Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, na nitachangia upande wa Fungu 31, Idara ya Mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mazingira kwa umuhimu wake ni jambo ambalo mpaka sasa naona hatujalipa umuhimu wa kutosha kama ambavyo linastahili. Labda nitaje sekta ambazo zinaathirika kwa namna moja au nyingine na suala la mazingira, kwa namna zozote zile; sekta za maji, kilimo, afya, miundobinu na uchukuzi, nishati, madini, mifugo na uvuvi, maliasili na utalii, viwanda na biashara, teknolojia, elimu and the list goes on.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka hapa tulipo sisi kila Mbunge anawakilisha jimbo analotoka, kwa namna moja au nyingine hawezi kukwepa kuzungumza suala la mazingira na sasa hali ilivyo, mabadiliko ya tabianchi. Lakini inasikitisha kwamba upangaji wetu na mgawanyo wa fedha katika bajeti zetu za miaka ya fedha kwenye sekta ya upande wa maendeleo kwenye upande wa mazingira hatujatendea haki sekta na idara ya mazingira kama ambavyo inastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitaje kwa mfululizo miaka ya fedha mitatu mfululizo; fedha za miradi ya maendeleo zimetengwa kwa kutegemea sana fedha za nje katika kiwango kilichokithiri. Mwaka 2021/2022, Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 2.979, lakini asilimia 86.54 ya fedha hizi zilikuwa za nje, sawa na shilingi bilioni 2.570. Fedha za ndani zilikuwa milioni 400 tu ambayo ni sawa na asilimia 13.54, ndiyo hizo pesa zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2022/2023 Bunge liliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 18.642, lakini fedha za nje zilikuwa asilimia 98.5, sawa na shilingi bilioni 18.360. Fedha za ndani ambazo ni za kwetu zilikuwa asilimia 1.5, sawa na shilingi milioni 282 hivi; hiyo ndiyo pesa yetu sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu wa fedha, Serikali imeomba shilingi bilioni 16.656, lakini tunategemea shilingi bilioni 15.056 fedha za nje, sawa na asilimia 90.4. Lakini fedha za ndani, za kwetu sisi sasa, ni shilingi bilioni 1.6 pekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, atahari ya kutenga fedha kwa kutegemea fedha za jirani, fedha za wahisani, fedha za nje, ili upange mipango yako, ni sawasawa na sikukuu imefika unataka upike pilau lakini wewe una sufuria na mwiko, unategemea kila kitu pamoja na nyama na kuku na kila kitu kutoka kwa jirani. Jirani akiuguliwa, akifiwa, akiwa anapigana vita, wewe huwezi kula athari yake ni kubwa. Labda nikiongea hivi inawezekana ikawa lugha nyepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano. Mwaka 2017, Mfuko wa Green Climate Fund (GCF) ulitenga fedha kwa ajili ya Mradi wa Climate Change wa Mkoa wa Simiyu Dola milioni 187.7, lakini fedha hizo hazikuletwa zikaweza kuletwa mwaka 2020. Kutoka mwaka 2017 athari zimetokea, mradi umefanikiwa kupita kwenye vigezo vyote vya kupewa fedha lakini fedha imeletwa mwaka 2020. Kwa sababu anayetoa fedha ndio anayechagua wimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, athari zilizosababisha watu wa Mkoa wa Simiyu wapewe hizi fedha bado zinaendelea. Lakini kwa sababu tumeomba fedha kwa wahisani – na ni kitu kizuri, sisemi kwamba ninabeza kwamba haifai kupewa fedha za wahisani – lakini kuitegemea fedha za nje kwa kiasi hiki, zaidi ya asilimia 90, maana yake unashindwa kutekeleza miradi yako kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta nyingine zote nilizozitaja hapa zimetengewa fedha za ndani. Utekelezaji wake unategemea hizi fedha.

TAARIFA

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba hata hizo fedha ambazo mradi unatekelezwa kule Simiyu ziliombwa kupitia Save the Children Fund, Tawi la Canada. Kwa hiyo, hoja yake ni ya msingi sana kutenga fedha za kutosha hata hapa ndani. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nusrat, taarifa hiyo.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napoikea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu chako ukikiuona ni cha muhimu utakipa first priority na utakitengea fedha. Bahati mbaya sana Serikali inapeleka fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali kwenye sekta nyingine ambazo nilizitaja hapa ambazo zinaathirika kwa namna moja au nyingine na mazigira. Lakini fedha hizi utekelezaji wake pia unategemea stability ya mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunashindwa kutekeleza miradi ambayo Serikali imeitengea fedha nyingi kwa sababu ya athari za mabadiliko ya tabianchi na athari za kimazingira. Kwa hiyo, tunasababisha kupoteza wakati mwingine rasilimali za nchi kwa sababu hatuja-prioritize kutoka kwenye vyanzo vyetu vya uhakika ambavyo ni vya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitoe mfano. Mwaka huu ili tuone umuhimu wa kutenga fedha kutoka kwenye vyanzo vya ndani – mwaka huu wa fedha hizi shilingi bilioni 1.6 ambazo ndiyo chanzo cha ndani, asilimia 9.6 ya fedha za ndani kwenye mwaka huu wa fedha, hizi zinakwenda kujenga vitu vya msingi sana, wameongea watu wa kutoka upande wa pili wa Muungano, tunakwenda kujenga kingo ya Mikindani, Mtwara na Sipwese, Pemba kule, kwa hiyo unaona umuhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutakuwa na projects za namna hii ambazo zinaangalia palipoathirika zaidi na kwenda kutafuta namna ya ku-solve pale kutoka kwenye vyanzo vyetu vya ndani, sisi ndiyo tutakuwa tumetoa fedha na wimbo tumechagua sisi maana yake tunakwenda kutibu athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo wananchi wanaziona moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nizungumze jambo la pili kwenye climate funding. Green Climate Fund ndiyo mfuko mkubwa ambao Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi (UNFCCC) wanautumia kwa ajili ya ku-fund projects za masuala ya climate. Lakini sisi nchi yetu, taasisi za Serikali hakuna hata taasisi moja ambayo iko accredited, haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ndiyo nchi ambayo ina miradi mitano tu kupitia Green Climate Fund, lakini Kenya wana miradi 16, Uganda wana miradi 10, Rwanda wana miradi tisa. Sisi tumeshindwa kuzisaidia taasisi zetu ambazo ziko chini ya Serikali kupata accreditation ili tupate hizi fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, CRDB peke yake ndiyo imepata accreditation lakini mnakumbuka CRDB wanafanya kwa njia ya mikopo, siyo grants. Sisi taasisi zetu zinatakiwa zipate fedha…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)