Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Wizara hii nyeti Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo utajikita katika Tume ya Haki za Binadamu, Fungu 55. Katika Ibara ya 130 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katiba imeweka wazi kabisa majukumu inayopaswa kutekelezwa na Tume hii ya Haki za Binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma majukumu haya kwa umakini na kwa umakini utaona namna ambavyo tume hii imepewa majukumu mazito sana, majukumu nyeti, majukumu ambayo yasipotekelezwa kwa ufanisi wake Taifa hili litajikuta liko katika hatari kubwa sana ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo hiki kwa maana ya Tume ya Haki za Binadamu pamoja na majukumu mengine tume hii ina wajibu wa kumulika taasisi zote za Kiserikali kuangalia kama misingi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora vinasimamiwa, vinatekelezwa kwa ukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu hili ni kubwa sana na ukiangalia ukubwa wa majukumu ya tume hii utakubaliana na mimi kwamba Bajeti ya Tume hii inapaswa kwenda sambamba na uzito wa majukumu yaliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla sijaendelea mbele naomba nilipitishe Bunge lako Tukufu katikati ya Bajeti za miaka mitatu mfululizo ya Tume hii ya Tume ya Haki za Binadamu ili kwa pamoja tuangalie kama kweli bajeti hii inaendana sambamba na majukumu mazito ambayo tume hii imekabidhiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022 tume hii iliomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 373.6. Nafahamu wewe ulikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, unafahamu vizuri majukumu haya. Katikati ya majukumu haya tume inaomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 373.6 pekeyake. Hiyo kama haitoshi, fedha hizi kwa 100% ni fedha za kutegemea wahisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofika hatua Taifa lianweka rehani haki za Watanzania kwamba sasa wahisani ndiyo waje sasa kulinda haki zetu nchini, tunapotea na tunazidi kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa Fedha wa 2022/2023, tume hii iliomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 115 tu. Kumbuka mwaka uliopita ilikuwa ni shilingi milioni 373 nayo ilikuwa ni ndogo tulipiga kelele. Sasa ikaenda mwaka unaofuata ikasema sasa hatuhitaji hata hiyo mia tatu sabini na kitu. Ikasema tunahitaji shilingi milioni 115 tu ambazo fedha hizi kwenye Wizara zingine hata kwenye baadhi ya mafungu ya Katiba na Sheria ni fedha za viburudisho tu, chai yaani chai na korosho, lakini tume inatuambia inahitaji milioni 115 kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kulinda haki za Watanzania, this is a joke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, milioni hii 115 iliyoombwa mpaka Februari mwaka huu haijatoka hata shilingi moja. Ina maana gani hii? Ina maana ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 Tume hii ya Haki za Binadamu ilikuwa ofisini kabisa inakula bata. Kwa sababu fedha hizi ni fedha za maendeleo na tume hii ili uweze kutoka na kwenda kutekeleza wajibu wake lazima fedha ya maendeleo iwepo kwa 100%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituko kingine sasa mwaka huu wa fedha ambao sasa tuko hapa tunajadili bajeti ya Tume hii ya Haki za Binadamu, tume hii imesema yenyewe haina kazi kabisa ya kufanya. Yaani haiihitaji hata shilingi mia kutimiza wajibu wake na kwa lugha nyingine tume hii inataka kulieleza taifa au inataka kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba uvunjwaji wa Haki za Binadamu nchini umeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haujaisha na ndiyo maana Mama yetu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kila anapokutana na watu kila anapokwenda anakemea juu ya uvunjifu wa Haki za Binadamu. Wabunge wengine wamesema lakini hata vyombo vingine vinavyosimamia ambavyo siyo vya Kiserikali ambavyo vinasimamia vinafuatilia mwenendo mzima wa Haki za Binadamu nchini wanasema ukiukwaji wa Haki za Binadamu nchini kwa sasa ni mkubwa kuliko wakati mwingine ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwamba fedha hizi kwa 100% ni fedha za wahisani. Utakumbuka kwa sasa taifa au niseme dunia kila nchi sasa hivi inapambana na hali yake kupambana na mapenzi ya jinsia moja kwa maana ya ushoga. Asilimia kubwa ya wahisani ambao wanasaidia nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania ni wale ambao wanaamini kwamba mapenzi ya jinsia moja ni Haki namba moja ya Binadamu; which is not true.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea kutegemea fedha za wahisani matokeo yake ndiyo haya tume inakaa ofisini haina kazi ya kufanya, ni watumishi ambao wana ajira za kudumu, wanalipwa mishahara inayotokana na kodi za Watanzania ambao ndiyo wanyonge hao hao ambao haki zao zimebinywa, zimepokwa na wanalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili halikubaliki na niseme kabisa Waziri atakapokuja ku-wind up hapa atueleze hivi anadhani tume hii inapaswa kuendelea kuwepo? Tume ya kukaa ofisini, tume inayokuja leo inasema tunahitaji mtupitishie bajeti tu ya mshahara na viburudisho, sisi hatuna kazi ya kufanya. Waziri asiponipa majibu yanayojitosheleza, siku ya leo nitakwenda kukamata shilingi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niendelee kusema katikati ya changamoto za Tume ya Haki za Binadamu, tume ambayo haifanyi kazi kabisa kwa sababu kwanza haina fedha inahitaji uwe na kiongozi mwenye moyo wa kujali na kulinda Haki za Binadamu kama Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan ambaye aliona kwa jicho la pembeni kwamba tume hii siyo tu imelala, yaani imeshajivua wajibu wake kabisa wa kikatiba ndipo alipoamua baada ya kusikia kelele za Watanzania kutokana na haki zao kupokwa akaamua kuunda Tume Maalum, Tume Maalum ambayo kazi yake ni kuchunguza mwenendo wa Haki za Binadamu nchini. Jukumu ambalo kikatiba wamekabidhiwa tume ya haki za binadamu na kwa lugha nyingine kuwa na tume nyingine hii ambayo Mama yetu Samia Suluhu Hassan ameiona na huenda asingeiweka tungekuwa katika hali ya hatari sana ya ukiukwaji wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lugha nyingine ni kwamba kwa sasa hivi Tume hii ya Haki za Binadamu imeisababishia Serikali kuingia gharama nyingine ya kuunda tume nyingine ya kufanya majukumu yake yale yale wakati tume yenyewe iko ofisini na mshahara unaotokana na kodi za Watanzania wanachukua kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Nimekuwa nikijiuliza na niliwahi kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwenye kamati, nikasema; Tume ya Haki za Binadamu ina jukumu la kumulika taasisi za Kiserikali ili kuona kama Haki za Kibinadamu zinatendeka na nikasema kama ndiyo hivyo, tumekuwa tukimwona CAG akileta taarifa zake hapa Bungeni za kila mwaka na tumekuwa tukiona vituo vingine visivyo vya kiserikali viantaoa taarifa zake mfano kama hii hapa nikipata muda wa kuielezea nitaielezea ni kwa nini basi tume hii yenye wajibu wa kikatiba isiwe inaleta ripoti yake ya uchunguzi wa mwenendo wa haki za binadamu hapa Bungeni? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Agnesta.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Agnesta muda wako umekwisha.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.