Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba nitumie fursa hii kwanza kabisa kushukuru kwa kupata fursa ya kuweza kuchangia Wizara yetu ya Madini. Mimi kwa sababu ya muda nitajielekeza kwenye mambo manne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kuhusiana na madini ya tanzanite kuweza kuuzwa kwenye masoko yote ya madini nchini. Hiki kimekuwa ni kilio chetu cha muda mrefu sana. Tunafahamu kwamba tarehe 7 mwezi Julai mwaka 2021 Serikali ilitoa tamko la kuelekeza kuwa madini ya Tanzanite yauzwe kwenye soko moja la Mererani peke yake. Lakini masoko haya ya madini ni masoko ambayo yapo kwa mujibu wa Sheria; na sisi watu wa Arusha tuna bahati moja kubwa sana. Wakati nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ndugu yangu na rafiki yangu Mheshimiwa Daktari Dotto Biteko alikuja pale Arusha akatuzindulia soko letu la madini, na soko hili limekuwa ni soko lenye mafanikio makubwa sana kwenye nchi hii ya Tanzania lakini cha kushangaza baadaye Serikali hiyo hiyo na chini ya Waziri huyo huyo ikaja na kanuni zilizobadilisha mfumo wa kufanya biashara ya madini hasa biashara ya madini ya tanzanite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya consultations nyingi na Mheshimiwa Waziri wa Madini kama sekta husika na wadau wote wa masuala ya madini. Kwa pamoja wameona changamoto ambazo zimetokana na matamko hayo ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kimsingi ningependa leo niwape taarifa ifuatayo; kwamba wakati ule Mheshimiwa Waziri alipokuja kuonesha soko la Madini mwaka 2019 kwa mwezi wa saba mpaka wa kumi na mbili 2019 tuliweza kupata madini ya tanzanite yaliyosanifiwa na kung’arishwa karat 76,303 na thamani yake ilikuwa ni bilioni 24. Kodi iliyopatikana Serikalini ilikuwa ni milioni 487. Lakini kwa madini hayo hayo ya tanzanite ambayo yalisanifiwa na kung’arishwa baada ya kuhamishiwa Mererani sasa mwaka 2021kuanzia Januari hadi Disemba tuliweza kuwa na karati 15,820 kutoka karati 76,000. Tuliweza kupata thamani yake ya shilingi bilioni mbili mia sita thelathini na sana kutoka bilioni ishirini na nne, mia tatu na sitini na moja; lakini pia na kodi au ada iliyolipwa ilikuwa milioni 52 kutoka milioni 487.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pia kwenye upande wa madini ya tanzanite ambayo ni ghafi yaliyo chini ya two grams, kwa upande wa soko la Arusha kwa July-December 2019 utakuta karat ambazo zilipatikana zilikuwa ni 7,920,000, thamani yake ilikuwa ni bilioni 12, kodi na ada zilikuwa ni milioni 848, na jumla ya thamani ilikuwa ni bilioni 36 na jumla ya kodi yote ilikuwa ni 1,336,000,000. Kwa upande wa Mererani kuanzia July hadi December 2021 utakuta madini hayo ambayo ni ghafi chini ya gram mbili tulipata shilingi 3,467,000,000 kutoka bilioni 12, lakini pia walipata karat 10,000 kutoka karat 7,920,000,000. Jumla ya mapato yake yalikuja milioni 39 kutoka 1,336,000,000. Tumepata hasara si chini ya asilimia 70. Kwa hiyo vielelezo kama hivi vinaonesha kabisa Serikali inayo sababu, inayo haja na kuna tija kabisa ya kutafakari maamuzi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiacha hasara hiyo bado pia tumeweza kupata hasara kwenye upande wa ajira. Kuna ma-broker pale kati ya 2,500 hadi 3,000 ambao leo wamekosa ajira kwa sababu ya fursa hii ambayo imeondoka kwenda kwenye eneo jingine. Yawezekana Wizara ya Madini kwa data zao ma-broker wakawa ni wachache kwa sababu wengine wengi wameacha kukata leseni kwa sababu mwisho wa siku wameona fursa hiyo imeondoka kwenye eneo hilo. Bado pia kuna majengo ya Serikali ukienda AICC, NSSF, PSSSF nako pia kulikuwa na mashine 437 zimefungwa, ambapo zile mashine leo hazifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiangalia na hiyo bado kuna kodi ambayo Serikali ilikuwa inapata kwa kila square meter katika jengo lile. Kwa hiyo, kwa ujumla wake naona maamuzi haya kwa kweli hayana tija na yameitia hasara nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia sizungumziii Arusha tu peke yake, hizi data ni za sehemu moja tu, nenda Mkoa wa Dar es Salaam, nenda Mkoa wa Mwanza, nenda Mbeya, nenda Zanzibar, nenda kwenye masoko ya madini yote nchi nzima utagundua kwamba hasara ni kubwa kupita kiasi na Serikali yetu chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali ambayo imetoa motisha sana kwa wafanyabiashara. Kwa hiyo ni imani yangu Serikali ya Awamu ya Sita itakwenda kupitia maamuzi haya ili mwisho wa siku tuweze kurejesha furasa hii kwenye masoko yote ya madini nchi nzima ambayo yapo kwa mujibu wa sheria na watu waendelee kunufaika na fursa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tulikuwa tumeendelea kujenga hoja kwamba siku za nyuma kulikuwa kuna minada ya madini inafanyika, pia kulikuwa kuna maonesho ya madini yalikuwa yanafanyika, hapa katikati yamepotea. Minada ile na maonesho yalikuwa yanasaidia pia kwenye utalii, inaleta wageni wengi kutoka nje ya nchi. Siku za nyuma tulikuwa tunafanyia pale kwenye Hoteli yetu ya Mount Meru, leo kuna hoteli nzuri nyingine ya Melia na Hoteli nyingine nzuri zaidi zimejengwa kwenye mji wetu. Kwa hiyo, fursa ikirudishwa itasaidia kwanza kuleta wageni ambao watalala kwenye mahoteli, watanunua bidhaa mbalimbali na mwisho wa siku fursa zitakuwa ni kubwa zaidi. Kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Madini atusaidie kuhakikisha kwamba maonesho yanarudishwa, minada inarudishwa ili kuongeza fursa mbalimbali katika biashara na maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusiana na changamoto ya wafanyabiashara ya vito, watengenezaji na wauzaji nwa bidhaa za usonara kwa maana ya urembo na dhahabu nchini. Hapa ndio sielewi kabisa, sijui kuna changamoto kubwa kiasi gani. Ukiangalia Sera ya Madini ya mwaka 2009 inasisistiza kuwahamasisha Watanzania na wananchi wote duniani kuweza kuongeza thamani ya madini yetu. Hata hivyo, ukiangalia Sera inavyosema na ukiangalia matakwa ya kisheria yaani ni mbingu na ardhi, ni vitu viwili tofauti kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015, Serikali yetu ilianzisha Mchakato wa Rasimu ya Sheria ya Uongezaji wa Thamani ya Madini, ilikuwa iitwe Mineral Value-Added Act, lakini kabla ya hapo kulikuwa na sheria ambayo Sheria hii kama ingeanzishwa ililenga kufuta ile Sheria ya Gold Smith and Silver Smith Act, CAP 228. Hii Sheria ya nyuma hata sielewi nchi yetu ina changamoto kubwa kiasi gani. Ukiangalia kwenye upande wa biashara ya Usonara. Ili mtu aweze kufanya biashara ya Usonara anahitaji kuwa na leseni tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni ya kwanza ni Metallic mineral dealers license, kuna maombi dola 200 na kuna kulipia leseni dola 1000; Kuna Game stone dealers license, kuna maombi dola 200, kulipia leseni dola1000; Kuna Diamond dealers license maombi dola 200, kulipia dealer dola 2000; Gold dealers license maombi dola 200, ada ya leseni dola 1000; na Business license 300,000 unalipia Wizara ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijumlisha gharama zake zote zinakuja sio chini ya Shilingi Milioni 13. Sasa unajiuliza hivi leseni na yenyewe ni chanzo cha mapato au leseni ni namna ya kumtambua mfanyabiashara aingie kwenye mfumo ili mwisho wa siku sasa Serikali iweze kumtambua, afanye biashara na aweze kulipa kodi. Mwisho wa siku sasa tunajikuta na leseni imekuwa ni chanzo cha mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ile sheria ambayo ilikuwa inatakiwa kutungwa ya Mineral Value Added Act mchakato wake ambao uliishia mwaka 2016 kwenye kikao cha Makatibu Wakuu, Waziri achukue Sheria hiyo iendelee na mwisho wa siku alete Bungeni hapa tuweze kuhitimisha na Watanzania waweze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kumalizia tunalo ombi pia, tunaomba uwepo wa leseni moja ya wafanyabiashara wa madini nchi nzima, ikishindikana kabisa basi watoe angalau kikanda. Leo mtu anaomba leseni akienda Mererani awe na leseni, akienda Arusha aende na leseni, akienda Shinyanga afungue leseni halafu kwenye kila Mkoa TRA wanawaita wale watu kwa ajili ya kuangalia masuala ya kodi na masuala mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona Mtanzania ana kitambulisho kimoja tu cha NIDA? Kwa nini pia na leseni isiwe moja ila waweke mfumo mzuri kila anapokwenda kufanya biashara kwenye Mkoa fulani aende akaripoti kwa Afisa Madini wa Mkoa huo na mwisho wa siku aweze kuendelea na shughuli zake. Huo urasimu wa kuwa na leseni kila mahali, hauna tija na unawaongezea tu gharama wafanyabiashara lakini pia usumbufu na kuwapa fursa TRA kuendelea kuwachungulia chungulia kwenye masuala mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusiana na kodi ya PAYEE na SDL kwa wachimbaji wadogo wa Mererani. Siku za nyuma hili suala lilizungumzwa sana na nadhani lilieleweka, kwa sababu kutokana na nature ya biashara ya madini ukimwambia mchimbaji mdogo wa madini leo alipe PAYEE na SDL …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)