Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kunijalia na kutujalia sisi sote tukiweo hapa afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamo wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri wa Madini na Watendaji wa Wizara ya Madini. Mheshimiwa Rais tarehe 17 aliweka Saini mkataba mkubwa wa dola milioni 667. Mkataba huu unakwenda kuleta uchumi mkubwa katika Mikoa ya Lindi, Songwe na Mkoa wa Morogoro. Mikoa hii kwa muda mrefu ilikuwa inasemekana kwamba ina madini ya kutosha lakini ilikuwa bado kigugumizi. Sasa, kitendo cha Mheshimiwa Rais kufungua na kuingia katika mikataba rasmi kwa kweli tunaona kabisa Lindi kuchele. Naona Ruangwa kuna dhahabu, graphite na madini madogo madogo. Tunaona Liwale kuna dhahabu lakini ndani ya Selous kuna wachimbaji, ambayo tunaona wanachimba kiholela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kuwa Serikali itakuwa macho, wale waliopewa vitalu kule ndani wasitufanye shamba la bibi, tunataka tuhakikishe yanayopatikana ndani ya Selous au yale madini kama kuna wachimbaji wanajificha ficha, hasa watu wenye sura pana; nilipata nafasi mimi ya kuzungukia na nilipewa muda na watu wangu wa Habari Conservation, wa kutembelea maeneo ya corridor ya Wanyama tukakuta maeneo watu wanachimba, lakini financer wakubwa ni sura pana. Sitaki kutaja majina watasema Riziki umetaja mananii ya watu lakini tafuteni ni na sura pana wanajulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 nikiwa Kamati ya PIC nilikuja na recommendation kuwa STAMICO ifutwe kabisa imeingia katika hasara ya nchi, lakini hawa STAMICO walikuwa wameingia katika hasara ya nchi kwa ajili ya mikataba ambayo wao haikuwahusu. Ilikuwa ni mikataba midogo ambayo imeifanya STAMICO wawe paralyzed; lakini leo nataka nitoe ushahuda wangu mwenyewe STAMICO inakwenda juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 STAMICO imeweza kupeleka gawio la Serikali bilioni 2.5, na mwaka huu tunategemea kupata bilioni tano kwa taasisi ambayo ilishakufa haikuwa na mishahara na haikuwa na uwezo wowote. Lakini, kwa kupitia Mkurugenzi Mkuu, kwa uwezo aliokuwa nao wakishirikiana na watendaji wa STAMICO sasa STAMICO ni taasisi moja wapo inayoongoza, na inafanya kazi kubwa ya kuleta Tato la Taifa. Hongera sana Mkurugenzi Mkuu Venant Mwase, endelea kufanya kazi, Watanzania tuna matumaini makubwa na wewe. Sasa hivi nenda Lindi kahakikishe kila kanda wanafanya competition ya kujua yako wapi madini ili watu wa pale waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kamati ya LAAC mwaka 2007 nikatembelea Geita. Ilikuwa kwamba katika mikoa sita maskini na Geita mojawapo, leo nimeenda Geita nakuta mpaka traffic lights ziko barabarani. Nimetoka Geita, Katoro mpaka Bwanga watu wa kule sasa hivi unaona kabisa maisha yao mazuri. Niwapongeze Rais wa Madini Mr. Bina hongera sana kwa kazi kubwa unayoifanya kuwasimamia wachimbaji wadogo wadogo, ambao nao sasa wananufaika. Nimpongeze mwanamke shujaa Semeni John, huyu ni mwenyekiti wa wanawake wa wachimbaji wadogo wadogo. Tulikuwa kwenye mkutano mkubwa sana wa wachimbaji wadogo wadogo, kwakweli ule mkutano umetufanya tufarijike sana. Wanawake, vijana na wenye ulemavu ndio wanaoingiza forty percent ya uchumi mkubwa wa dhahabu; lakini hawana vitendea kazi, hawana mitaji; ni kundi ambalo linachimba katika mazingira magumu. Huko ndiko Serikali inapaswa ipambane na isimamie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri tulikuwa naye anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha tasnia hii inakwenda vizuri. Hongera sana Doto Biteko, mtoto msikivu, mwenye heshima, Mwenyezi Mungu azidi kukubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninazungumzia sekta ya chumvi. Mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Pwani yote mpaka Tanga ni mikoa ambayo ilikuwa kando kando ya Bahari inashughulika zao la chumvi; hili zao lilikufa kabisa. Leo STAMICO wameamua kulifufua hili zao la chumvi kwa kutengeneza data ya kuhakikisha kwamba wanawajua wachimbaji wote wanafanya kazi gani ili kuweza kuingia katika soko la Afrika na SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chumvi inahitajika Rwanda, Malawi, Zambia mpaka Congo pamoja na Uganda. Kwa kweli akisimamia hili eneo na wananchi hawa wakanufaika na uchimbaji wao wa chumvi kwa kweli suala la umaskini Mikoa hii ya Kanda ya Pwani itakuwa imepungua; nimpongeze sana kwa kazi anayofanya. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, anafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuja katika wachimbaji wadogo wadogo walemavu. Mimi ni shuhuda nilikwenda Mbogwe nikishirikiana na madini kwenda kugawa vifaa na mitambo kwa walemavu viziwi, wenye usikivu hafifu. Kumbe walemavu hawa mkiwatengea mazingira mazuri wanaweza kuleta uchumi mkubwa sana. Ningeomba baadhi ya Wizara zingine ziige mifano hii. Vile vile ningetamani mifumo iongee. Katika Wizara ya Wanawake tujue kuna wanawake wangapi wanachimba madini, hiyo naipa kazi Wizara; waje hapa watuambie wanawake hawa wanachimba madini. Lakini vile vile Wizara ya kazi wajue vijana wangapi wanafanya kazi ya kuchimba madini ili mafunzo yazidi kuendelea. Ninashukuru Waziri wa Fedha tayari ametoa bilioni tatu kwa ajili ya mafunzo kwa vijana. Hizi zikitumika kuwasomesha na kuwapa mafunzo maalum ninaimani baada ya miaka tunazungumzia utajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ushauri wangu? Tuna kanda ya kati ina madini, kanda ya kusini ina madini, kanda ya kaskazini tumeona Mererani kote kuna madini angalau kule kumeshapewa mwelekeo mkubwa. Matumaini yangu kwa sasa hivi Serikali iangalie, mikoa hii ambayo ina madini kwa wingi haya madini yote yanakwenda panya road, na katika kwenda panya road hatuoni manufaa ndio maana kama sasa hivi unaona only forty percent inakwenda kwa wachimbaji ambao wanaonekana wadogo wadogo. Ina maana madini mengi yanayotoka hapa yanaingia katika panya road yanaingia katika utoroshaji kwenda nje. Sisi wenyewe tukiwa tunategemea kuwa na matumaini makubwa sasa hivi tupambane nyumbani kwanza, mzalendo kwanza, Mtanzania kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wengine wanakuja misamaha ya kodi, misamaha ya mafuta yote wapewe, misamaha ya mitambo, inakuwaje wanashindana na watu ambao wanatumia vingondoli na majembe wakawa wanafika forty percent? Hawa wachimbaji wadogowadogo wakiongozwa na akina John Bina, kina Semeni ninaamini kuwa watu hawa watatoka vizuri na wataweza kufanikiwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali, na nishukuru sana Serikali, Mheshimiwa Rais katika mradi huu ambao umekwenda Mikoa hiyo, hasa mimi Lindi, nasema ninamuunga mkono kwa asilimia mia moja. Ninakwenda Lindi kusimamia wachimbaji wadogo wadogo. Wanawake na vijana sasa hivi ni muda mwafaka wa kuwaingizia uchumi. Hii tunayopata sasa hivi mwakani tutegemee kupata maradufu. Mheshimiwa Waziri nipe nguvu, niko tayari kama balozi wako kusimamia hili na wala sitakuangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti,baada ya kusema hapa ninawashukuru sana na ahsanteni sana; Mungu Ibariki Tanzania.