Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nashukuru pia kwa kupata nafasi ya kuchangia. Naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa taarifa yake nzuri ambayo ameitoa. Kipekee naipongeza Serikali kwa ujumla, Mheshimiwa Rais na Serikali nzima kwa kazi nzuri ambayo tunaendelea kushuhudia inafanyika kwenye diplomasia ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulialikwa juzi kwenda kushuhudia uwekaji sahihi wa uwekezaji wa madini; niyaite madini adimu (rare minerals). Hizi ni dalili kwamba tunaendelea kuungwa mkono huko nje na watu wanaendelea kutuelewa; na ni dalili kwamba Wizara inafanya kazi yake vizuri. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana watu wote wanaofanya kazi na Mheshimiwa Waziri na kumpongeza sana Katibu Mkuu mpya kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kielelezo cha kwamba kazi zinakwenda vizuri ni mafanikio ambayo yamefika sasa kwenye asilimia 9.7 ya malengo ambayo yaliwekwa na Serikali na Bunge hili ili kuweza kuchangia uchumi kwenye bajeti ya nchi. Jambo hili haliwezi kufanikiwa kama Wizara haizungumzi lugha moja. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio makubwa ya Wizara hii yanatokana na mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo kwa taarifa ya Wizara, wanachangia takribani asilimia 40 ya mauzo ya dhahabu nje ya nchi. Jambo hili ni kubwa na hatuwezi kuliacha lipite hivi hivi. Kwa nini tumefanikiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanikiwa kuondoa usumbufu uliokuwa unawakuta wachimbaji wadogo; tumeondoa urasimu uliokuwa unasababisha sekta hii haikui; tumefanikiwa kuimarisha na kuongeza masoko ambayo sasa siyo tena jambo la ajabu kusikia kwamba kuna soko kila kona ya nchi hii. Sasa Serikali ina jambo moja tu la kufanya katika eneo hili. Ni kufanya sera yake ya kodi kwenye eneo la wachimbaji wadogo iweze kutabirika na iweze kueleweka. Naishukuru sana Serikali, wanafanya utafiti na utafiti huu utawapeleka kwenye kuamua aina gani ya kodi wafanye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema hapa kwamba, fedha tunazoziona kwenye mauzo ya dhahabu ya mchimbaji, siyo faida. Mchimbaji mpaka anafikia kwenda sokoni kuuza dhahabu, investment yake aliyoiweka wakati mwingine ni asilimia 200 ya anachoenda kukiuza. Kwa hiyo, ni vizuri sana tuwe na sera zinazotabirika na zinazoeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ili uweze kufikia malengo sasa unayokwenda zaidi ya Shilingi trilioni moja point; aliwahi kuzungumza Mheshimiwa Kishimba, hakuna Chuo cha Wizi, Serikali inafundisha tu namna ya kumdhibiti mwizi, lakini kuna watu wanajifunza namna ya kuiba. Mikakati yote ambayo mnafanya, lazima pia mjue kuna watu wanajifunza namna ya kuiibia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unafahamu, kuna watu wanafanya mkakati wa ku-lower purity ya dhahabu, lakini kuna watu wanafanya smuggling na hii smuggling inatuathiri sisi wenye Halmashauri tunazotegemea kupata Service Levy kutoka kwenye mauzo ya dhahabu. Sasa lazima Serikali nzima ifanye kazi kwa pamoja; vyombo vyote, ili tuweze kufikia malengo haya ambayo mimi nayaona tunaenda kufikia, kwa sababu, tayari tumeanza kukaribisha wawekezaji wengine katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka kulichangia, nataka kuishukuru sana Serikali. Tumekuwa na mgogoro wa muda mrefu Geita wa vigingi pamoja na mipasuko. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Shigela. Baada ya kufika Mheshimiwa Shigela amekuja na formula tofauti na Wakuu wa Mikoa wengine. Kwanza ameshirikisha makundi yote kwa kukaanayo, akawashirikisha wawekezaji, baadaye akaunda kamati ambayo imefanya kazi yake. Sina uhakika na taarifa ya Kamati, lakini nina imani kubwa, Kamati ile kwa mchanganyiko wake na muundo wake, itakuwa inakwenda kuleta suluhu ya wananchi wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu Mheshimiwa Waziri, jambo hili lifike mwisho. Wananchi walikusikia tarehe 09 Januari, ulitoa miezi mitatu, miezi mitatu imekwisha. Wengi wanaomba namba yako wakupigie ili waweze kujua limefikia wapi, lakini siwezi kuwapa namba, nina imani kwamba utakwenda kusema sasa jambo hili linaishaje. Nani analipwa fidia, nani halipwi fidia na kazi zinaendelea kwa staili gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa sababu umeonesha dalili ya kwamba unataka lifike mwisho. Ninawaahidi wananchi wa Geita kwamba Serikali yao inawapenda na kuwasikiliza, na mwakilishi wao ambaye wamenituma hapa sasa wawe na uhakika kwamba nakwenda kulimaliza suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu; tulifanya mabadiliko ya sheria hapa kuhusu local content. Naomba kuipongeza Serikali; imefanikiwa sana kwenye utekelezaji wa local content. Ni miongoni mwa halmashauri ambazo mtu akitaka kujifunza namna ambavyo local content inasaidia kukuza uchumi wa wananchi aje ajifunze Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana GGM, ninawapongeza katika maeneo yote. Kwenye michezo nadhani mnafahamu habari ya Geita Gold. Tunayo timu nzuri, tumepandisha timu nyingine ya wanawake, Geita Gold Queens, ambayo na yenyewe tunawashukuru sana Geita Gold kwa sababu bila mchango wao hatuwezi kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru Geita Gold kwa sababu local content imesaidia sasa wananchi wa Geita wanaweza kushiriki kwenye uchumi mkubwa ambao ni uchumi wa madini. Sasa…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kanyasu.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, dakika moja.
MWENYEKITI: Malizia.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu; Twiga Mining pamoja na Geita Gold na mashirika mengine, kwa mfano Twiga Mining wameweka middleman pale katikati ili uweze kufanya biashara na mgodi, inawaongezea gharama wafanyabiashara. Tunashukuru kwa nafasi hiyo lakini tunaomba tupunguze huo urasimu ili kusaidia wananchi wengi kushiriki kwenye uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)