe upya kitaalamu. Ikiwezekana tufanye, sasa naomba kutumia lugha ya Kingereza, tufanye restructuring ya madeni yake kwa kupitia benki. Baada ya kufanya hivyo, yatakayoonekana kwamba bado ni madeni au ni fedha ambazo tunahitaji kwa uwekezaji tukope kwenye benki. Tunaweza kutumia benki yetu kama TIB. Tukope kwenye benki halafu tu-charge assets zote za ATCL kwenye benki katika maana kwamba tuweke rehani assets zote kwenye benki. Tukifika hapo maana yake ni kwamba hizi assets zitakuwa zinamilikiwa na benki. Kwa hiyo, hakuna anayezidai wa ndani wala wa nje wala anyeidai Serikali ambaye anaweza akagusa mali hizi kwa sababu zitakuwa zinamilikiwa na benki.

Mheshimiwa Spika, nadhani hii ni njia mojawapo ambayo ikifanyiwa kazi kitaalam inaweza ikatufikisha katika utatuzi wa tatizo hili la ATCL ambalo tumelia nalo kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimejaribu kuangalia mashirika mengine ya ndege, umiliki wake uko namna gani. Kenya Airways kwa takwimu zilizoko kwenye mitandao na tovuti zao za 2022, za mwaka jana, 48.9% ndiyo inayomilikiwa na Serikali na katika hizi 48.9%, 38.1% inamilikiwa na fungamano (consortium) ya mabenki ambayo yameikopesha KQ. Kwa hiyo, utakuta zaidi ya 51% haimilikiwi na Serikali. Ukija South African Airways, 51% inashikiliwa na fungamano la makampuni (consortium) inayoitwa TAKATSO, 51%.

Mheshimiwa Spika, Rwanda airways yeye alikuwa anamilikiwa na Serikali lakini mwaka jana kuna mazungumzo yalikuwa yanaendelea, sijapata matokeo yake ya mwisho, walikuwa wanakusidia kuuza asilimia 49 kwa Qatar airways.

Mheshimiwa Spika, British Airways wakongwe wenyewe wanamilikiwa na Parent Company inaitwa International Airline Group, asillimia 25.1 hii Parent Company inamilikiwa na Qatar Airways. Ninachosema ni nini? tukitoa asilimia 51 ya hisa za ATCL ikawa haimilikiwi na Serikali ina maana kampuni hii haitakuwa ya Serikali kwa sababu majority share…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, private, kwa hiyo hii itasaidia…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOSEPH A. TADAYO:… hakuna atakayeweza kuikamata ndege zetu kwa ajili ya madeni ya Serikali kwa sababu mmiliki hatakuwa Serikali katika maana ya majority shareholding. Na suala la kumiliki…

SPIKA: Mheshimiwa Tadayo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Halima Mdee.

TAARIFA

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa kuchagiza tu kidogo, Indian Airways ambayo imebeba jina la nchi inamilikiwa kwa asilimia 100 na Kampuni binafsi ya TATA, kwa hiyo nakubaliana na wewe kwamba haya mambo lazima tuyafikirie na kuyachakata. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Tadayo unapokea taarifa hiyo.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo mimi nilizozifanyia utafiti Indian Airways haikuwa mojawapo lakini mimi ninaona fahari kwamba airline yetu imefufuliwa in the National Carrier. Wakati ulikuwa ukisafiri kwenda hata Nairobi au Ethiopia ukiangalia ndege zao zimepangwa pale National Carrier kama ng’ombe wa Mmasai halafu sisi tulikuwa hatuna ndege ilikuwa ni jambo la kusikitisha. Kwa hiyo huu ni mchakato ni mzuri, nakubaliana na hiyo taarifa; lakini tuendelee kufanya mchakato wa kulinda na kuokoa ndege zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata suala zima la kumilikiwa hizi ndege na Wakala wa Serikali nadhani kuna benefit zingine ambazo tulikosa. Kwa mfano kuna taasisi inaitwa International Civil Aviation Organization (ICAO) ambayo inashughulikia mambo ya kufanya tathmini zinapotokea ajali za ndege, mambo ya bima na vitu vingine vingi sana. Sasa sidhani kama ile taasisi inaweza ika-admit ndege ambazo zinamilikiwa na Serikali kwa sababu ile ni purely kwenye mambo ya biashara.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda wangu nafikiri bado dakika chache naomba tu nizungumzie suala moja tu juu ya sekta ya utoaji haki. Naipongeza sana Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya utoaji haki hasa kwa mfano katika eneo la Idara ya Mahakama.

Mheshimiwa Spika, majengo haya mazuri na facility zingine bado hazitaweza kutufikisha tunapotaka, kama sheria zetu za procedure hatujazibadilisha. Mwalimu wangu Marehemu Dkt. Lamwai Mungu amlaze mahali pema, aliwahi kuniambia kwamba kila mtu anajua haki yake lakini jinsi ya kuipata ndio ambayo watu hawafahamu. Kwa hiyo tusiporahisisha sheria zetu hizi katika kupata haki mbalimbali bado sheria zitakuwepo pale zinatupa haki lakini jinsi ya kuifikia inakuwa changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona kengele imegonga nisiendelee sana kwenye hilo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)