Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 Bunge hili lilitunga Sheria inayoitwa Natural Wealth and Resources Permanent Sovereignty Act, 2017, ambayo ni Sheria inayoeleza umiliki wa milele wa rasilimali na maliasili za nchi yetu. Na lengo la Sheria hii ilikuwa ni kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanatamkwa kwenye Sheria kwamba ndio wamiliki wa rasilimali za Taifa hili na maliasili zote. Niwapongeze sana Wabunge waliokuwepo wakati huo kwa wakishiriki kutunga Sheria hii. Kwa sababu ukweli ni kwamba Watanzania na wanachi wote, sisi ni miongoni mwao ndio, wamiliki wa milele wa rasilimali zetu. Lakini haitoshi kusema kwenye Sheria kwamba Watanzania ndio wamiliki wa milele wa rasilimali na maliasili ya nchi yetu tukaishia hapo bila kuonesha kwa vitendo athari ya kimaendeleo inayotokana na umiliki wao wa milele wa rasilimali za nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na utangulizi wa Sheria hiyo ambayo imetungwa na chombo hiki kitukufu ambacho hata leo hii mimi nimesimama hapa naongea kwacho kwa sababu tukumbuke na tuone umuhimu wa chombo hiki kwenye Taifa hili. Kwa sababu kwenye chombo hiki kuna wawakilishi wa nchi nzima, Wabunge, Wawakilishi wa Majimbo yote Tanzania nzima wako kwenye chombo hiki. Maana yake uwakilishi wa Tanzania nzima wa hao wamiliki wa rasilimali za nchi yetu upo katika chombo hiki. Kwa hiyo, tunategemea pia kuona kwa namna kubwa wanaotajwa kama wamiliki wa milele wananufaika pia na rasilimali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuzungumza kuhusiana na Sekta ya Uziduaji (Extractive Industry) na namna ambavyo sisi wa kizazi cha leo tunatamani wasifanye makosa waliyofanya watangulizi wetu kwa kuacha mashimo ya dhahabu na almasi, wakati ukitoka tu kwenye mgodi nje kuna watoto wana shule wanakaa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa natambua jitihada ambazo zimefanyika mpaka leo kuna CSR, kuna miradi ambayo imetokana na uwekezaji ambao umefanywa kwenye Sekta ya Uziduaji. Hata hivyo bado, kama vijana na Watanzania ambao tunasema ndio wamiliki wa milele wa rasilimali zetu, tunatamani tushiriki katika value chain ya migodi, value chain ya madini yetu ambayo tunayo kwa sababu haitoshi kuitwa wamiliki wa milele, ni lazima tuoneshe na tuonekane kwa vitendo tumetajirika sisi binafsi kutokana na rasilimali tulizonazo kwenye ardhi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015, Bunge hili lilitunga Sheria ya Uziduaji ambayo iliitwa Extractive Industry Transparent and Accountability na leo nitajikita hapo tu, uwazi na uwajibikaji kwenye mikataba ya Sekta ya Madini. Kwa wivu mkubwa sana, mimi kama mwakilishi wa chombo hiki kitukufu, nasikia wivu sana kama nitakuwa sijui nini kinaendelea katika makubaliano kati ya nchi yetu na mataifa mengine na kampuni nyingine za uziduaji kama haitajadiliwa kwenye Bunge hili kwa sababu tutajua vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wanaoshiriki kuingia mikataba hii ni binadamu, ndio maana tunahitaji vichwa hivi kutoka Tanzania nzima vishiriki katika kujua mikataba hii line to line ili tushauri kwa sababu hakuna mtu ana bifu na hii nchi, tunaipenda na tunataka rasilimali zetu ziwanufaishe Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Aprili nchi yetu imeingia makubaliano, wasiwasi wangu mkubwa sana athari ya Mikataba ya kutoletwa Bungeni imeanza kuonekana juzi. Waheshimiwa Wabunge wakiingia kwenye tablet zao website ya Kampuni inayoitwa peak layer earth limited utaona mkataba wa Nguala - Songwe umesainiwa juzi hata mwezi haujapita. Kwenye Mkataba wale wa kampuni wanasema project ina-expect kutumia Shilingi Dola Milioni 320, lakini kwenye website ya Wizara inasema project inategemea kutumia shilingi Dola Milioni 439 difference ni Dola Milioni 119.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niamini ni errors, ni kukosea kwenye kuandika, lakini siamini kama nikukosea kwenye kuandika kwa tofauti kubwa kabisa ya fedha hizi ambazo ni sawa na zaidi Shilingi za Kitanzania Bilioni 276.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nisingezungumza hapa kama mkataba na mikataba ya design hii ikaletwa Bungeni tukajadili. Hakuna mtu ana bifu na mtu yeyote, hakuna mtu ana wasiwasi na chochote katika nchi hii, bali tunataka tujue kwa sababu ya sheria ambazo zimetungwa na Bunge hili kwamba kila Mtanzania ni mmiliki wa milele wa rasilimali za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa sababu tuna mashimo ya gold, tanzanite na madini mengine tumeyaacha kule. Sasa hivi tunazungumza critical Minerals, layer earth element ni miongoni mwa critical minerals, ni kitu ambacho ni kipya na na tunakichukulia kama kipya, tunafikiri tunaweza kufanya kama tulivyofanya zamani. Sioni kama ni busara, kama ni sahihi kufanya kama tulivyofanya zamani. Natamani tuwe na jicho jipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi hata Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabau za Serikali hana mikono kwenye kukagua mikataba ya madini inayoingiwa katika nchi yetu. CAG aliondolewa mamlaka kisheria ya kupitia hii mikataba na kuikagua. The only provision ambayo CAG anapewa ni ambayo ataombwa na TEITI kwenda kukagua mikataba hii tena ikitokea kuna hitilafu kwenye hesabu, si chini ya one percent kwenye hesabu ndogo ndogo ambayo ataomba na TEITI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, kwanza, Ripoti za TEITI zote, kwa sababu CAG hana mamlaka kwenye ukaguzi wa mikataba, basi kwa sababu tumempa TEITI, basi wakati tunajadili ripoti za CAG, tujadili na ripoti za TEITI kwenye Bunge hili, ili sasa tupitie huko kwenda kuuliza nini kinaendelea kwenye mikataba yetu, kujua in details what is going on kwenye Sekta ya Uziduaji kwenye Taifa letu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria ilitungwa na Bunge hili na sisi ni wajibu wetu kuitekeleza sheria. kwa hiyo, naomba sasa Sheria ya Extractive Industry Transparent and Accountability itekelezwe. Tuletewe mikataba iliyoingiwa na Serikali ili Bunge hili kwa heshima yake lijadili kinaga ubaga na lijue mikataba ambayo Serikali yetu imeingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, CAG aruhusiwe kwenda kukagua mikataba kwa sababu sisi kama Bunge, CAG ndiyo jicho letu na ndiye tunamtegemea .

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, kwa sababu sisi tumesema tunataka tutekeleze Sheria ya Watanzania ku-enjoy rasilimali zao, basi waziduaji na wachimbaji wadogo wa madini ni sehemu ya Watanzania ambao tunatamani washiriki na wao kiasi kusherehekea rasilimali ambazo tunazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi sasa ninavyozungumza kuna mambo mawili. Kwanza, Serikali ilionesha nia ya kutaka kuwasaidia wachimbaji wadogo na kuna vitu wamewafanyia, lakini kuna VAT kubwa sana katika suala la umeme. Hii ni kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Madini watu wake wa migodi uunganishaji wao utasababisha watu wa madini waongeze kuchangia pato la Taifa, kwa sababu wanalipa kodi. Hata hivyo, kwa sababu wanarundikiwa madeni makubwa, wameunganishwa na umeme lakini wanatozwa VAT kiasi kubwa, kuna malimbikizo makubwa, wanashindwa kuendesha migodi, matokeo yake Serikali haipati pato na wachimbaji wadogo wanashindwa kupata pato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sasa Mheshimiwa Waziri atafute namna bora ya kuona namna gani anaweza kuwasaidia wachimbaji wadogo. Vile vile, hao hao wachimbaji wadogo kwenye upande mwingine kuna tax exemption walipewa kwenye vifaa vya kuwasaidia kuchimba madini, lakini wanaopewa tax exemption wanarudi wanakatwa tena na Serikali wakati wa kutoa vile vifaa bandarini. Kwa hiyo, sidhani ile nia bora ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, kama tutakuwa tunaitekeleza kwa vitendo kama tunawapa kwa mkono huu na tunachukua na mkono huu. Nchi hii ni ya kwetu wote na lengo letu wote tu-enjoy rasilimali za Taifa kwa pamoja na tuweze kunufaisha nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)