Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi niweze kuchangia, ieleweke tu kwamba tunayokuwa tunayazungumza mengi ni kwenye kuboresha na sio tuchukulie kwa nia mbaya.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na suala la TASAF. Nimeuliza swali asubuhi hapa, natambua kwamba miongoni mwa wananchi walionichagua mimi wapo ambao ni wanufaika wa TASAF na wapo ambao wana-enjoy na hili jambo, lakini nataka niboreshe kidogo.

Mheshimiwa Spika, nia inaweza ikawa njema, na kwa sababu si Mawaziri wanaoshuka chini kwenda kukutana na wanufaika, approach inayotumika kwanza kuwapata wanufaika ina changamoto nyingi sana; na tusikwepe kwamba hilo jambo halipo wakati lipo. Leo tunapozungumza Wenyeviti wa Serikali waliokabidhiwa hilo jukumu, nchi nzima ni wa Chama cha Mapinduzi. Wanavyokuwa wanakwenda hawaitishi mikutano kama ambavyo mwongozo umesema, walipita na madaftari yao, wanaona hii nyumba huyu mtu ni CHADEMA hawapiti wanaenda nyumba nyingine, na ikitokea aliingia kwa bahati mbaya lazima uenguliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi fedha lazima ziende kwa nia iliyokusudiwa na tusikwepe hapa kwamba sio la kisiasa lipo. Mimi ninayezungumza nimeshazungumza kwenye Baraza la Madiwani…

SPIKA: Mheshimiwa kwa sababu hilo jambo nimeshalieleza hapa mbele, wewe niletee majina ya hao wananchi wako ambao ni wa CHADEMA waliokosa kwa sababu ya chama chako; niletee hayo majina. Kwa sababu na wa CCM wamesema na kwao wamekosa sijui kama wale waliokosa pia ni wa CHADEMA, ila wewe kwa sababu umesisitiza kwenye hoja hiyo niletee majina ya hao ambao wamekosa kwa sababu ya CHADEMA. Ukishaniletea hayo majina mimi nitachukua hatua. (Makofi)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nimesema miongoni mwa changamoto zilizojitokeza kwenye kuwapata wanufaika suala la ubaguzi wa kisiasa lilikuwepo, jambo…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Kama lilikuwepo si ndio utaniletea majina.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, sawa nitakuletea.

SPIKA: Wewe niletee majina ya wapiga kura wako wa Jimbo la Nkasi Kaskazini walionyimwa TASAF kwa sababu ni CHADEMA, niletee hayo majina ili mimi nichukue hatua. (Makofi)

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitafanya hivyo kwa maslahi mapana…

SPIKA: Mheshimiwa Agness Marwa kwa sababu niliyekuwa nazungumza ni mimi ukisema taarifa wakati mimi naongea ni kama unanipa taarifa mimi. Kwa hiyo, inabidi usubiri aanze kuchangia muhusika halafu ndipo uombe taarifa. Mheshimiwa Aida Khenani.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitambue kwamba aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara hii Mheshimiwa Deo alifika mpaka Nkasi na alikutana na hayo mambo na akasema wanakwenda kufanya utaratibu wa kupitia upya…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Sasa Mheshimiwa Aida, mimi nimekaa hapa mbele, unataka kusemaje? Kama mlishamalizana na Mheshimiwa Waziri basi agizo langu linaisha na huo mchango wako ninauondoa kwa sababu ndio hoja niliyokuwa naongea na Mheshimiwa Lwehikila hapo, sasa na wewe unarejesha hiyo hiyo. Nakwambia niletee ushahidi ili nichukue hatua unasema Naibu Waziri alikuja kama tatizo halikwisha?

Kama Naibu Waziri alikuja na tatizo halijaisha mimi nakwambia nikusaidie bado unang’ang’ania hivyo sasa unataka mimi nikusaidieje? Kama huna ushahidi ondoa hayo maneno, kama unao ushahidi niletee ili Bunge lianze kuchukua hatua, kwa sababu kuna watu wanaonewa kwa sababu ya vyama vyao. Kama huna ushahidi kwa usalama wako ondoa kwenye Taarifa Rasmi za Bunge, kama unao ushahidi niletee ili Bunge lichukue hatua kwa watu kuonesha upendeleo kwenye kupewa TASAF, ndio hoja iliyoko hapa mezani. Mheshimiwa Aida Khenani.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nategemea muda wangu unalindwa pamoja na maboresho na majina nitaleta…

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani, Mheshimiwa Kombo mpe nafasi achangie halafu ndio utampa taarifa.

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, haya ahsante.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema hiyo kuna masuala ambayo yanaendelea ya watu kufanya kazi ambao ni wanufaika wa TASAF, ningeomba Wizara iweke utaratibu huo vizuri, wananchi waeleweshwe vizuri. Kama ni vibarua kama vibarua wengine basi lisiwekwe kama wanufaika ili watu wakafanye kazi, kwa sababu wanahitaji kufanya kazi, kwa sababu wale wanufaika kuna wazee, wanafunzi, watu wenye ulemavu ambao hawawezi kufanya hizo kazi. Kwa hiyo, sura inayokwenda huko kwenye jamii yaani as if kwamba wote ambao ni wanufaika wanatakiwa kufanya hiyo kazi ya vibarua ambao kwa siku ni shilingi 3,000 jambo ambalo si sawa. Kwa hiyo, kama kuna maboresho ya hilo jambo au elimu basi itolewe vizuri ili nia ya hilo jambo ieleweke.

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye utumishi. Changamoto ya watumishi ni kubwa sana…

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani kwanza alisimama Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa.

TAARIFA

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana nilitaka kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba anapaswa ajue kwamba hasa jimboni kwake hakuna ubaguzi wa vyama, na ingekuwa kuna ubaguzi wa vyama yeye asingechaguliwa na asingekuwa Mbunge wa jimbo leo, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Sawa sijajua hiyo taarifa inaelekea kwenye hoja gani ya Mheshimiwa Aida Khenani, lakini kanuni zinataka nikuulize Mheshimiwa Aida Khenani unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, hiyo taarifa nilikuwa nimeshamaliza nimeingia kwa watumishi na naomba niendelee.

Mheshimiwa Spika, mahitaji ya watumishi…

SPIKA: Mheshimiwa Kombo.

TAARIFA

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, nilitaka nimpe taarifa tu dada yangu kwamba mimi hata kule jimboni kwangu kuna Mwenyekiti wangu wa Tawi wa Chama cha Mapinduzi ana sifa za kuingia kwenye mpango na amekuja kunilalamikia mpaka leo hajaingia. Kwa hiyo, nilikuwa nataka kumwambia kwamba hili haliko kisiasa, ni kila mwenye sifa ndio anaingia, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Sawa sasa kwenye hilo wacha nimsaidie yeye kasema anao ushahidi akishaniletea mimi ndipo tutachukua hatua kuanzia hapo. Mheshimiwa Aida Khenani malizia mchango wako.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kuna mambo tunatoana kwenye reli kidogo.

Mheshimiwa Spika, mahitaji ya watumishi ni makubwa sana nchini pamoja na kwamba tunatofautiana. Mahitaji ya watumishi Wilaya ya Nkasi ni 3,946 walioko ni 2,071 upungufu ni 1,265.

Mheshimiwa Spika, kipindi cha nyuma walikuwa wanajua watu wakipelekwa Nkasi ni sehemu ya adhabu na wengi walikuwa wanakimbia, lakini tunatakiwa tuondoje hiyo dhana kwamba ile si sehemu ya adhabu? Ni kutofautisha hawa watumishi wanaokwenda huku wapewe motisha ili waone na wao ni watumishi kama maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, leo ukiangalia miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa nyuma kielimu ni pamoja na Mkoa wa Rukwa, lakini utakuta kuna shule ambazo hakuna mwalimu wa kike kabisa wakati hapo tunategemea tupate akina Samia wengine kutoka Nkasi, wakina Tulia Ackson wengine kutoka Nkasi, wakina Aida wengine kutoka Nkasi. Sasa unawapataje wakati hiyo shule haina mwalimu wa kike? Kwa hiyo, hata yale mambo mengine ambayo mtoto wa kike anaweza akatengenezewa mazingira rafiki ili kufikia malengo yanakuwa hayafanani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kuna watumishi ambao wamekuwa wanakaimu kwa muda mrefu kinyume na utaratibu. Aidha, ni Wakurugenzi kutokujua kwamba mtu anatakiwa akaimu kwa kibali cha Katibu Mkuu au kwa makusudi. Kwa hiyo, anapokuja anatafuta haki zake kwamba mbona nimekaimu muda mrefu unakuta kwamba kukaimu kwake ni kinyume na utaratibu. Kwa hiyo, mambo hayo niwaombe Wizara, ni vizuri pia wanapopata taarifa za kila wakati wawe wanajua ni wangapi wanakaimu na wamekaimu kwa muda gani na je, wamekaimu kwa mujibu wa sheria ama la.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la maadili kwa watumishi; nimeona Mbunge mwenzangu alikuwa anazungumza hapo kwamba imefikia mahali sasa tumejenga hofu sio kufata sheria tena, hofu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba mtumishi anaweza akawa mfanyabiashara na anaweza akawa mkulima, haimzuii yeye kuwa mtumishi kwamba hawezi kufanya biashara nyingine za kumuingizia kipato. Nini kinatokea hapo? Aidha, ni suala la uwazi ndio imekuwa shida kwa Watanzania au ni hofu imetawala zaidi kuliko suala la uwazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapaswa kujua kwamba pamoja na changamoto nyingi ambazo zinawakabili watumishi, watumishi hawa wanaweza kufanya shughuli nyingine isipokuwa zisiathiri zile shughuli zao za kiutumishi na lengo litakuwa ni jema tu ili waendeleze maisha yao.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda niingie kwenye utawala bora; tunapozungumzia utawala bora tunazungumzia utawala wa sheria, demokrasia na uwazi. Hivi ninavyozungumza nimeona hata taarifa zinazokuja hapa; mimi ni Mbunge wa kuchaguliwa na wananchi. Hapa nazungumza Mbunge wako, Wakuu wa Idara wote na watumishi wote wa Wilaya ya Nkasi wamepigwa marufuku na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kutokunipa ushirikiano wa aina yoyote. Mimi ni Mtanzania na ni Mbunge na najua ofisi inajua. Hapa ndani Bungeni nimezungumza leo ni mara ya tatu.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua huu ni utaratibu wa wapi, kwa nini tuwapangie watu wamchague mtu fulani ndio apewe ushirikiano, hawa watumishi ni wa Serikali. Wana-Nkasi na wao ni miongoni mwa Watanzania wengine ambao wanatakiwa kupata huduma. Ninapokuwa ninatengwa leo mimi Serikali inajua. Nilishaandika barua kwa Waziri mara kadhaa hakuna kitu kinafanyika. Huo utawala bora tunauzungumza hapa, kama tumeamua kutokukubali mfumo wa vyama vingi mtoke kwenye huo mfumo kuliko haya yanayoendelea leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inaumiza wakati mwingine, leo tunawanyima haki Wana-Nkasi kwa sababu za interest. Natamani Serikali iniambie leo kwamba wanajua taarifa hizo, na kama wanajua ni maelekezo yao, na kama si ya kwao wamechukua hatua gani?

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mbunge, natakiwa nipewe haki zangu zote kama Mbunge kwa mujibu wa Katiba yetu ya nchi, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Aida umesema umepeleka barua, umepeleka barua ya malalamiko wapi?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nimepeleka kwa Katibu Mkuu, TAMISEMI, nimepeleka kwa Waziri mwenyewe amepewa nakala, lakini Mkuu wa Mkoa

mwenyewe nilianza kumlalamikia kwa Mkuu wa Wilaya kwamba yeye ni Mkuu wa Mkoa achukue hatua, hakuna chochote kilichofanyika mpaka leo, ni mwaka wa tatu sasa.

SPIKA: Jamani jambo zito hili linaloonesha kwamba kuna ubaguzi. Japo nina maswali mengi, lakini sina haja ya kuyauliza sasa, lakini Mheshimiwa Aida nimeshawahi kumsikia wakati akimpongeza hapa Rais kwamba maendeleo na kule kwake yanaenda; na kwa hatua anazozichukua Mheshimiwa Rais sidhani kama wateule wake wanaweza kutoa maagizo kama hayo ya kukataza ushirikiano na kiongozi aliyechaguliwa na wananchi. (Makofi)

Sasa kwa sababu sina taarifa za kutosha hapa Mheshimiwa Aida na umesema uliandika barua TAMISEMI, nadhani Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alifuatilie hilo jambo, halafu mimi nitapata mrejesho kutoka kwa Mheshimiwa Aida Khenani.

Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu kama ni katazo kwa namna anavyolisema yeye maana yake ni katazo lililotolewa hadharani pahala, kwa hiyo pengine upo ushahidi, kwa sababu sidhani kama pengine una ziara halafu Mkuu wa Wilaya hajaja, halafu ukaona huo ndio ushirikiano ulionyimwa. Lakini kama ni katazo basi nadhani mtusaidie hizo taarifa, Mheshimiwa Aida Khenani utaniletea mrejesho. Nadhani tupeane mwishoni mwa wiki ijayo utaniletea huo mrejesho wa wewe kubaguliwa na viongozi walioteuliwa kwenye eneo lako la kazi.