Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii kwa kuchangia Wizara hii. Kwanza nianze moja kwa moja kuomba Serikali iwaangalie sana wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu hali ya ajira kwa kweli ni mbaya sana katika Taifa letu la Tanzania na kama wamejitolea kujiajiri wenyewe basi ni vizuri au ni vyema wakaangaliwa kwa jicho la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna maeneo ambayo wamechukua wawekezaji wakubwa ambayo yamekaa muda mrefu na hawajafanyia kazi yamekwisha rudishwa Serikalini. Sasa basi ni vyema Serikali ikaona ni jinsi gani ya kuangalia kuwagawia maeneo hayo wawekezaji wadogo wadogo ili na wao waweze kufaidi sungura katika Taifa lao la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ni vyema sasa yakaangaliwa maeneo yote ambayo wanachimba wachimbaji wadogo wadogo wakafikishiwa umeme. Hili kwa kweli limekuwa ni tatizo kubwa sana na haswa Mkoani kwangu Mara Wilayani Bunda, Wilaya ya Musoma ya Vijijini, Wilaya ya Tarime, lakini na kote kule ambako kuna wachimbaji wadogo wadogo katika Taifa hili la Tanzania. Naamini kabisa umeme umekuwa ni tatizo kubwa sana na wao pia kwa sababu wanajisimamia ili kupata kipato basi ni vyema wakaangaliwa kwa jicho la ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu Doto Biteko pale walipokuwa wasikivu walinikubalia tukaenda nao kwenye Mgodi wa North Mara Nyamongo tukaongea na wale wawekezaji na wale wawekezaji pia ni wasikivu. Kuna mara nyingine tunawapiga lakini kuna kipindi pia inabidi tuwapongeze pale wanapofanya vizuri. Kwa kweli wamejenga baadhi ya shule kwa mfano wamejenga Shule ya Julius Kambarage Nyerere wamejenga Shule ya Bulege wamejenga pia Sekondari Nyarokoba lakini pia wamejenga Ingwe Sekondari, wamejenga hosteli ambazo baadhi wamerekebisha majengo lakini pia wamejenga hosteli na baadhi ya vituo vya afya wametujengea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado tuna jambo moja ambalo kidogo lina utata, kutokana na kwamba sisi Wanamara lakini pia Wanatarime kama ninavyokuwa naongea mara kwa mara lakini hata watu wote wanajua kwamba ametokea muasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Katika mazingira hayo basi mkoa wetu unatakiwa uonekane mkoa wa mfano lakini mkoa wa kipekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo,wawekezaji wamekwishwa pata faida kubwa sana kutokana na Mgodi wa North Mara lakini pia kule Butiama ambako pia walimaliza na walipata faida za kutosha. Basi ni vyema wakatuwekea barabara wao kama wawekezaji sio wawe wanasubiri tu Serikali itoe pesa ya barabara. Hata wao faida walizopata pia wanaweza kutuwekea basi barabara nzuri ya lami na sisi tukaoneka tukafanana fanana na dhahabu naamini kabisa bado hatujafanana na dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende moja kwa moja kwa kuishauri Serikali kwenye hili suala la malipo ya wale wanaolipwa fidia. Haya malipo yametumia muda mrefu sana ni muda mrefu sana sasa Serikali ikiwa inavutana na wale ambao wametoa ardhi yao kwa ajili ya wawekezaji. Naamini kabisa Serikali imekwisha faidika na uwekezaji ambao umewekwa katika Mgodi wa Nyamongo (North Mara) ambako mwazo ilikuwa Barrick na sasa jina limebadilika limekuwa ni North Mara ambayo ipo ndani ya Barrick.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira hayo sasa ni muda mrefu, toka mwaka 1995 ambapo wananchi wale walitoa ardhi yao kwa ajili ya wawekezaji. Naamini kabisa wamekwisha pata faida ya kutosha na bahati nzuri Dada yangu Mheshimiwa Angeline Mabula, Waziri wa Ardhi alitoa ufafanuzi hapa juzi lakini pia wanapaswa kuliangalia hili. Basi akae Waziri wa Madini, akae na Waziri wa Ardhi waliangalie hili, ili kusudi na wale wananchi pia waweze kumaliza tatizo hili, lakini Sheria ya Ardhi inasema mtu anapofanyiwa uthamini wa ardhi yake na ardhi ikarudi Serikalini baada ya miezi sita, ikivuka miezi sita alipe pia faida ya ile ardhi yake kwa sababu haitumii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tokea mwaka 1995 ni miaka 20 na zaidi. Naamini kabisa Serikali sikivu italifanya hili na kutokana na kwamba wananchi wa Tanzania sasa wana hali ngumu sana, huo ndio ukweli hali ni ngumu, vitu vimepanda bei, gharama ni kubwa wale watu wanajenga nyumba ambazo kwa kweli inakuwa thamani yake ni ndogo sana na wengine wanashindwa kumalizia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nimuombe Waziri atakapokuja hapa ku wind up atuelezee ni jinsi gani atafanya ili kusudi wale wananchi, kwa sababu sasa ni miaka mingi imepita wapewa riba yao. Katika ile pesa yao, katika ardhi yao ambayo waliitowa kwa ajili ya wawekezaji ambayo naamini kabisa tunapofanya tathmini au uthamini kwa ardhi inapokuja kwetu itakuwa ni fundisho pia ambalo watalipwa haraka wanaokuwa wameshafanyiwa uthamini kwa sababu sasa hili tatizo linatokea. Naamini kabisa sio tu mkoani kwangu Mara hata maeneo mengine ya Tanzania naamini hili tatizo limekuwa ni kubwa sana la kutolipwa mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende moja kwa moja kwa kusema nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, unachapa kazi Mwenyezi Mungu akubariki sana kwa kweli unaweza na unaiweza Wizara Mungu akubariki sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio chetu kikubwa kwa Wanamara na Wanatarime tunaomba…
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tulipwe pesa zetu za uthamini kwa sababu hadi sasa mashimo yamekwishwa kuwa makubwa sana, wawekezaji wamekwisha pata pesa nyingi sana. Hivyo tunaomba basi na sisi tulipwe ili kusudi na sisi tufaidi ile dhahabu yetu ambayo sisi wenzenu Tarime tulikuwa hatujui biashara ya kulima..
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, … na kilimo chetu sisi ilikuwa ni dhahabu sasa kama wametutoa kwenye dhahabu na sasa wanataka tulime au tufanye shughuli nyingine basi nafikiri ni vyema tukalipwa ili kusudi na sisi tufaidi. Tufaidi angalau kasungura ka Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na Mungu akubariki.