Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote, naomba nitoe pongezi nyingi sana kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hasa katika usimamizi wa Sekta hii ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutoa pongezi nyingi sana kwa Waziri wa Madini, ndugu yangu Mheshimiwa Dotto Biteko pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Stephen Kiruswa kwa kazi kubwa wanayoifanya. Vile vile, niendelee kutoa pongezi kwa Katibu Mkuu wa Wizara hii ndugu yangu Kheri, wanafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Wakuu wa Taasisi zote ambazo zinasimamiwa na Wizara hii ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba hazidanganyi, tumeona jinsi gani Sekta ya Madini inavyozidi kupaa kwa kuongeza pato la Taifa kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 mpaka sasa hivi tunaongelea asilimia 9.7. Hii ni hatua kubwa sana, inastahili pongezi na kwa kweli kazi kubwa sana imefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Madini tunaweza tukawa na madini yako chini ya ardhi na sisi Tanzania asilimia 90 ya madini tuliyonayo hatujayachimba. Pia madini yakiendelea kukaa chini maana yake ni kwamba uchumi wake hatutauona katika mchango wa pato la Taifa. Sasa nini kifanyike? Tunaona juhudi kubwa zinazofanyika, tuiombe leo Serikali, Wizara ya Fedha waangalie kwa jicho la kipekee hasa hizi Wizara ambazo zinazalisha fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Wizara ziko hapa nyingi tofauti, Mheshimiwa Rais anatengeneza Serikali yake kwa kuunda Wizara mbalimbali, lakini tunatambua kabisa kuna Wizara za matumizi na tunawapongeza Mawaziri humu kwa kufanya kazi kubwa ya kutumia. tunawagongea makofi, wamejenga zahanati, madarasa, barabara na wamejenga na vitu vingine. Wizara zao zinafanya kazi ya kutumia fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuangalie kipekee Wizara zinazokusanya fedha kwa ajili ya matumizi hayo na Wizara zinazokusanya fedha mojawapo ni hii Wizara ya Madini. Wizara zinazokusanya fedha ikiwemo hii Wizara ya Madini, ni lazima tuzipe fedha za kutosha ili zilete fedha zaidi. Haiwezekani tukapata fedha nyingi bila ku-invest fedha kwenye Wizara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wizara ya Madini wanaipatia Bilioni 22 kwa ajili ya Maendeleo, leo tunawapa Bilioni 23, halafu tunawapa lengo la kukusanya trilioni 1.006, ni lazima tutambue kwamba ni lazima tuingize fedha kwenye miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunawawezesha wachimbaji wadogo wadogo ili kusudi wachimbe kwa tija, wapate fedha wao wenyewe, lakini wapeleke pato kubwa kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wachimbaji wadogo ambao wanachangia asilimia 40, tuna wachimbaji wakubwa ambao wanachangia asilimia 60. Wachimbaji wakubwa ni wachacvhe lakini wanachangia kingi. Hawa leo na kesho mmoja au wawili waki-drop, itatokea shake kubwa kwenye mchango wa mapato, kwa sababu wanachangia kingi na wako wachache. Kwa hiyo, wawili au watatu kwa namna moja au nyingine ikitokea tatizo mmoja au wawili wakashindwa kuchimba, madhara yake ni makubwa kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wadogo wanaochangia asilimia 40, ndio walioingiza ajira asilimia 80 ya uchimbaji na ndio Watanzania wengi wako kule wanachimba. Pia hii asilimia 40 wawili, watatu, wanne wakishindwa, impact haitaonekana kwa sababu ni wengi wako wachache wadogo wadogo wanachangia kingi asilimia 40. Tukiwawezesha hawa tuna hakika ni ajira ya Watanzania na wakati huo huo ndio watakuwa wazalishaji wakubwa na kuingiza fedha katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Tuendelee kuwapa fedha GST na STAMICO ili wajikite katika uwekezaji wa kufanya utafiti, kwa sababu utafiti ndio njia pekee ya kuwafanya watu wachimbe kwa uhakika na kuleta pato la Taifa. Wachimbaji wadogo wakichimba kwa uhakika, pato la Taifa litaongezeka. Hivyo basi, tunaomba GST wawezeshwe, waendelee kuongezewa fedha kwa ajili ya mikakati ya kufanya tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya kitu kinaitwa resource estimation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji sasa hivi wanatoka nje ya nchi na wengine wanatambua kuna dhahabu hapa, lakini hawatambui dhahabu hiyo ipo kwa kiasi gani na wa-invest kwa kiasi gani ili waweze kupata kipato. Tukifanya resource estimation vizuri kupitia GST, itakuwa ni rahisi kupata wawekezaji na watakuja kwa masharti nafuu na watachimba kwa uhakika kwa sababu tayari utafiti umefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, GST leo wamekosa kibali cha kuajiri watafiti kwa maana ya watumishi wa GST. Naomba nishauri, kwenye Sekta ya Afya pamoja na Sekta ya Elimu tulitoa watu wa kujitolea volunteerism, watu wa kujitolea wameorodheshwa wakafanya kazi kwenye hizo Sekta za Afya na Elimu. Niwaombe hata GST ikiwezekana wako vijana wengi wana hizo taaluma za utafiti, Serikali itafute fedha, wajitolee, waingie kule wafanye kazi za kujitolea bila kuajiriwa. Hawa wafanye, ikitokea nafasi ya kuajiri wawaajiri hao. Waende wakafanye utafiti watawasaidia wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mengi ya kuongea. Kingine ni suala la ufungaji wa migodi. Ufungaji huu huwa unaanza wakati migodi inaanza. Mpango wa kufunga migodi pamoja na kulinda mazingira huwa ni mpango unaoanza wakati mgodi unaanza. Leo Mheshimiwa Waziri ametueleza hapa kuna baadhi ya migodi imezuiliwa kufunga kwa sababu hawajafuata tu taratibu. Niwaombe Wizara wawe karibu na wale wanaoanzisha migodi. Ile migodi mipya, wanapoanzisha migodi hapo hapo na plan ya kufunga iwepo. Leo ukienda Buzwagi kuna pit kubwa imeshindwa kufunikwa, ni kwa sababu inawezekana kabisa kulikuwa kuna utaratibu umekiukwa toka mwanzo wakati mgodi unaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Liganga na Mchuchuma. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, leseni ya Liganga na Mchuchuma mwenzangu Mheshimiwa Profesa Manya alikuwa anazungumza hapa akaishia njiani. Liganga na Mchuchuma leseni zimetoka mwaka 2016, tuna chuma kingi zaidi ya tani milioni 150, tuna makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 400 zipo zimekaa dormant, hazifanyi kazi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu ameshindwa kuchimba kuna Sheria ya Madini, kwa nini Waziri asifute hizi leseni? Kwa sababu kutokuchimba kwa madini ya Liganga na Mchuchuma pale yale madini ya makaa ya mawe pamoja na madini ya chuma anayekosa fedha ni Waziri haingizi kwenye wizara yake.

Kwa hiyo, mchango wa Shilingi Trilioni moja, nina hakika ni mdogo kama tutajikita vizuri katika mipango yetu tutapata fedha zaidi. Kesi ya NDC na wale wawekezaji sijui Wachina Waziri aache waendelee na kesi, yeye afute leseni, ampe STAMICO achimbe, watu waendelee kufanya kazi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nyongo.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)