Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii ili leo niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Madini.

Kwanza nianze kabisa kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kujadili hotuba ya bajeti ya leo. Vile vile, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitapeleka shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika nchi hii lakini hasa katika Sekta ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Mheshimiwa Rais, Mama yangu Samia Suluhu Hassan ametuheshimisha wachimbaji wadogo wadogo kwenye Nchi hii ya Tanzania. Historia inaonesha katika watu waliokuwa wakidharaurika katika nchi hii ilikuwa ni wachimbaji. Hata hivyo, leo hii unapozungumzia habari ya wachimbaji wadogo wadogo unaona kabisa ni watu wenye heshima zao, wanaweza kwenda wakakaa sehemu wakaonekana ni watu wenye heshima, wakawekeza, wanafanya mambo yao kisomi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Biteko anafanya kazi kubwa sana. Asubuhi hapa nimemsikia Mbunge mwenzangu akishauri Serikali waone kuwa na mpango wa kuweza kumpatia certificate, lakini nasema kama vyama vya wachimbaji vinanisikia huko viliko kwa maana ya FEMATA, TAWOMA na nimeona hapa chama kimoja cha wachimbaji vijana kiko hapa, wanafanya kazi kubwa kwa maana ya kusimamia wachimbaji vijana katika Sekta ya Madini. Kuna haja kubwa ya kumjengea sanamu Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko, ametufanyia kazi kubwa sana kwenye Wizara hii ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapozungumza mchimbaji mdogo mdogo aliyekuwa akichangia asilimia 20 na sasa asilimia 40, sio miujiza. Ni mipango mzuri, mikakati mizuri inayosimamiwa na Dkt. Dotto Biteko chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, nimpongeze hata Naibu wake Waziri na niwe wazi, katika Wizara ya Madini, Mheshimiwa Rais amefanya uchaguzi mzuri kabisa. Ukienda kwa Mheshimiwa Waziri ni msikivu na mnyenyekevu, ukienda kwa Naibu Waziri naye ni msikivu na mnyenyekevu, ukienda kwa Katibu Mkuu ndio usiseme meno 32 wakati wote sijui anachukia saa ngapi Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara hii. Ukienda kwa Mtendaji Mkuu wa Tume, yuko vizuri, Kamishina naye yuko vizuri. Hiyo inatufanya sisi wachimbaji wadogo wdogo kuwa na moyo wa kuwekeza na kuonesha kwamba Serikali kweli inatujali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana, leo hii tunazungumzia habari ya STAMICO. Utaona kabisa STAMICO hapo mwanzoni ilivyokuwa na sasa ilipo inafanya kazi nzuri sana. Wameanzisha miradi mbalimbali na leo hii wanazungumzia habari ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika kutunza mazingira.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kassim kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwita Waitara.

TAARIFA

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Kassim kwamba kwa wema wa Mheshimiwa Dkt. Biteko na mwenzake Mheshimiwa Kiruswa, leo ninapozungumza wananchi wa Nyamongo hawanywi maji ya sumu tena, wanakunywa maji safi ya bomba. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Biteko kwa kazi nzuri. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kassim taarifa unaipokea?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii mimi naipokea kwa mikono yote miwili, Dkt. Biteko anafanya kazi nzuri sana, hata siyo Nyamongo tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mwita Waitara ukija Kata ya Bulyanhulu na Mheshimiwa Amar yupo pale Nyang’wale utaona fedha nyingi ya CSR ambayo inatumika kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Msalala tunazungumzia tumemaliza zahanati 34 kwa mpigo, yote haya ni matunda ya Mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Dkt. Biteko.

Tunazungumzia habari ya vituo vya afya hapa juzi nilizungumzia habari ya lami tayari wako site wanaendelea kumalizia taratibu za kuanza ujenzi wa lami kilomita 76 kiasi cha Shilingi Dola Milioni 40 yote haya ni matunda mazuri ya Mheshimiwa Dkt. Biteko chini ya uangalizi wa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kipenzi cha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninataka kuzungumzia hapa, naomba nishauri tuna Vyama vya Wachimbaji hivi ambavyo kazi yao ni kusaidia wachimbaji, niombe sana STAMICO na Mheshimiwa Waziri niombe sana vyama hivi hebu oneni namna ya kuvisaidia viweze kuwasaidia kwa kazi nzuri mnayoifanya. Leo hii tunazungumzia habari ya uchimbaji kuna wachimbaji vijana wapo lakini ukiwaangalia kutafuta nani anawasaidia vijana hawa huoni na ndiyo maana umeona kuna taasisi imeanzishwa kwa ajili ya kuwasaidia vijana. Leo hii utaona kuna watu wanauza madila nani anawasaidia madila leo hii ukienda utaona kuna watu wana-plant nani anawasaidia plant? Vyama hivi ni lazima vikae chini vione namna ya kuunda reform, waunde umoja na umoja huu utasaidia katika kuhakikisha kwamba inaisaidia Wizara ili iweze kufanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie habari ya wachimbaji kwenye Jimbo langu la Msalala, amezungumza Mheshimiwa Nusrat Hanje nimuombe Mheshimiwa January Makamba na hili nitalizungumzia tunavyokuja kuzungumzia suala la umeme, changamoto kubwa ya umeme inakwamisha shughuli za madini katika maeneo yetu, hilo nitalizungumzia nitakapokuja kuchangia kwenye suala zima la REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Waziri wachimbaji wadogo wadogo hatuendelei kwa sababu ya kukosa mikopo. Leo katika hotuba yako nimeisikiliza vizuri, tumepongeza hapa mabenki yamefanya kazi kubwa ya kukopesha wachimbaji wadogowadogo, lakini nataka nikwambie inawezekana takwimu hizi za ukopeshaji haya mabenki wanakopesha wachimbaji wakubwa, lakini bado kwa wachimbaji wadogowadogo kupitia imani ambayo wewe mwenyewe umeijenga bado hawakopesheki, hakuna benki ambayo inakopesha mchimbaji mdogomdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri na niombe BOT, tumeona BOT imetoa fedha nyingi zaidi ya Bilioni kadhaa kuyapa mabenki ili mabenki haya yaweze kuwakopesha wachimbaji wadogowadogo, lakini unapoenda mchimbaji mdogomdogo kukopa fedha kwenye mabenki haya haukopesheki mpaka wanakuomba aidha ufungue biashara nyingine au uwe na dhamana nyingine, wakukopeshe fedha zile kupitia mgongo wa biashara nyingine na siyo madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kama wachimbaji wadogowadogo inapelekea wanakosa mitaji ya kuendeleza shughuli za uchimbaji leo hii utaona, akija hapa Mzungu na briefcase akapeleka plan kwenye mabenki haya anapewa mkopo lakini akienda ngozi nyeusi kwenda kuomba mkopo hapewi, mabenki haya yatueleze kama yana ushahidi yamempatia nani mchimbaji mdogomdogo watueleze waweke ushahidi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest, mimi ni mchimbaji ninachokisema hiki ninauhakika nacho, hakuna mchimbaji mdogomdogo ambaye kakopeshwa fedha na mabenki haya. Sasa kuna haja ya kukaa na mabenki haya niiombe BOT ikae na mabenki haya, kwanza ukiona BOT inawapa mikopo mabenki haya kwa asilimia ndogo sana, asilimia tisa na lengo la mikopo hii ni kutukopesha wachimbaji wadogowadogo lakini utaona wachimbaji wadogowadogo bado hawaaminiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na Mheshimiwa Waziri kufanya kazi kubwa ya kuwapatia leseni wachimbaji wadogowadogo lakini bado leseni zao hazitumiki kama kigezo cha wao kupatiwa mikopo, kwa hiyo niombe sana na niombe Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ananisikia waweke mkakati wa kuhakikisha kwamba wanakopesha wachimbaji wadogowadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hii hapo zamani wachimbaji tulikuwa tunakopeshwa walikuwa wanakopeshwa wote kwa maana ya mikopo na baadae Serikali iliondoa, sasa wewe mwenyewe umetueleza Mheshimiwa Waziri kwamba wachimbaji wa sasa ni wa kisasa, hebu nikuombe sasa kwa sababu tayari wachimbaji wa sasa wako kwenye reform, mikopo iliyokuwa ikikopeshwa iweze kurudi sasa ili iwasaidie wachimbaji kuelekeza kuchimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nyongo amezungumza hapa Habari ya GST. GST inaendelea kufanya vizuri, niombe waendelee kufanya kazi kubwa kuzunguka maeneo yetu, waweze kuandaa ripoti wafanye reserve estimate, wawapatie wachimbaji wadogowadogo na Wizara mkitupatia hiyo mikopo wachimbaji wadogowadogo maana yake ni kwamba itaenda kusaidia katika kuhakikisha kwamba sekta yako Mheshimiwa Waziri inakua kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia habari ya ufungaji migodi hapa Mbunge mwenzangu, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana pale Kahama tuna mgodi wa Buzwagi ambao umefungwa, plan iliyopo pale ni kwenda kufanya kuwa eneo la economic zone sikatai ni wazo zuri, lakini niendelee kuomba sana kwa sababu Kahama nzima inategemea uchumi wa madini na leseni ile kwa sababu hawa watu wanaenda kuiachia, na kwa kuwa wanaenda kuiachia bado ina madini ambayo wakipewa wachimbaji wadogowadogo wanaweza wakapata fedha kupitia maeneo yale. Ninaomba Mheshimiwa Waziri ikiwezekana ikikupendeza hebu gaweni ile leseni sasa kwa wachimbaji wadogowadogo pale Buzwagi ili iweze kukuza uchumi wa Kahama Mjini na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya GST na STAMICO, leo hii utaona GST katika maeneo haya wanazo maabara za upimaji madini katika Jiji la Dodoma na niwapongeze Mheshimiwa Waziri wameenda kufungua maabara nyingine Geita. Sasa maeneo mengine mengi Mheshimiwa Waziri kama Chunya, Kahama ambayo ndiyo maeneo ambayo yanazalisha dhahabu kwa wingi ninaomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kuanzisha maabara kubwa kwenye maeneo haya ili tuwarahisishie wachimbaji wadogowadogo wanapoweza kuchimba madini yao waende wakapime sampuli zao kwenye maabara za Serikali ambazo zitawapa uhakika, kwa sababu wachimbaji wengi wanafilisika sana kwa sababu ya vipimo vya maabara hizi zilizoko mitaani ambazo hazina uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana watu wa GST..

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kassim muda wako umeisha.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga hoja kwa asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)