Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Kwa hakika leo katika Bunge lako tumeshuhudia mjadala mzuri uliogusa upande wa Mazingira, lakini na upande wa Muungano. Pia naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa aliyoifanya na anaendelea kuifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi naomba niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe ambao wamenipa dhamana ya kuweza kuhudhuria katika Bunge hili, kwa hakika sina cha kuwalipa Mungu ndiye atakae walipa. Pili, nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nilivyosema awali, Makamu wa Rais kama kiongozi wangu katika Ofisi lakini halikadhalika Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikishukuru sana kiti chako hiki ndicho kimetuendeshea mjadala mzuri sana katika sehemu nzima ya Muungano na Mazingira. Nipende kuishukuru familia yangu kama nilivyosema awali kwa utulivu mkubwa wanaonipa ili niweze kufanya kazi yangu ya kutimiza majukumu haya ya kitaifa, Nawashukuru sana familia yangu kwa ujumla. Niwashukuru pia Mabalozi wa mazingira na wadau wote mbalimbali wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri zimekuja hoja mbalimbali na katika hili tumepata hoja kutoka katika Kamati zetu, Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, halikadharika Kamati ya Maji na Mazingira. Naomba niwahakikishie Wanakamati kwamba yale yote ambayo yametolewa kama maoni ya kamati, ni jukumu la Ofisi yetu kuhakikisha kwamba tunaenda kuyatekeleza na hasa kuangalia masuala yale ya kuwakilisha upande wa Muungano na Upande wa Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, hususani katika Kamati ya mazingira nilikokoteza ajenda ya upande wa Bajeti halikadhalika lakini NEMC kuwa mamlaka kuondokana na hadhi iliyo nayo sasa hivi. Naomba niwahakikishie katika suala zima la kuifanya NEMC kuwa Mamlaka, sasa hivi tunapitia Sheria yetu ya Mazingira, Sura Namba 191 na katika hili eneo hilo lipo na linafanyiwa kazi. Kwa hiyo, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati kwamba eneo hili linafanyiwa kazi kwa kina, vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hoja yetu hii imechangiwa takribani 11, ukiacha wawili ambao ni Wenyeviti wa Kamati, lakini tisa waliongea moja kwa moja hapa Bungeni ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru maoni yote yaliyotolewa, kwa upande wangu nasema haya yote ni maoni especially katika upande wa mazingira. Kulikuwa na suala zima la bajeti. Ni kweli tumeliangalia tumeona hata katika Kamati, naomba niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati waliliona hili. Hata hivyo, tumesema kwamba tumeanza tulikotokea, ukiangalia bajeti yetu tulianza na bajeti ya ndani wastani wa milioni 400 na huko nyuma ilikuwa hakuna kabisa, leo hii tumefika 1.6 billion. Katika hili tumshukuru sana Mheshimiwa Rais hasa katika kutafsiri maana ya mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwambie Waheshimiwa Wabunge, ukiachia hii bajeti inayopita katika Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo sisi kazi yetu kubwa ni suala zima la uratibu upande wa mazingira. Wizara mbalimbali za kisekta zimekwenda kutekeleza suala zima la ajenda ya mazingira na hii ndio maana nasema tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukiangalia katika bajeti ya mazingira, tumechimba malambo, ujenzi wa visima virefu katika maeneo mbalimbali, lakini maelekezo ya Mheshimiwa Rais katika Wizara za Kisekta ndio maana kupitia Wizara ya Kilimo kwa mfano, imetangaza kandarasi za ujenzi wa malambo takribani 10 yenye wastani wa Shilingi Bilioni 100. Yote hii ukiunganisha Wizara za Kisekta fedha ambazo Serikali imeelekeza katika Sekta ya Mazingira ni fedha nyingi zaidi. Hata hivyo, tumechukua concern ya Kamati na concern ya wajumbe. Ni kweli kazi yetu kubwa sasa katika Ofisi ya Makamu wa Rais, baadaye kuona ni jinsi gani tunapata bajeti kubwa ya kutosha ili kusaidia baadhi ya miradi mingine ya mazingira iweze kufanya kazi katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wizara ya Mifugo halikadhalika, tumeona katika maeneo ya Simanjiro kule tumejenga mabwawa na malambo ya kunywesha mifugo. Pia Wizara ya Mifugo imetenga bajeti kubwa vile vile kwa upande wa mifugo, lengo letu ni nini? Ni kuhakikisha jinsi gani kazi zote kwa pamoja zinasaidia katika ujenzi wa shughuli za mazingira hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni suala zima la biashara ya hewa ya ukaa. Ni kweli naomba niwaambie ndugu zangu Wabunge, tulikotoka mwanzo ni kwamba hapa tulikuwa kabisa hatusomeki vizuri, ni halmashauri pekee ya Tanganyika ilikuwa inasomeka kwa mwaka inapata collection takribani kwa wastani wa Shilingi Bilioni tatu kwa Mwaka. Ni fedha nyingi zaidi, ndio maana Ofisi Makamu wa Rais iliamua kuandaa mwongozo na kanuni kama nilivyosoma katika hotuba yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuna Kanuni ya Biashara ya Hewa ya Ukaa. Imani yetu kubwa katika kupitia biashara hii ya hewa ya ukaa na kanuni tulizozitengeneza, tutakwenda kufungua mlango mpana wa upataji wa fedha itakayosaidia miradi mbalimbali na hususani miradi ya kimazingira. Katika hili nipende kuipongeza Halmashauri niliyoisema ya Tanganyika, kwa kweli imeonesha mfano ndani ya nchi yetu. Naomba niwambie Waheshimiwa Wabunge, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Idara ya Mazingira na Kituo chetu cha Carbon Monitoring Centre hivi sasa tunafanya registration ya watu wanaokuja kwa ajili ya biashara ya hewa hii ya ukaa na hili ndugu yangu Chumi aliuliza, je, hivi sisi tunaopanda miti tunahusika?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwambie biashara hii ya hewa ya ukaa itawahusu watu wa TFS ambao wana misitu inahifadhiwa, itahusu halmashauri yenye Misitu ya Halmashauri, itahusu vijiji vyenye Misitu ya Vijijii, itahusu watu binafsi wenye misitu yao waliyoipanda wao wataingia katika biashara ya hewa ya ukaa. Kanuni ziko wazi katika eneo hili, niwaombe Watanzania hii ni fursa kubwa sana kwamba nchi yetu tunakwenda kufungua mlango mwingine mkubwa wa kujenga uchumi kupitia biashara ya hewa ya ukaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lingine ambalo lilizungumziwa hapa ni suala zima la uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro. Ni kweli Mlima Kilimanjaro ni tunu yetu tuliyokuwa nayo, ni lazima tuilinde. Bahati nzuri mwaka 2022 nilishiriki wakati tulipopata ile changamoto ya moto na kweli hali ilikuwa ni mbaya. Ndio maana sisi kupitia ofisi yetu tuliamua tutengeneze utatu TFS, Ofisi ya Makamu wa Rais, lakini wenye Mamlaka ya kuhifadhi huo Mlima ambao ni wenzetu wa KINAPA na jambo linaenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, timu hiyo imeanza kuratibu vizuri na concept paper imeshaanza kuandikwa na naomba niwambie Watanzania, tunaenda kufanya tafiti kuangalia ni jinsi gani tunaweza kuilinda barafu ya Mlima Kilimanjaro, kwa sababu hii ndio tunu yetu ambayo inatuletea utalii mkubwa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande mwingine ni upande wa Muungano. Nishukuru sana hoja mbalimbali zimeletwa katika Muungano, naomba niwahakikishie kama alivyosema Naibu wangu hapa ni kwamba tumefanya kazi kubwa na katika hili tumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mchakato wa kushughulikia hoja za Muungano ulianza toka mwaka 2006, mwaka 2010 hoja mbili za Muungano zilipatiwa ufumbuzi na mwaka 2020 hoja tano. Kwa hiyo, kati ya hoja 25, katika hiyo miaka yote zilitatuliwa hoja saba tu za Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka miwili ni hoja takribani hizi tunazosema 18 tumeongeza zile hoja zingine sasa hivi, hii yote ni kazi kubwa imefanyika ndugu zangu. Katika hili mnyonge mnyongeni, lakini Mama Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamefanya kazi kubwa kutatua hizi hoja za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu bado kuna makandokando mengine na hasa usafirishaji wa mizigo. Hili tulikubaliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha na hasa mambo haya mengine ni mambo ya uratibu tu na kiutendaji na hili Wizara ya Fedha wamesema wanalichukua kwenda kulifanyia kazi. Imani yangu, hizi kero tunazoziona sasa hivi kwa kadri tulivyokubaliana jambo hili tutapata ufumbuzi na tutaondoa kabisa kero hizi ndogo ndogo ambazo tunasema ni petty issue katika mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya ajira haya tutayafanyia kazi, tunashukuru ushauri wenu tunaenda kuratibu vizuri kuangalia katika taasisi zetu za Muungano, lengo letu ni kuufanya Muungano wetu kuwa rafiki zaidi, naomba niwaambie Muungano wa Tanzania ni unique, leo hii tuko humu ndani huwezi ukamtofautisha Wakojani wala huwezi ukamfananisha wa Bagamoyo wala wa Kakonko wote tuko pamoja hapa, hakuna nchi ambayo inanufaika na matunda mazuri kama haya ya Muungano tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu letu kubwa ni kuuenzi Muungano wetu na hasa ndugu zangu nawaambia kazi kubwa wanayofanya Viongozi wa nchi yetu, tuwaenzi kwa hii tunu waliyotupatia tuendelee kuulinda Muungano wetu. Bahati nzuri Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza mwaka huu sherehe ya Muungano mwaka huu isherekewe tofauti kila Mkoa watu washerehekee Muungano wafungue miradi, wapande miti na mambo mengine yote, jambo hili maana yake tunaleta urafiki, humu leo Bungeni watu wameoana Bara na Visiwani, hongera sana kwa Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya ndugu zangu naomba nishukuru sana, hoja zote tumezichukua kwa ajili ya kuzifanyia kazi naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.