Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia hoja ya Waziri wa Madini ambayo inatamani tupitishe Bajeti ya shilingi 89.3 kwa ajili pia ya malengo makubwa ya kukusanya maduhuli yanayofikia Trilioni
1.006 na nitangulie kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwamba kesho yetu ya madini kama sekta ni kesho njema na hivyo tuunge hoja mkono kwa kupitisha Bajeti yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ambazo tumeshuhudia ukuaji wake mwaka hadi mwaka ni sekta ya madini na ni kweli kwamba kwa mwendo ambao tunakwenda nao ile asilimia 10 ya kuchangia Pato la Taifa kufikia Dira yetu ya Taifa ya mwaka 2025 itaweza kufikiwa bila shida. Hii inatokana na maono makubwa ya Wakuu wetu wa Nchi lakini pia na uongozi mzuri wa Wizara na Taasisi zilizo chini yao, pia na uelewa mkubwa wa wadau kwa maana ya wachimbaji wakubwa na wadogo pamoja na watu wote ambao wanajihusisha na sekta ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nitoe pongezi za dhati na za pekee sana kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa diplomasia yake ya hali ya juu. Hii ni kwa sababu katika ile ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani tulisikia ahadi ya kujengewa kiwanda kinachotengeneza betri kwa kutumia madini yetu ya nickel. Huu ni ukombozi mkubwa na lazima tumpongeze sana Rais jinsi ambavyo anajua kutumia diplomasia yake katika kuvutia uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachochagiza ukuaji huu wa sekta pamoja na mambo mazuri ambayo tunayashuhudia ni pamoja na yale mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017. Ni kweli kwamba hatua kubwa imepigwa na hasa katika kuwawezesha Watanzania kushiriki kutoa huduma katika migodi lakini pia na kuwahudumia wachimbaji wadogo, kama kuna Wizara inatamani kujua namna local content inavyotekelezwa waende Wizara ya Madini. Kwa hiyo, hilo ni jambo la kujivunia na tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo katika miaka hii Sita ya kuwepo kwa Sheria ya Madini ni muhimu pia tukafanya tathmini kuona kama zile fikra tulizokuwa nazo mwaka 2017 zinatekelezeka zingine au zingine hazitekelezeki na kwa jinsi hiyo kuna mambo ambayo kama Wizara wanaona kwamba hayakuwa sawa na matarajio basi yanaweza yakaletwa ili kwamba yaweze kurekebishwa na moja ya mambo kama hayo ni leseni hodhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni hodhi zimerudishwa Serikalini kwa njia ya sheria lakini wawekezaji nao bado ni kama hawana ridhaa nalo, lakini pia wachimbaji wadogo wanaziangalia na kuzichokonoa fulani kwa hiyo unakuta kwamba siyo sisi wala Serikali wala wawekezaji wanaonufaika nadhani hili Mheshimiwa Waziri anaweza akaona kama ndani ya muda huu linamletea shida, basi anaweza likafanyiwa marejeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wakati Tume ya Madini inaanzishwa ilileta pamoja watumishi ambao walikuwa na viwango tofauti vya mshahara, na ilitegemewa katika kuleta upatanifu na ulinganifu, wale wadogo wasogezwe katika wale waliokuwa na mshahara mkubwa, lakini jambo hili halikufanyika hivyo badala yake wale wakashushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linapunguza morale na wakati ambapo ndio watu unaowategemea waweze kukusanya maduhuli ya trilioni moja. Sasa hawa ni watumishi, walikuwa juu halafu wakashushwa na ukiangalia hiyo payroll kama mtu alikuwa ana commitments zake huko nyuma, wengine walipata mshahara negative (hasi), anaendaje kukusanya maduhuli huku hana fedha? Kwa hiyo, hili nadhani liko kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Simbachawene Wizara ya Utumishi hebu vuta mafaili ungalie hawa watu, kwa sababu pia wakati mwingine Serikali tujifunze kulipa ujira sawasawa na kazi ya mtu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anakwenda Mererani kilomita mbili anakwenda kuchukua Tanzanite ya bilioni tatu halafu anapoileta juu badala ya kuthaminisha mshahara wake unahesabika maelfu kadhaa. Nadhani tujifunze kulipa kwa kadri ya ujira wa mtu. Siyo sawa mtu aliyezama kilomita Mbili analeta madini ya thamani ya bilioni tatu mshahara wake mwisho wa mwezi unahesabika. Yeye si naye ana roho, nyama na damu jamani au? Kwa hiyo, hilo nadhani Mheshimiwa Simbachawene unaweza ukaliangalia hebu livute katika mafaili yako wasaidie hawa watumishi wa Tume ya Madini ili morale yao ipande ili waweze kukusanya maduhuli ya Trilioni 1.006. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye hoja yangu ambayo nataka kuichangia asubuhi hii ya leo. Siasa za Kimataifa zina makundi ya wenye uchumi Nchi Saba tunawaita G7, pia siku za karibuni kuna kundi la watu wanaitwa BRICS hawa ni Brazil, Urusi, India pamoja na China na Afrika Kusini. Hawa watu katika kujaribu kuondoa matumizi ya dola kwa sababu ni kama ni makundi yanayoshindana wameamua kwamba wao watakalolifanya kubwa ni kununua dhahabu kwa wingi, kuweka akiba katika nchi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naleta siasa hizi za Kimataifa katika mjadala wangu asubuhi ya leo? Hoja hapa ni kwamba kama hawa ambao wanajaribu kuona kwamba ili uchumi wao uweze kutengemaa wanaiona dhahabu kuweka akiba kama njia ya kuimarisha uchumi kwa maana ya kwamba wakati ujao yawezekana nani ajuaye dola yawezekana isiwe na nguvu katika kufanya biashara ya Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kwamba na kwa sababu pia sheria yetu inaturuhusu Kifungu cha 88 cha Sheria ya Madini, Kifungu Kidogo cha Pili kinasema mrabaha hapo mbele uweze kukusanywa kwa thamani ya madini yaliyosafishwa (refined gold) ili itusaidie na sisi kama nchi tuweze kuwa na akiba ya dhahabu, ili tuweze kulinda na kutegemeza uchumi wetu ambao unaendelea kukua siku kwa siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kwamba dhahabu tunayo, refinaries, tunazo hebu sasa tufikirie yaani ifikie mahali tunapopanga mipango yetu ya uchumi na kuukuza basi tununue dhahabu na kuiingiza katika benki yetu ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu nyingine niongee habari ya Liganga na Mchuchuma kidogo, pamoja na kwamba inapenda kuongelewa katika Wizara ya Viwanda lakini bado ni madini na wala siyo bidhaa hadi pale yalipo kwa hiyo ni sawa tu kuiongelea katika muktadha wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Liganga kuna chuma, vanadium na titanium. Madini yote ambayo yana thamani kubwa sana, lakini pia Mchuchuma kuna makaa ya mawe mazuri kabisa na kimsingi ndio huwa kuelelezo cha makaa ya mawe katika mfuatano wa madini Tanzania. Sasa hawa watu walipewa leseni kwenye kampuni ya ubia mwaka 2014 na sheria zetu za madini zinawaruhusu angalau miezi 18 wawe wameanza uchimbaji hawajaanza.

MWENYEKITI: Malizia mchango wako Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninakushukuru kwa hayo, wakati mwingine Mungu akijaalia. (Makofi)