Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Madini; lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii tena ya kuweza kutupa nafasi ya kuchangia Bungeni leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kufanya kazi kubwa ya kuilea Wizara hii, na sasa tunaona maendeleo na ukuaji wa sekta unaendelea kuwa mkubwa. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa yeye, Naibu Waziri na wataalam kwa kusimamia sekta hii kiasi kwamba inaonekana ukuaji wake ni mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana kwenye kumbukumbu kwamba mwaka 2020 ukuaji wake ulikuwa ni asilimia 6.7 lakini sasa mwaka 2021 inaonekana imekuwa inakwenda kwenye asilimia 9.6, maana yake kuna ukuaji, kuna positive gain hapo, kuna positive growth; kwa hiyo tunaamini kwamba kuna kazi kubwa wanayoifanya viongozi wetu hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye mchango wa Pato la Taifa, napo nilikuwa najaribu kuangalia, inaonekana wamelinganisha vipindi ile first quarter ya mwaka ambayo ndiyo naona imekuja kwenye vitabu vyetu. Kwamba ukienda kwenye mwaka 2020 utaiona 6.7, 2021 utaiona 7.2 na mwaka 2022, kwa kipindi hiki utaiona ni 9.7. Sasa, hapa nilikuwa nataka kushauri, kwamba ikiwezekana wakati mwingine wanapokuja na taarifa hizi, kwa sababu leo tuko kwenye quarter ya tatu tunakaribia ya nne sasa basi tupate data za quarter ya pili ili data za quarter ya kwanza ambazo zinakuwa mpaka 9.7 zinaweza zikawa zimepitwa kidogo na wakati. Tungepata za quarter ya pili zingetuonesha uhalisia wa nini kunaendelea hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati napitia ripoti hii nikilinganisha ninaona kwenye bajeti ambayo walipata mwaka jana takribani bilioni 83.4 na mwaka huu wamepata 89.3. Sasa nikiangalia kwenye maendeleo, mwaka jana tulikuwa na asilimia 26.4, mwaka huu tuna asilimia 25.9 maana yake maendeleo pesa yake inazidi kupungua kwa maana ya pesa nzima inayotolewa lakini bado sekta hii inatakiwa ikue. Kwa hiyo nilitegemea kwa sababu sekta hii inatakiwa ikue basi pesa ya maendeleo mwaka jana ya iwe kidogo ya mwaka huu iwe nyingi. Mwaka huu inaonekana kama ni nyingi kidogo lakini percent yao kwa maana ya pesa ya jumla ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe tu hapo, kwa sababu ndipo mahali ambapo sisi tunaotoka kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo; nishukuru nimepata taarifa leo kwamba asilimia 80 ya madini yanayochangia kwenye Pato hili la Taifa ni dhahabu na mimi natoka sehemu wanayochimba dhahabu. Kwa hiyo nilitegemea kabisa hii pesa ya maendeleo inapoongezeka ndipo fedha ya STAMICO ilipo, ndipo fedha ya GST ilipo wanaoweza kufanya utafiti na kutupatia kanzi data ya madini yako wapi na watu wetu wakachimbe kwa urahisi. Huku ndiko fedha ya STAMICO Ilipo, mahali ambapo wanaweza kununua vifaa vya kwenda kuwasaidia wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lakini niseme tu kama changamoto, hata mwaka jana niliona STAMICO wamepata mitambo ambayo inasaidia wachimbaji wadogo lakini nikifanya sensa jimboni kwangu wanakochimba sana ni wapi sasa ambako STAMICO wameanza ku-support kwa mitambo ile wachimbaji wadogo, sipaoni. Kwa hiyo niwaombe sana Wizara, inawezekana tukawa na mitambo lakini kwenye utekelezaji, kwenye implementation plan kukawa kuna tatizo. Tumeona kuna mitambo ya bilioni nne lakini bado kwa wananchi hatujaona ile impact kubwa. Kwa hiyo niwaombe sana watu wa STAMICO waende na data za kutuonesha ni wapi wamewasaidia wachimbaji wadogo ili tuweze kupata mchango mkubwa wa pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu cha pili ambacho nilitaka nikiseme hapa ni kile ambacho ndugu yangu Kigua alikisema hapa, kuhusu leseni. Mwaka huu tumeshatoa leseni 6,381 na malengo yalikuwa elfu sita mia moja kama sitini na kitu hivi, maana yake tumezidisha lile lengo, maana yake kazi inayofanyika ya kukata leseni ni nzuri sana. Changamoto niliyonayo kama aliyosema mwenzangu asubuhi, hapa kwenye Sheria ya Mineral Right na Sheria ya Surface Right kuna changamoto kubwa. Tunaonekana kabisa mchango kwa Pato la Taifa ni mkubwa na fedha ya madini ni nyingi lakini kiuhalisia wananchi wakaida wanaotoka vijijini wanazidi kuwa maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanazidi kuwa maskini kwa sababu gani? hawa wenye leseni wengi wanaotajwa hapa ni wale wanaoenda kuingia kwenye mfumo huu wa sasa wa kidigitali. Mwananchi wa kawaida kwa elimu ya kawaida huo mfumo hawaujui, na ndugu zangu wanaoshughulikia mtandao hata 3G kule kijijini haipo anawezaje ku access portal ile ilhali 3G haipo? Kwa hiyo kimsingi wanaoweza ku-access ni watu wa mjini. Kwa hiyo leseni zote hizi zitakuwa ni za watu, wajanja wa mjini, na wale wananchi wetu kule chini wakiwa hawana leseni yoyote inayoweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kwenye eneo hili, watu wetu wa ardhi na watu wetu wa madini fanyeni hii surface right na mineral right isomane, ikisomana maana yake tutapunguza haya malalamiko. Mimi mara nyingi huwa nina mifano ya wazi; nimebahatika kutembelea maeneo yanaitwa Kaseme, kata ya Kaseme pale kwetu. Moja ya hoja ambayo waliyokuwa wanazungumzia ni hii. Mtu jioni ameona vimacho macho vya dhahabu eneo lile, asubuhi akiamka anaambiwa kuna mtu alishaingia kwenye mfumo amekatiwa leseni tayari kwa hiyo eneo lile ni la kwake chini kule. Sasa yeye anabaki kuanza kubabaika anaambiwa analipwa shilingi ngapi hajui kwa sababu sheria hizi hazijulikani na elimu hatujatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu wa madini, hebu tujikite kutoa elimu kwanza kwa wananchi na tuwafundishe hii portal tunaingiaje. Kwa sababu leo hii nikimpigia mtu yeyote kijijini nikamwambia unaifahamu hiyo portal ya madini wanayoingia anasema hiki ni kitu fulani cha ajabu tu, hakijui. Hebu tuwape elimu hao watu ili kusudi na wao waweze kufaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo wamekaa miaka 20, kesho wanaambiwa mineral right kuna mtu anachimba anamwambia nitakulipa shilingi laki moja moja kila hekari yako moja, ana hekari 29 maana yake analipwa milioni mbili, huyo anayechimba anapata ela ya kutosha lakini huyu mtu anabaki kuwa maskini. Kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu wa madini tutoe elimu kwa wananchi wale wa kawaida ili kusudi wajue nini wafanye kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaweza kupata maendeleo kwenye mdini hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa malengo ambayo umeweka hapa, vipaumbele vyako. Umesema wazi kabisa kwamba unaenda kuwaendeleza wachimbaji wadogo. Nikushukuru vile vile nimeona unakwenda kujenga Jengo la Afisa Madini wa Mkoa wa geita kwa fedha nyingine inayobaki Wizarani. Nikuombe sana, wakati unalijenga hili vile vile tuhakikishe kwamba tunajenga uwezo wa wananchi wetu kuendelea kuchangia kwenye eneo hili. Tukifanya vizuri kwenye eneo hili la madini nina uhakika kuwa mchango wa Taifa badala ya kuwa asilimia kumi utakuwa asilimia 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.