Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamo wa Rais Mazingira na Muungano. Mimi nitajikita katika sehemu ile ya Mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika,ni kweli kwamba suala la mazingira ni mtambuka, na kama walivyotangulia wenzangu lina gusa Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na Sekta binafsi; na kwa jinsi hiyo tungetamani hata kwa namna ambavyo suala la mazingira linashughulikiwa ndani ya Serikali liweze kuwa na mfumo ambao pia ni jumuishi; la sivyo likiachiwa Wizara moja kama Wizara moja tutaona kwamba athari zake zinaweza zisishughulikwe ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika kuchangia hoja hii na mimi ningependa kuendelea kuweka msukumo zaidi, kwamba bajeti inayotengwa kutoka fedha za ndani kwa miradi ya maendeleo bilioni 1.6 dhidi ya bilioni 15 za wahisani nadhani hatujitendei haki. Tunapaswa tukubali kwamba wakati mwingine changamoto zinazotokana na athari za mazingira ni changamoto ambazo ni zetu binafsi kuliko hata zile ambazo zinatoka kwa fedha za wahisani na kwa hiyo tuombe Serikali; kwa mwaka huu kama ilivyopendekezwa sawa; lakini kwa miaka ijayo tuendelee kuweka msukumo wa kuongeza bajeti ili itusaidie kuweza kushughulikia hoja za mazingira ndani ya nchi yetu wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nipende kuwapongeza Serikali kwa jinsi ambavyo wamekuja na kampeni ya upandaji miti kote nchini. Lakini kampeni hii ingefanikiwa sana iwapo kungekuwa na mwongozo wa aina gani ya miti ipandwe kulingana na hali halisi ya maeneo husika. Kuna hatari ya kupanda miti katika vyanzo vya maji, na tunajua kuna miti ya mikaratusi, ukiipanda kwenye chanzo cha maji itanyonya maji yote na chanzo hicho kitakauka. Sasa tumeanzisha kampeni nchi nzima lakini mwongozo unachelewa. Tuwaombe Wizara waharakishe mwongozo kwa kuangalia ikolojia ya mahali husika ili wapande miti kulingana na mahitaji ya eneo husika, hilo litaweza kuwa na tija zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nilikuwa nikiwaza kidogo, kwamba kama tungekuwa tunafanya maamuzi haya ya kujumuisha pamoja; muda mfupi uliopita Serikali imejenga majengo mengi sana ya taasisi za Serikali kwa maana ya shule na hospitali; laiti tungeliongeza fedha kidogo halafu tukaweka mifumo ya ukasanyaji maji katika taasisi hizi maana yake ni kwamba tungekuwa na maji ya kutosha kwa ajili hasa ya kumwagilia miti hii ambayo tunataka ipandwe nchi nzima. Kwa hiyo wakati mwingine tunapokuwa tunakuja na hoja ambazo ni jumuishi tuone kwamba tunaweza tukalisaidia. Leo kama kila shule iliyojengwa ingekuwa na mfumo wa ukusanyaji maji au kila hospitali iliyojengwa ingekuwa na mfumo wa ukusanyaji maji tungeona kwamba maji yangekuwepo yakutosha. Hata kumwagilia miti itakayopandwa na hata ukame utakapokuja bado miti inaweza ikakua vile vile.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda uliobaki naomba nichangie kuhusu uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya makazi; na haya yanasimamiwa vizuri tu kwa bajeti iliyopo, kwa hiyo tunachosisitiza hapa na kuomba ni usimamizi wa taasisi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni kelele na mitetemo katika makazi ya watu. Bado tunashuhudia katika nchi ambayo tuko katika uchumi wa kati, nchi ya wastaarabu baada ya saa nne usiku tunashuhudia kelele kutoka katika vilabu, kutoka katika nyumba za ibada. Sijui kuna shida gani katika hili, lakini sio sawa, kwamba katika nchi ya wastaarabu bado tuendelee kusikia mziki anao upenda DJ wa klabu husika wakati mimi siupendi mziki kwa wakati huo na ninahitaji kulala; na mara nyingi imetusumbua tunakwenda mahali kufanya kazi katika mji husika lakini unalazimika kusikiliza mziki uliochaguliwa na klabu hadi saa nane usiku, hili jambo halipendezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tena kwa mara nyingine, NEMC wanaweza, mahali kwingine walikwenda na wakapiga stop na haikuendelea tena; lakini mahali kwingine wanatoa faini tu na bado watu wanaendelea kupigia watu kelele usiku. Tunadhani kwamba sisi ni nchi ya wastaarabu ambayo inapofika saa nne usiku hatuhitaji kuendelea kupigiwa kelele.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, na hili nalo linahitaji usimamizi wa kawaida tu. Mfumo wa ukusanyaji wa taka ngumu. Nilikuwa nataka nipendekeze kwa Wizara na taassisi husika. Kwamba, mbona sisi katika nchi yetu leo bado tunachanganya maganda ya ndizi na ya viazi pamoja na chupa ya coca cola na heineken iliyoisha halafu wote unakuwa ni uchafu mmoja upelekwe dampo, kwa nini? Yani tumeshindwa kama nchi kutoa elimu ya kwamba taka zinazotoka jikoni zitengwe mahali fulani, chupa zitengwe mahali fulani hata basi ziende zikatumike tena. Ninadhani tutatenda haki sana iwapo tutawaambia wananchi wetu waweze kutenganisha aina ya taka za nyumbani ili kwamba ziweze kutumika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu viwanda. Viwanda vingi sana vimejengwa katika maeneo ya makazi, na wakati mwingine viwanda hivyo vinatoa moshi mzito na kutiririsha maji machafu katika maeneo ya makazi. Kwa mfano ni wakazi wa Kibangu Makuburi. Viwanda vile vilivyoko pale EPZA vinaendelea kutoa moshi mzito pamoja na kutiririsha maji machafu. Hili hebu NEMC walisimamie vizuri. Kupiga faini peke yake hakutoshi, unapiga faini leo lakini tatizo bado lipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, sijui kama ni mimi binafsi lakini nadhani kwamba Watanzania wote tunaona. Sasa hivi maeneo ya mjini, hasa katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani utagundua kuna vituo vya mafuta vinajengwa katika makazi ya watu kila baada ya mita 100, na wakati mwingine vituo hivi vya mafuta viko upande wa kushoto na kulia mwa barabara ya lami. Sasa unajaribu kujiuliza, kwa nini hali hii iko hivyo? Hivi hatuoni hatari ya kwamba vituo vya mafuta viko katika makazi ya watu na wakati mwingine havina hata uzio? Hivi ikitokea ajali ya moto tutasemaje? Kwamba ni kwa sababu hatuwezi kusimamia? Au ni kwa sababu tumeona hii hali ya kujenga holela ya vituo vya mafuta iendelee katika makazi ya watu? Sidhani kama hili ni jema kwa usalama wa Raia wa nchi yetu. Tunaomba sana Wizara husika iweze kulishughulikia kwa ufasaha. Utitiri wa vituo vya mafuta katika makazi ya watu katika jiji la Dar es Salaam si afya na wala si jambo la usalama kwa usalama wa raia.

Mheshimiwa Naibu Spika,baada ya kusema hayo najua muda wangu unakwisha, naomba niunge mkono hoja, ahsante sana.