Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukua nafasi hii kukushukuru wewe kunipa hii nafasi ya kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Madini. Kipekee ninamshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya katika Taifa letu la Tanzania, namshukuru Ndugu yangu mtani wangu, Waziri wa Madini Dkt. Biteko na Kaka yangu pale Naibu Waziri wa Madini Dkt. Kiruswa. Pia ninampongeza na kumshukuru Afisa Madini wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano mkubwa ambao anaendela kutupatia watu wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nitaongelea mambo mawili jambo la kwanza nitaongelea fursa ya madini ya dhahabu - Manyoni lakini jambo la pili nitaongelea fursa ya madini ya chumvi - Manyoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na fursa ya madini ya dhahabu Manyoni. Mika miwili iliyopita Rais wetu wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu kama sijakosea aliwahi kutamka na alitoa challenge kwa Wizara mbili, Wizara ya Madini na Wizara ya Maliasili aliwaambia kuna baadhi ya mapori ya akiba na hifadhi yanasemekana kwamba yana madini, lakini inaonekana hakuna jitihada zozote zile za kuhakikisha yale madini yanachimbwa, na akasema kwamba hivi wale Tembo na Digidigi watakula hayo madini, hizo dhahabu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki na katika Wilaya ya Manyoni tuna mapori ya akiba matatu, tuna Pori la Akiba la Kizigo, tuna Pori la Akiba la Muhesi na tuna Pori la Akiba la Rungwa. Katika haya mapori yote matatu kuna viashiria vya madini. Huko nyuma iliwahi kutokea booming ya madini ya dhahabu katika Kata ya Sasilo, eneo linajulikana Iruma ambako kuna Pori la Akiba la Muhesi na Kizigo. Vilevile katika Kata ya ya Rungwa, Kata ya Mwamagembe kuna madini ya dhahabu na kule nako kuna pori la akiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Iseke Kijiji cha Simbangulu kuna eneo linaitwa Myunga, hili ni eneo mabalo ni very popular kwa watu wanotoka Kata ya Isseke, kila nikienda kufanya mikutano kwanza wananchi wanalalamika sana, kila wakati wanafukuzwa na watu wa Maliasili, kule kunasemekana vilevile kuna viashiria vya madini ya dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi sasa kwenye ile kauli aliyoitoa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, aliwapa challenge hizi Wizara mbili waende wakatafakari watuambie, kwa nini kama kuna maeneo ambayo yana madini ni Hifadhi za Taifa au Mapori ya Akiba, kwa nini tusije na utaratibu rafiki wa kuhakikisha kwamba tunakuwa it is a win-win situation, wafanye cost benefit analysis, watuambie hivi tukisogeza mpaka tukachimba madini, je italeta athari kwenye hizo hifadhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni nini? Ningemshauri Waziri wa Madini na Waziri wa Maliasili na Utalii watuletee taarifa kutokana na kauli aliyoitoa Rais mmeifikia wapi, hatujaona utekelezaji wa agizo la Rais. Rais akishatamka ni agizo lakini mpaka leo hii tukienda kwenye mikutano watu wanauliza mbona Rais alishauri, aliagiza hatuoni utekelezaji? Kwa hiyo, nawashauri hawa ndugu zangu wawili Waziri wa Madini na Waziri wa Maliasili na Utalii hebu nendeni mkalichakate hili, mtuambie kama kuna potentiality ya sisi kuchimba yale madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingene sanjari na hili ukiangalia kwa mfano yale mapori ya akiba ukiangalia michango yao hata kwenye ile service levy ya Halmashauri ni ndogo sana, kwa mwaka sijuwanachangia Milioni 30 tu, sasa ukiangalia contribution yake is almost insignificant. Kwa hiyo, mimi ningeshauri kwa kweli tuangalie kama hayo maeneo tunaweza tukawachia wenzetu wa madini, wakachimba na yakawa na impact kubwa kwenye GDP lakini yakawa na impact kubwa kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri mimi ningeweza kushauri hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tuna madini eneo linaitwa Londoni ya dhahabu, ndugu yangu mtani wango Dotto unayafahamu. Ndugu yangu Dotto wewe ni mtani wangu siyo ndugu yangu, pale kinachokosekana ni umeme tu, ukipeleka tu umeme utaongeza kiwango cha uchimbaji wa madini pale Londoni Makulu. Kwa hiyo ninaomba mtani wangu Mheshimiwa Dotto hebu nisaidie hili, wapelekee umeme wale wachimbaji wadogowadogo pale Londoni ili tuongeze uchimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho na la pili ni fursa ya madini ya chumvi. Leo nilipitia madukani nimekutana na chumvi inatoka India, nimekutana na chumvi inatoka Kenya, Mheshimiwa Halamga hapa ameeleza tuna-deposit za chumvi nyingi sana Tanzania, tuna kiwanda cha chumvi Kigoma, tuna kiwanda cha chumvi Tanga na Dar es Salaam. Tuna chumvi Lindi, Simiyu na Manyoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Manyoni Mashariki kuna eneo linajulikana kama Kinangali na ile chumvi inajulikana kama chumvi ya Kinangali. Naibu Waziri ulishafika mwaka jana ninakushukuru sana, ulitembelea zile site zote tatu kuanzia Mahaka, Majiri, Kinangali na Mpandagani, ukaagiza Afisa Madini wa Mkoa wafanye utafiti, sasa mpaka sasa hivi taarifa ya utafiti siifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ipo katika maeneo makubwa mawili, kwanza mimi tangu nizaliwe natumia chumvi ya Kinangali mpaka leo hii hakuna uwekezaji wowote wa Serikali katika eneo la Kinangali! Sasa najiuliza kama mimi tangu nizaliwe sasa hivi nakimbilia miaka 50 natumia hiyo chumvi, then utaniambia kwamba chumvi hakuna pale Kinangali hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Serikali watuambie Je, ni kwa kiwango gani ile chumvi ipo pale in terms of quantity, pili watuambie Je, ile chumvi ina ubora? Tatu watushauri sasa kwamba Je, tunaweza kuweka uwekezaji wa aina gani? Tunahitaji viwanda vya size ya kati, lakini viwanda vidogovidogo kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nirudie kumshukuru sana Waziri wa Madini.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chaya kabla haujahitimisha naona kuna taarifa hapa, kutoka kwa Mheshimiwa Cecil Mwambe.

TAARIFA

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Chaya kwamba kuna uzembe mkubwa sana ufanyika kwenye uwekezaji wa chumvi, ukiangalia eneo la Bahari toka Lindi mpaka Tanga eneo hili lote lina chumvi lakini bado wawekezaji wanaruhusiwa kuingiza chumvi nchini kitu ambacho siyo sahihi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Chaya unapokea taarifa.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa ya Mheshimiwa Cecil na labda kabla sijamalizia kama alivyotangulia kusema Mheshimiwa Cecil, sisi kama Nchi hatujawekeza vizuri kwenye fursa ya chumvi hususan katika eneo langu la Manyoni katika Kata ya Majiri hususan Kinangari. Nadhani ni fursa ambayo ingeweza kukuza ajira. Ile chumvi inachukuliwa na watu kutoka Congo, Rwanda na Burundi wanachukua kama raw material wanaenda ku-process wanai-process halafu wanaturudishia tunakuja kununua kwa bei ya jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)