Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Bakar Hamad Bakar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nami kunipa nafasi hii ili kuweza kuchangia hotuba hii ya bajeti ambayo iko mbele yetu ambayo inahusu Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niwapongeze viongozi wetu wawili; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo wanaendelea kushirikiana na kwa namna ambavyo wanaendelea kufanya kazi ya kuleta maendeleo kwa Serikali zote mbili; Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na timu yao kwa utendaji wao mzuri wa kazi hizi na niwaambie tu kwamba tunaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba mambo haya ya Muungano yanaendelea kuwa mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwaomba Watanzania wote, hususan vijana, kuendelea kuulinda, kuutetea na kuupigania Muungano wetu huu kwa faida ya nchi zetu zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba vikao vya Kamati ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Muungano vinaendelea na hoja mbalimbali – kama ambavyo Mheshimiwa Waziri leo amewasilisha – hoja mbalimbali tayari zimepatiwa ufumbuzi; niipongeze sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi hizo bado tunazo kero mbalimbali ambazo zinaendelea kuleta changamoto kwa nchi zetu mbili. Alisema kwamba hoja ya mizigo inayotoka Zanzibar kuja Bara imeondolewa kodi zile ambazo zilikuwa ni kodi mara mbili, lakini bado hoja hii inaonekana kuwa ni changamoto, hasa kwa mizigo midogomidogo ambayo inatoka Zanzibar kuja Bara.

Mheshimiwa Naibu Spika, iliyoondoka ni hoja ya wafanyabiashara lakini haijaondoka hoja ya wananchi wanaosafiri kwenda Zanzibar na kurudi Bara wanaosafiri na mizigo yao midogo midogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani mwananchi amesafiri na kilo mbili za sukari anafika nazo Bara anaambiwa alipe kodi. Haiwezekani mwananchi amesafiri na TV moja, tena used, anakuja kutumia nyumbani, anafika Bara anaambiwa alipe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni nchi moja, haiwezekani wananchi hawa anayetoka Morogoro kwenda Dar es Salaam halipi kodi anaondoka na mizigo yake, anaondoka na mambo yake kama hayo lakini hakuna sehemu yoyote ambayo anasimamishwa kulipa kodi. Lakini anayetoka Zanzibar kuja Bara akifika Dar es Salaam anatakiwa alipe kodi kwa TV moja ambayo anakwenda kutumia nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili halijakaa vizuri. Niiombe sana Serikali ilifanyie kazi jambo hili. Bado kabisa halijakaa vizuri na inaleta kero kubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona magari ya nchi jirani mbalimbali yanayozunguka hapa Tanzania na hayana usumbufu wowote, hayaletewi usumbufu wowote, lakini kuna changamoto kubwa kwa usajili na utambuzi wa magari yanayotoka Zanzibar kuja Bara kuweza kutumika hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu hii ni moja, Tanzania ni moja. Ni kwa nini mpaka leo hakujawekwa sheria inayotambua, inayosajili magari yanayotoka Zanzibar kuja kutumika hapa Bara.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, jambo hili limezungumzwa muda mrefu sana na linaendelea kuwa kero. Niiombe sana Serikali, nikuombe sana Waziri, utuambie ni lini utaleta sheria ya kuweza kuweka wazi masuala ya usajili wa vyombo vya usafiri…

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba juzi tu nilinunua TV nilivyofika bandarini nikachajiwa difference laki mbili. Kwa hiyo, tatizo hili ni kubwa kweli kabisa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bakar, taarifa.

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado changamoto hii. Kwa hiyo tuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie, Sheria ya Usajili wa Vyombo vya Usafiri ni lini italetwa Bungeni kuweza kujadiliwa na kuweza kupitishwa rasmi na kuondoa mkanganyiko na usumbufu huu unaotokea kwa vyombo vya usafiri vinavyotoka Zanzibar kuja Bara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la ajira, hasa kwa taasisi za Muungano. Upo uwiano ambao umebainishwa wa asilimia 21 kwa Zanzibar na asilimia 79 kwa Bara kwa zile taasisi zote za Muungano. Bado pia hapa kuna changamoto; hakuna utaratibu ambao uko wazi unaobainisha hizi asilimia 21 zinapatikanaje na asilimia 79 zinapatikanaje. Kwa hiyo, naomba sana Serikali hebu ifanyie kazi jambo hili, iweke utaratibu ulioko wazi, unaoonekana na ambao hauna mkanganyiko, kwamba tujue asilimia 21 zinapatikanaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imeshauri kwamba kuna haja na umuhimu mkubwa wa kufanya tathmini ya watumishi wa Umma wanaofanya kazi kwenye sekta za Muungano; bado. Likifanyiwa tathmini jambo hili naamnini itakuja kutuletea majibu hapa kwamba jambo hili hasa likoje. Ni kweli asilimia 21 inatekelezwa? Ni kweli ajira hizi ziko hivyo ambavyo inazungumzwa? Lakini pia tutapata majibu mengi na tutaondosha manung’uniko mengi ambayo yapo sasa hivi yanayoendelea. Niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje na majibu haya kwa ufasaha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha jambo hilo pia kuna suala la ushiriki na ushirikishwaji kwa taasisi ambazo siyo za Muungano. Tunafahamu kwamba ushirikishwaji na ushirikiano wa taasisi za Muungano hakuna shida sana, lakini kwa taasisi zisizo za Muungano, na hasa kwa mikutano inayofanyika ya kimataifa ambapo Tanzania inakwenda kushiriki kule, Zanzibar bado baadhi ya taasisi hazijaweza kushirikishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba baadhi ya taasisi tayari, kwa mfano Ofisi ya CAG tayari mikutano mbalimbali Zanzibar inashirikishwa. Lakini kuna taasisi kwa mfano suala la Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Zanzibar tuna mamlaka yetu na Bara tuna mamlaka nyingine. Kwa hiyo, niombe sana kwa mikutano ya kimataifa ambayo Tanzania inakwenda kushiriki kwa taasisi ambazo siyo za Muungano basi Zanzibar iweze kushirikishwa kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la mwisho ambalo ni suala la mazingira. Amezungumza hapa Mheshimiwa Simai, Mbunge wa Nungwi, kwamba jambo hili ni changamoto kubwa, hasa kwa visiwani. Mabadiliko ya tabianchi ni jambo kubwa sana kwa visiwa. Visiwa vinaendelea kuliwa na maji. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali iweke msisitizo na mkazo mkubwa kwenye suala hili la mabadailiko ya tabianchi na kuongeza fungu hili la bajeti, hasa kwa maeneo ya visiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya kusema hayo, niiunge mkono hoja hii. Nakushukuru sana. (Makofi)