Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na afya njema kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu na leo kuwa miongoni mwa wachangiaji kwenye hotuba hii ya Wizara ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiongoza nchi yetu na ninaamini kabisa kupitia Wizara hii malengo na mafanikio ya kujenga uchumi imara yanaenda kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa, nilikuwa nikipitia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini na katika maelezo yake kwamba, sekta hii ya madini hadi kufikia Septemba, 2022 imechangia takribani asilimia 9.7 kwenye pato la Taifa. Ni jambo la kupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naamini kabisa kwamba jitihada hazijafanyika za kutosha kwa sababu nchi hii maeneo mengi yana madini. Wachimbaji wadogo wadogo na wachimbaji wa kati bado hawajawezeshwa hatimaye kuweza kuisaidia nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa yake hii Mheshimiwa Waziri, imeonesha pia kwamba, madini yamechangia kiasi cha Dola milioni 3,395 ambayo ni sawa na asilimia 56 ya mauzo ya nje. Hili ni jambo zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, zipo changamoto ambazo wenzetu wa Wizara ya Madini ni lazima wakubali kuzipokea na waweze kuwasaidia hususan wachimbaji wadogo wadogo. Moja ya maeneo ambayo nilikuwa nataka niyaseme na ambayo nimeona Serikali ya Mheshimiwa Rais imefanya ni ya kupeleka umeme katika maeneo ya wachimbaji. Ni jambo la kupongeza sana. Ni takribani kama miezi miwili iliyopita, Mheshimiwa Rais alikutana na Wizara ya Nishati akisaini mikataba. Moja ya maelekezo yake ilikuwa ni kutoa maelekezo kwamba miradi ile mikubwa iende katika migodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameona kwamba madini haya hayachimbwi ipasavyo. Uwekezaji umekuwa una gharama sana kwa sababu, wachimbaji wanakuwa wanatumia mafuta ya dizeli, sasa kitendo cha Mheshimiwa Rais na Serikali yake kuamua kupeleka umeme mkubwa kwenye machimbo haya maana yake unaenda kuwezesha uchumi wa wananchi hatimaye na Taifa kwa ujumla. Ni jambo la kupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kuchangia ni Sheria yetu ya Leseni ambayo inaruhusu kukata leseni kupitia mtandao. Ni sheria nzuri sana, lakini sheria hii ina matobo ambayo ni lazima sisi kama Waheshimiwa Wabunge tuiangalie na tuweze kuirekebisha. Leo hii mtu anaweza kuomba leseni akapata leseni hata katika jengo letu la Bunge hili bila kutazama kwamba hapa pana nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niliseme hili kwa sababu, limekuwa likileta migogoro sana, hususan katika maeneo ambayo yana wachimbaji, kama Kilindi na maeneo mengine. Mtu anapata leseni halafu anamkuta mwenye shamba pale. Sheria hii inatenganisha Sheria ya Ardhi na Madini. Sasa haimpi haki mwenye ardhi, au mwenye shamba. Sasa hili limekuwa na mgogoro mkubwa sana; na hili kwa kweli lazima tulitazame. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji anaweza akapata leseni pale, akaanza kuchimba, anaanza kuingia mgogoro na mwenye ardhi. Sasa ni lazima tutazame na tujifunze kupitia maeneo mengine. Tutembee maeneo mengine tuone: Je, wenzetu wameweza kuepuka migogoro namna gani? Tuone namna ambavyo kama mwekezaji akipata aneo akamkuta mkulima pale, basi zile shares zisiwe diluted. Hii ndiyo namna pekee ambayo inaweza kumsaidia mwenye eneo lake. Hili limeweza kufanikiwa katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matobo mengine ambayo ni mabaya kabisa, sheria hii kwa kiasi kikubwa inachangia kuongeza deni la Taifa. Naomba niliseme hili kwa mifano. Unakuta barabara inatakiwa kujengwa, mkandarasi anapotaka kuanza kujenga barabara anakuta sehemu ya mawe. Anapotaka kutengeneza kokoto, siku mbili kabla hajaanza site, kuanza kujenga barabara anakuta eneo limetolewa leseni. Mtu katumia shilingi 50,000, yule aliyepewa leseni anaanza kuomba kuanza kufidiwa. Sasa hili limeleta shida kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano mmoja. Tunayo barabara yetu ambayo inatoka Handeni – Kiberashi hadi Singida, mkandarasi aliweza kuchelewa zaidi ya miezi minne kwa sababu, eneo ambalo alikuwa anataka kuchimba kokoto, alikuta tayari mwekezaji kapewa leseni na muda wote alikuwa hajapewa leseni. Jambo hili ukitaka kuangalia, kuna syndicate kati ya watumishi wachache wa Wizara ya Ujenzi na wenzetu wa Madini. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuona namna gani ya kubadilisha sheria yetu ili isiweze kuruhusu Serikali kuingia gharama kubwa kutokana na sheria ambayo tumeitunga wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hotuba hii. Ahsante sana. (Makofi)