Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukurukwa nafasi hii na mimi. Kwanza nitumie nafasi hii kwa kweli kuishukuru na kuipongeza Serikali na Rais wetu kwa kufanikisha kuwaondoa Watanzania kule Sudan katika uwanja wa vita; jambo hili limetujengea heshima. Hawakuondoa Watanzani tu lakini pia wameondoa raia wenzetu katika nchi nyingine za Kiafrika; na dunia yote ijue kwamba hisia ambayo iliasisiwa na mwalimu Nyerere ikaongoza ukombozi wa Bara la Afrika bado ni ile ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili na mimi nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Madini na timu yake kwa kazi nzuri ya kusimamia sera na sheria za madini. Nilikuwa naangalia ule mpango wa maendeleo, nadhani ni moja ya Wizara chache ambazo zinaelekea kukamilisha lengo la mpango wa maendeleo ambao tumesema sekta hii ichangie asilimia kumi; kwa jinsi ambavyo tunakwenda tunaweza kufikia hapo. Kwa hiyo tunashukuru na kuwapongeza kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niweke mchango wangu katika eneo moja tu. Ni suala la nafasi ya sekta ya madini kwenye kupambana na umaskini kwenye nchi hii. Hakuna shaka kitakwimu tunakwenda vizuri lakini ukweli ni kwamba sekta hii bado haijatusaidia kwenye kutuondoa kwenye umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nchi zote ambazo zimeendelea ni kwa sababu ya mambo mawili tu ama zina rasilimali watu au na asilimali asili na sisi tunayo rasilimali watu lakini tuna hii moja rasilimali asili muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano, mwezi uliopita, huu Februari kulikuwa na mkutano mkubwa sana pale Cape town South Africa, Engaba Mining Conference. Kwenye mkutano ule kwa mara ya kwanza Marekani ilipeleka ujumbe mkubwa sana; na ilimtuma mwakilishi wao maarufu Amos Horsen ambaye ni mwakilishi maalum kabisa wa Rais Joe Biden katika sekta ya madini, na hawakuficha. Malengo yao ni mawili, moja Marekani inataka kuona kwamba inatumia sekta ya madini kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi hapa duniani lakini pili imeweka wazi kwamba imeshangazwa na imeshtushwa na ukweli kwamba kwa sasa biashara kwenye sekta ya madini kwa kiasi kikubwa inatawaliwa na China, kwa hiyo wanataka kuwa-take over.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni kwamba kuna vita kubwa ya madini inakuja. Haya mataifa mawili yakishaamua kupambana kuna vita inakuja uko mbele. Wametaja madini kwa mfano Lithium, graphite, Nickel, Cobalt, wameyataja haya ndio madini wanayalenga. Jumla wameainisha aina hamsini za madini; maana yake ni nini, ni kwamba kuna haja ya kuangalia upya model yetu ya uendeshaji wa madini hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshapitia hatua tatu, kwanza tulianza na wakoloni, walipokuja wakoloni hapa Waingereza ule mradi wa Mwadui, wanafahamu watu wa madini, walikuwa wanamiliki De Beers ailimia 50, Serikali ya Uingereza asilimia 50. Sisi tulipokuja kwenye Azimio la Arusha tukatangaza kwamba madini yote katika nchi hii yatakuwa chini ya Serikali, ndipo tukaunda STAMICO. Haikufanya vizuri sana na sababu zinajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 1990 tukahama tukaenda kwenye ubinafsishaji, na tukasema kazi ya Serikali ni kukusanya kodi na kuweka mazingira ya kuvutia wawekezaji basi, uchimbaji na kadhalika waende sekta binafsi. Hii ikatuletea matatizo, ndiyo ikatubakishia mashimo, hatujafaidika sana miaka 20 ya sera hiyo. Naiyo maana mwaka 2015 na 2017 tumekuja na Sheria hizo mbili, tumezitekeleza, tumebadilisha na tumefaidika kwa kiasi. Hata hivyo, kwakweli ambacho kimebadilika kikubwa tumebadilisha sana numbers lakini bado suala la umiliki liko mikononi mwa wawekezaji na wawekezaji wa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mapendekezo yangu ni kwamba ile sera ambayo tulikuwa nayo mwanzoni, hapa tulipofika Serikali na sisi kama Bunge tukubaliane kuchagua baadhi ya madini ambayo piga ua asilimia mia moja yatakuwa chini ya Serikali. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri mwenyewe kwenye hotuba yake ameshaainisha madini haya yapo vanadium, Nickel, Graphite, yametajwa pale, vizuri kabisa; na hii ambayo ameongea Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria hapo ya mambo ya Liganga na Mchuchuma, tuwekeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia uwekezaji, ukiangalia katika miaka, wenzetu wa Tume ya Madini wameanisha madini mengi pale lakini nimechagua saba. Thamani ya uwekezaji wa madini haya kwa miaka kumi mpaka ishirini ijayo ni bilioni 4.385 sawa na tirioni kumi. Mauzo yatakayotokana na uwekezaji huu ni dola za Kimarekani bilioni 63, hii ni GDP ya Tanzania kwa sasa almost, sawa na trilioni 145. Sisi tutapata nini? Tutapata dola bilioni 17 sawa na trilioni 39 asilimia 27, sijui kama unanielewa hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani uwekezaji wote huo tutaambulia asilimia 27 ambayo ni chini hata ya corporate tax; na hapa tumeshachukua royalty, inspection fee, corporate tax, kodi zote, tutaishia kupata tirioni 39; na haya ni madini ambayo ni muhimu sana. Zipo nickel na lithium humo. Kwa hiyo ninachotaka kupendekeza hapa ni kwamba, tubadilishe model ili baadhi ya madini yaende STAMICO, STAMICO imarishwe, ipewe mtaji, ipewe watu sahihi ili iwe hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na itakuwa siyo sisi peke yetu, wanafanya hivyo Botwana. Botswana yale madini yote ya dhahabu yapo chini ya Debswana Company Limited ambayo ni ya Serikali kwa asilimia mia moja. Botswana madini ya dhahabu hayachimbwi na private sector. Ukienda India wanayo NMBC, South Africa ambayo tunaiona hapo wakati wa Makaburu waliijenga tunayoiona ile kwa sababu ya dhahabu, na walikuwa wanamiliki Makaburu wenyewe. Kwa hiyo hii model ambayo tunayo tuchague baadhi ya madini tuwe na model tatu. Uwekezaji upo, ipo ya hamsini kwa hamsini lakini ya tatu asilimia mia moja yawe ya kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwisho ni suala la umakini kwa wataalam wetu katika ushauri tunaoutoa kwa Serikali. Hapa tunapoongea nchi yetu ipo kwenye disputes mbalimbali za kimataifa ambazo zinatokana na uwekezaji. Nilikuwa napitia website ya dispute and judgement navigator, tuna kesi takriban saba, tatu za madini. Kampuni ya Montero, Nachingwea, Wisher tumeshitakiwa kule na watu wamepeleka madini; lakini ukiangalia sababu ni kwamba watalam wetu walitushauri wakaishauri Serikali hii, wakasema kwamba baada ya kubadilisha Mining Act ya 2017, wakabadilisha zile regulation 2018, wakashauri kwamba leseni ambazo zilikuwepo zifutwe, zile provisional license, wakasema hakutakuwa na shida, lakini shida ipo. Sasa wasomi wetu walete ushauri wa kisomi sio ushauri wa kishujaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa sekondari kulikuwa na methali inasema kwa mwoga huenda kicheko na kwa shujaa huenda kilio. Wale wanafunzi tuliokuwa tukisoma nao wanajifanya hawataki kusoma, hawasomi kwa bidii, wanakwenda disco wanajifanya mashujaa; akitoka disco anakwenda kwenye mtihani. Wale ambao walikuwa wanasoma wanaambiwa wanoko wanafanya revision kwa umakini wanafaulu, wale wanaopata division four, division zero wanalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wa kishujaa ndio huo. Kwamba unamwambia kiongozi hakuna shida usiwe na wasiwasi, humwambii ukweli, tunaingia kwenye kesi hizi na sasa hivi Serikali inalipa fedha nyingi. Wasomi wetu watupe ushauri wa kisomi. Ushauri wa kisomi ukweli ni kwamba huwa ni mchungu; unamwambia kiongozi ushauri ni mchungu, lakini ushauri wa kishujaa unampa kiongozi anachokitaka ili afurahi akupendelee sasa ushauri huo ni ushauri ambao hautusaidii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya madini imejaa wataalam wazuri wanajulikana nchi hii; hebu watueleze ukweli ni nini, tusiingize nchi yetu kwenye matatizo makubwa. Si sahihi kabisa kutoa ushauri wa kishujaa ambao siku hizi ushauri wa kishujaa unaitwa ushauri wa kichawa, huo si mzuri na hautusaidii kama nchi. Kwa hiyo ni jambo ambalo niliona niliweke mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti,lakini mwisho, ameongea Mwenyekiti wa Sheria pale; hili la Liganga na Mchuchuma sipendi kuliongelea kwa sababu na mimi nilishapitia huko, wanafahamu Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Mwijage, ni heshima kubwa. Ule mradi investment cost yake ni bilioni tatu, kwa nini Serikali kupitia STAMICO, kutokana na umuhimu wa mradi huu; kwa nini tusiachane na mambo ya uwekezaji na tutafute fedha, tukope tuwekeze kwenye mradi huu? Kama Serikali imekubali kukopa mradi wa SGR, imekubali kukopa kwenye mradi wa bwawa ambao returns yake ni long term, mradi huu ukishakamilika tunaanza kupata fedha sasa, hii ni muhimu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa mradi huu utatupa investment ni three billion lakini kwa mwaka tutakuwa tunapata more than 1.4 billion dollars. Kwa hiyo maana yake ndani ya miaka kumi tumepata Dola za Marekani bilioni 14; sasa tatizo ni nini? Kwa hiyo naomba Mheshimiwa wa Madini na Waziri wa Viwanda ile failure ambayo sisi tuliowahi kuwa mawaziri kwenye sekta hii tumepitia naomba iwaepuke kabisa. Shaurini mamlaka, tuachane na uwekezaji kwenye sekta, hii Serikali ikope fedha tuwekeze wenyewe ili Watanzania waweze kufaidika na mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)