Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Esther Edwin Maleko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii nyeti na muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nipeleke pongezi zangu za dhati kwa Waziri pamoja na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Najua jukumu la kutunza mazingira ni la nchi nzima, lakini ninasikitika sana, hata Wenyeviti wanapokuwa wanasoma taarifa zao za bajeti hapo, inaonekana bajeti ni finyu sana katika Wizara hii. Tujiulize, Wizara hii ndiyo imebeba Wizara nyingine zote. Bila kuwa na mazingira safi, bila kuwa na kutunza mazingira ya nchi hii, hivi vitu vingine vyote haviwezi kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaona katika mlima wetu wa Kilimanjaro moto unatokea sana, ni uharibifu wa mazingira. Tunaona Serikali inatumia fedha nyingi katika kuzima moto huo, lakini siyo hivyo tu, hata watu wanakufa wakati wa kuzima moto, na Serikali inapata hasara kubwa sana. Je, imejipanga vipi sasa kuweza kukabiliana na masuala yote hayo kama bajeti inakuwa ni finyu kiasi hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iweze kuangalia suala hili kwa umakini, kwa sababu, bila kutunza mazingira hatuwezi kufanya jambo lolote. Tukumbuke kwamba, hii dunia ni kama nyumba, na jinsi tunavyozidi kuiharibu, iko siku itatuangukia, nasi sote tutakuwa tumeangamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu uharibifu wa mazingira umekuwa ni mkubwa sana. Ninasema tena kwa sababu ya moto unaowaka Mlima Kilimanjaro na uharibifu mkubwa wa mlima ule tunaona hata kiwango cha barafu kinazidi kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipangaje sasa katika kuona namna ya kutoa elimu kwa wale wananchi wetu wa kule chini ambao ndio wahusika wakubwa kabisa wanaohitaji kupewa elimu hii ili waweze kutunza mazingira? Wao ndio wanapaswa kuambiwa ni namna gani watatunza mazingira, ni njia gani mbadala wanazoweza kutumia ili wasiharibu mazingira kwa kukata miti ovyo, lakini elimu kule chini bado haijafika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naishauri Serikali, leo tunaweza kuuza hewa ya carbon. Ni kwa nini basi Serikali isijikite kwenda kutoa mafunzo na elimu kwa hawa watu wa chini kwenye Serikali za Mitaa ili waweze kujua umuhimu wa kutunza mazingira, na zaidi ni namna gani wanaweza kufaidika kwa kuuza hewa hiyo ya carbon? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma katika andiko moja ambalo linasema, Wilaya ya Tanganyika kuna vijiji nane vimepata takribani Shilingi milioni 380 kwa uuzaji wa hewa hii ya carbon. Kwa nini basi Serikali isione jambo hili ni la muhimu tukaweza kushirikiana na Halmashauri na wengine sasa wakapata hiyo elimu na namna gani wanaweza kupanda hiyo miti na zaidi ya hapo tukaweza kuvuna hiyo hewa na kuiuza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijikite kwenye suala la uzimamizi na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira. Kama nchi, katika eneo hili tumefeli sana. Tanzania kwa mwaka mmoja inazalisha taka ngumu takribani tani milioni saba, lakini cha kusikitisha kiasi kinachoweza kukusanywa, yaani kuzolewa, ni asilimia 35 tu. Hebu tujiulize tunaishije kwenye mazingira kama haya ambayo taka kama hizo nyingine zote zimebaki, hazijapata ufumbuzi wa namna gani zinaweza kukusanywa na kuzolewa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila kukicha majiji na miji yanakua, ongezeko la watu mjini linakua, viwanda na biashara na kazi nyingine za kuingizia wadamu kipato zinakua, lakini suala la kuzoa taka na kudhibiti taka bado limekuwa ni changamoto kubwa sana. Ninaishauri Serikali, kutokana na sababu hizi kubwa ambazo zinaonekana zinaenda kutuletea shida katika majiji yetu na Halmashauri zetu, Serikali ione ni namna gani basi itaongeza bajeti kwenye Wizara hii ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo, asilimia 30.7 ya utupaji taka nchini ni holela. Watu wanatupa taka kwa maeneo ambayo hayajatengwa. Unaweza mnaweza kuona, hata mnapopita kwenye mifereji au mito imekuwa ndiyo sehemu ya watu kutupa taka. Mvua inaponyesha, yale matakataka yanakuwa yanaziba mifereji ya maji na baadaye kunatokea mafuriko na baadaye tunapata kipindupindu. Hili ni jambo la kulifanyia kazi. Siyo hivyo tu, asilimia 38.4 ya maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kutupa taka, lakini miundombinu yake haikidhi utupaji taka. Kwa hiyo, hili ni jambo la kulitazama kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya utupati taka, ni asilimia 27.8, lakini hayahudumiwi. Ni kwa nini yatengwe lakini yasihudumiwe? Ni kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Lakini leo tunasema asilimia 5.3 ya utupaji taka nchini ndiyo inahusisha utupati taka salama. Tunakwenda wapi kama asilimia hiyo yote ni sawa na asilimia 90 ya utupaji taka katika nchi yetu siyo salama? Kwa hiyo, tunawezaje kukwepa kupata kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko? Hivyo naomba sana Wizara hii iweze kuongezewa bajeti ili iweze kufanya kazi zake vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Halmashauri nyingi hazioni umuhimu wa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya suala hili na ukusanyaji na utupaji wa taka. Mimi ninaishi hapa Mlimwa C, hapa hapa Dodoma, nitolee mfano hapa. Tunaweza kukaa na taka ndani zaidi ya wiki mbili bila kuja kuzolewa, lakini wanapokuja kuzoa, gari linalokuja kuzoa zile taka na lenyewe ni takataka. Hata wale wanaokuja kuzoa taka ukiwaangalia, hawana hata vifaa vya kuwakinga kwa zile taka wanazokuja kuzibeba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tujiulize, tunakwenda wapi kama Taifa? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Kengele ya pili, ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)