Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kabla sijaenda kwenye hoja zangu, niungane na Waheshimiwa Wabunge ambao wanampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Dkt. Biteko, pamoja na Naibu Waziri, kwa kufanya kazi vizuri sana katika Wizara hii na kuijengea heshima kubwa sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu huohuo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ambaye amemuamini Waziri huyu katika sekta hii muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maeneo mawili ambayo ninatamani nichangie kidogo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza linahusu kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali za madini ambazo zimefanyika hapa nchini. Zipo tafiti nyingi sana zimefanyika na kubaini uwepo wa madini maeneo mbalimbali. Moja katika maeneo hayo ni Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mkoa wa Ruvuma. Imechukua takribani miaka zaidi ya 20 kuanza kutumia baadhi ya tafiti ambazo zilifanyika Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Halmashauri ya Madaba miaka 20 baadae baada ya kugundua uwepo wa madini aina ya makaa ya mawe ndipo tumeanza kutumia yale matokeo ya tafiti. Kimsingi tumechelewa sana, leo pengine Madaba tungekuwa mbali sana kiuchumi. Tumeanza kutumia matokeo yale leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri arudi kwenye makabati yake akaangalie matokeo ya tafiti za madini zinazohusu Madaba. Ndani ya Kijiji cha Ifinga katika Halmashauri ya Madaba kuna uwepo wa madini yenye thamani kubwa sana. Naomba kama itakupendeza Mheshimiwa Waziri, na ukiridhika, wasiliana na Dkt. Dalali Kafumu ambaye alishiriki kwenye utafiti huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni utafiti ambao utaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwenye Halmashauri ya Madaba na kwa Taifa katika ujumla wake. Nikuombe sana fanya jitihada za pekee. Binafsi naendelea kufuatilia lakini naomba unisaidie kwenye eneo hilo kwa sababu Wanamadaba wanasubiri kuanza kunufaika na uwepo wa madini hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba uridhie turejee kwenye mradi muhimu sana kwa maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe katika ujumla wake. Lakini manufaa haya hayaishii Njombe na Ruvuma pekee, manufaa ya mradi huu yanakwenda kugusa Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mingi sana, zaidi ya miaka 30, nenda kwenye Hansard za Bunge hili utakuta tunazungumza mradi wa Liganga na Mchuchuma. Tunaposema Liganga – naomba Watanzania waelewe na Waheshimiwa Wabunge tuelewe na tuunganishe nguvu – tunaposema Liganga hii ni deposit ya chuma, chuma inayoweza kujenga reli, inayoweza kuwa malighafi ya kutengeneza magari, inayoweza kuwa malighafi ya kutengeneza pikipiki na baiskeli, ambayo inaweza kuwa malighafi ya kutengenezea nondo na kujengea majengo ya aina yoyote, ambayo inaweza kuwa malighafi ya bati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea utajiri huu mkubwa ambao upo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa inayopakana na Madaba ndani ya Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea huu mradi wa Liganga na Mchuchuma, Mchuchuma tunazungumzia makaa ya mawe, Liganga tunazungumzia chuma. Makaa ya mawe ya Mchuchuma yana uwezo wa kuzalisha umeme megawati 600. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyosema megawati 600 Watanzania wanielewe, hii ni zaidi ya nusu ya umeme wote ambao Tanzania ilikuwa nao miaka mitano iliyopita. Kwa hiyo, siyo umeme mdogo, tusiuchukulie mradi huu kitoto kitoto, hebu tuupe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa maana ya multiplayer effect mradi huu mimi ningesema, mradi huu unafuatia kwa umuhimu ukiondoa mradi wa maji wa Bwawa la maji la Mwalimu Nyerere. Ukiondoa mradi wa maji wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere mradi unaofuata kwa multiplayer effect na kwa umuhimu wa Tanzania na kwa uchumi wake ni mradi wa liganga na mchuchuma. Mradi huu ulikuwa unaambatana na ujenzi wa reli ya kusini, reli ambayo ingeleta maendeleo makubwa sana kwa nchi hii. Lakini tunapozungumzia mradi huu tunazungumza pia barabara ya lami ya Mkiu-Madaba ambayo ingetumika kusafirisha malighafi ya chuma na makaa ya mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti,hii miradi yote hatujaipata kwa sababu hatujaamua kuchimba hii chuma. Tumewanyima wana-Ruvuma haki ya maendeleo, tumewanyima haki wana-Njombe kupata maendeleo. Tumewakatalia fursa za ajira watoto wa Madaba, Njombe, Peramiho na Songea Mjini kwa kukataa kujenga mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninamwamini sana Mheshimiwa Dotto, ni mtu wa viwango, amefanya mapinduzi makubwa sana kwenye sekta ya madini lakini anaacha lile jiwe la chuma likae pale kwa miaka mingapi? Nani atakuja kulichimba lile jiwe? Watanzania watasubiri ajira mpaka lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mutliplayer nyingi sana, sijasema kuhusu aakina mama, akina mama ntilie ambao wangepata ajira kwa kuuza chakula kwenye migodi ya chuma ile. Sijamwambia kuhusu idadi ya vijana ambao wangeajiriwa kwenye miradi ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya sita ilipoingia madarakani kulioneshwa dalili ya kwenda kuanza kuchimba lile jiwe. Na mimi niseme, Watanzani nchi nzima tujue tumekalia utajiri mkubwa sana pale Ludewa; na kama nchi hii haipigi hatua za kutosha ni kwa sababu hatujaamua kutumia malighafi ambazo tumepewa na Mwenyezi Mungu pale Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana uendelee kukazia Serikali na Mheshimiwa Doctor Dotto uko hapa naomba jitahidi kabla Awamu ya Sita hii haijamaliza kipindi chake cha uongozi tuwe tumeshachimba jiwe la chuma la liganga? Tuwe tumeshatoa ajira kwa wana-Ruvuma na Watanzania, tuwe tumeshazalisha malighafi kwa ajili ya baiskeli, magari na vifaa vingine vya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja.