Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini pia nichukue fursa hii nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kwenye upande huu wa kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini zaidi katika suala zima la mazingira. Tumekuwa tukiona mara kwa mara amekuwa akienda katika Mikutano mbalimbali ya Kimataifa kuiwakilisha nchi yetu hasa kwenye suala zima la mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliamua nisimame hapa nizungumze baadhi ya mambo ambayo yamezungumzwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kwamba mengine yalikuwa ni ushauri, lakini bahati nzuri mengine wanahitaji wapate ufafanuzi kuona kwamba kama Serikali ni jitihada gani ambazo tumezichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na jambo hili ambalo limezungumzwa na Profesa Manya, suala la mitetemo na suala la changamoto za uchafuzi wa mazingira hasa kwenye masuala ya viwanda. Niseme tu kwamba sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, zipo jitihada mbalimbali ambazo tumezichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tumeshatoa maelekezo kwa upande wa makelele, tumekaa na nyumba za ibada, wenzetu ambao wengi wao wanakuwa wanapiga hayo makelele, lakini tumekaa na wamiliki wa baa, tumekaa na wamiliki wa maeneo na vitu vingine ambavyo kwa njia moja au nyingine wanasababisha hili suala zima la uwepo wa makelele yanayosababisha mpaka watu kushindwa kupata usingizi kama alivyosema katika nchi ya wastaarabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyozungumza baada ya sisi kutoa maelekezo, Maafisa wetu wa NEMC tayari wapo field wanafuatilia na kusimamia yale maelekezo ambayo kama Wizara tumeyatoa. Kwa hiyo, niwaambie tu Wahemishimiwa Wabunge hili jambo sasa tunakwenda kulikomesha kulifanyia kazi kama ambavyo wananchi wantaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa viwanda tayari tulishatoa maelekezo. Kwanza tulishawaelekeza wamiliki wote wa viwanda nchini wahakikishe kwamba wanatengeneza na kuweka mifumo rafiki ambayo itakuwa iko salama kwao na kwa wananchi, mifumo ambayo inatirisha maji. Kwa sababu ni kweli tulishuhudia baadhi ya viwanda wanatiririsha maji kwenye vyanzo vingine vya maji na maeneo mengine ya makazi ya wananchi, kitu ambacho kimekuwa kero kwa wananchi. Kwa hiyo, tumekwishatoa maelekezo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwahi pia kutoa maelekezo na tunaendelea kusimamia maelekezo yetu kuhusu suala zima la utoaji wa moshi na sumu nyingine katika viwanda hivi. Lengo na madhumuni ni wananchi wetu waweze kuishi katika maisha ya furaha zaidi kwa hiyo, niwambie tu Waheshimiwa Wabunge, suala la kero ya makelele, moshi, maji machafu na kero nyingine katika viwanda vyetu tumeshalifanyia kazi na utekelezaji umeanza na hivi tunavyozungumza vijana wetu wako field wanasimamia suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuja hapa hoja ya visiwa. Ni kweli niseme kwamba hii ni changamoto na niwambie tu kwamba kwamba tayari Serikali kupitia Ofisi ya Makamau wa Rais, tumeshaanza kujenga kuta kwenye baadhi ya maeneo. Tumeanza kule Kwesekwese Pemba, tumeanza kule Mikindani, Mtwara na niwambie tu wale wote ambao wana changamoto hizi, tutakuja tufanye utafiti lakini pia tutahakikisha kuwa tunatenga fedha kwa ajili ya kujenga hizo kuta. Kwa sababu athari za haya maji kuingia kwenye vipando, kuingia kwenye maeneo ya makazi imekuwa ni changamoto. Jambo la Nungwi tumeliona na maeneo mengine tumeyaona tunaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wao waendelee kuwa na Subira, Serikali tunarafuta fedha kwa ajili ya kujenga hizo kuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuja hapa vile vile hoja ya kwamba tuongeze fedha zaidi katika fungu la Serikali rather than kukaa na kutegemea kutoka kwa wafadhili. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge tu kwamba, miradi hii ina sehemu nyingi, sio kwamba tunategemea eti kutoka kwa wafadhili tu. Kuna miradi ambayo inatekekelezwa na NEMC ambayo ni Serikali, kuna miradi ambayo inatekelewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo ni Serikali. Sasa hilo fungu ambalo linatoka nje sio kwamba tunakwenda tu, lakini ni kutokanana makubaliano ya Kimataifa ambayo tunakubaliana wakati tunapokwenda kukaa katika vikao vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi ni lazima fedha hizi wao wazitoe kwa sababu asilimia kubwa ya uchafuzi wa mazingira, ukiangalia na ndio maana wanakubali kutoa fedha hizi kwa sababu ni wao ndio wanatuchafulia mazingira ya anga na mazingira mengine. Kwa hiyo, niwambie tu Waheshimiwa kwamba wazo hili tunalichukua tunakwenda kulifanyia kazi, tutajitahidi tuongeze fedha kwenye hili fungu la Serikali ili tuimarishe miradi ile ambapo tutahisi fedha kutoka kwa wafadhili hazitoshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuendelea tumepata pia hili jambo la kulipa kodi lile ambalo Waheshimiwa wanalalamika kwa upande wa Muungano. Nataka niwambie Waheshimiwa kwamba, kwanza nataka watu wafahamu kwamba Muungano huu ndio wengi wetu umetuleta hapa, sisi wengi wetu ni wanufaika wa Muungano huu. Wakati tunajibu maswali pale tulieleza kwamba kero hizi zilikuwa nyingi, lakini leo tumekwishafika kero 22, zimebakia kero nne, kero ambazo tayari timu zetu ziko katika vikao vya majadiliano ili kuhakikisha kwamba tunachanganua kero hizi. Sidhani kama Muungano huu unaweza ukadumu kwa zaidi ya miaka 50 halafu ukawa una changamoto nyingi rather than mafanikio. Kwa hiyo, wakati tunahesabu changamoto za Muungano huu, basi tuhesabu zaidi mafanikio ya Muungano huu. Wapo waliosema kwamba wengine wana asili ya pande zote mbili kwa sababu ya umuhimu wa Muungano huu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)