Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Nami nichukue nafasi hii kupongeza walioaminiwa na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Wizara hii ya Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, Naibu wake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa utendaji mzuri ambao kwa hakika sisi kama Wabunge ambao tumepewa dhamana na Mheshimiwa Spika katika Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria ambayo tunaisimamia Wizara hii, tunaona namna ambavyo wanaitendea haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia utendaji wa wateuliwa wengine ambao wameaminiwa katika Wizara hii wakiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama, DPP, Solicitor General kwa kazi zao nzuri ambazo wanazozifanya. Mmeona wenyewe aliposimama Ole-Gabriel hapa, makofi yalikuwa mengi sana; ni kwa sababu ni mtu ambaye ana ushirikiano na wenzake na ni mtu ambaye anafikika kirahisi sana. Kwa hiyo, utendaji wake unaonesha ni namna gani ambavyo anastahili kuwepo katika nafasi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijikite katika kushauri, baada ya kutembelea na kuona majengo mazuri ambayo yamejengwa na Serikali kupitia Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Wizara hii ya Katiba na Sheria majengo ya Mahakama Jumuishi, na Mahakama za Mwanzo nyingi ambazo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti hapa amezitaja. Ni kwamba anaendelea kuonesha kwamba dhamira ya Nchi hii ya utoaji haki kuwa katika sehemu ambazo ni nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na changamoto kubwa hapo nyuma ambapo ukipita vijijini kwetu, wilaya na miji yetu, jengo lililokuwa baya sana ni la Mahakama, lakini sasa imekuwa kinyume chake, kwa sababu Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia ambao amewaamini kufanya kazi kwa niaba yake, wanafanya kazi vizuri na kwa weledi mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijikite kwenye jambo dogo tu na nichukue nafasi hii kulizungumzia, ni Tume ya Kurekebisha Sheria. Kuna sheria ambazo zinakizana na zipo lakini nyingine za miaka mingi sana. Kuna sheria za miaka ya 1970, na nyingine tumerithi kwa mkoloni, lakini zipo na still zinafanya kazi. Matokeo yake utendaji haki unakuwa haufanyiki vizuri. Sababu ni nini? Tunaendelea kuiomba na kuishauri Tume ya Mahakama iende ichakate sheria nyingi ambazo zinakizana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tu leo katika Bunge lako kipindi cha asubuhi, kulikuwa na hoja zilikuwa zinazungumzwa hapa kwamba kuna sheria zinakizana; Sheria ya Ndoa, Sheria ya Mtoto na Sheria ya Elimu. Hizi sheria zikitengenezwa vizuri, mgogoro ni mdogo sana kuliko tunavyodhani na tunavyoubeba. Ni nani anayehusika? Ni Tume hii ya Kurekebisha Sheria, inatakiwa ije na mchakato mahususi maalum ambao utafanya sasa tutoke katika kusuguana humu, sheria ipi ni bora na sheria ipi siyo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kukubali mchakato wa Katiba. Mchakato wa Katiba utaondoa manung’uniko machache ambayo yapo. Sisi ambao tunaamini Katiba hii ni nzuri, ni marekebisho kidogo tu ambayo inaweza ikayafanya. Nampongeza Mheshimiwa Rais katika hii Legal Aid Campaign ambayo anaifanya. Kwa kweli itawasaidia sana watu wetu ambao hawana uwezo wa kuweka mawakili ili kupata msaada wa kisheria. Kampeni hii pia itatoa elimu pana kwa mashauri mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Tume hii ya kurekebisha sheria, kuna mambo ambayo yanazungumzwa sana hapa sasa hivi kwenye mitandao na watu wetu, na katika Bunge lako Tukufu hili. Hapo nyuma kulikuwa na jambo ambalo linazungumzwa kuhusu ushoga la usagaji. Sheria za Ushoga zipo wazi sana, lakini Sheria za Usagaji bado zimejifumba, hazipo wazi. Atahukumiwaje msagaji na yule anayesagwa? Kwa hiyo, tunaiomba sana Tume ya kurekebisha sheria ije na hili, ilichakate ili kuja na sheria ambayo itatoa adhabu kali kwa hawa watu. Kwa sababu kwa sura iliyopo sasa hivi, ulawiti kwa watoto na kwa watu wa namna yeyote sheria zake zipo, lakini usagaji sheria imekaa kimya. Kwa hiyo, naomba sasa Tume hiyo ya Kurekebisha Sheria ije na mchakato huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nitapenda kulizungumzia kwa muhtasari tu kidogo, naona dakika zetu siyo nyingi; mwaka 2022 kwenye taarifa zilizopo ambazo siyo rasmi lakini ni za kweli, ni kwamba watoto waliolawitiwa mwaka 2022 ni 1,555. Kati ya hao, watoto 1,358 ni watoto wa kiume. Watoto wa kike waliolawitiwa ni 197. Ni jinsi gani tuone janga hili kwamba sasa limekuwa janga la Kitaifa. Kwa sababu gani? Tumekuwa tuna mchakato wa muda mrefu. Katika Bunge hili, miaka hii miwili tumekua tunaona hosteli zinajengwa nyingi hasa za sekondari kwa ajili ya wasichana, tumesahau vijana hawa, ambao ni watoto wadogo ambao sasa janga hili limehamia kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Tume hii ya Kurekebisha Sheria nayo ione. Pia Serikali iione kwamba sasa tutoke tulipokuwa tumejikita, tuone sasa wamehamia badala ya kukimbia kwa wa miaka 30, wanakimbilia kwa vijana wetu. Jambo hili ni hatari kwa jamii na tunaenda kutengeneza jamii ambayo baadaye sio mwanaume; atakuwa na sura ya kiume, lakini sio mwanaume. Sasa hawa wadada ambao wanakua, watapataje wanaume? Hilo nalo ni changamoto nyingine. Naomba tulisimamie hili kwa dhamira nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba kuishauri Serikali kupitia DPP, Solicitor General na AG. Uhalifu wa mitandaoni sasa unashika kasi sana. Ni vyema sasa na wao wakaenda na huu upepo wa kidunia, kwa sababu itabidi Mawakili wa Serikali kwenda kutetea kesi za mitandaoni, Waendesha mashtaka wataenda kuendesha kesi zinazotokana na wizi wa mitandaoni, na Mwanasheria Mkuu hivyo hivyo. Kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie na itoe elimu pana kwa Mawakili wetu wa upande wa DPP na upande wa Wakili Mkuu wa Serikali ili wapate elimu hii pana ya wizi wa mitandaoni ili waweze kunusuru watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)