Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kazi nzuri ambayo anafanya kwa ujumla wake lakini pia kwa kuchukua hatua na kutoa maelekezo kwa Waziri wa Madini Dkt. Biteko na wenzake kutanzua mgogoro mkubwa ambao ulikuwa pale Tarime wa mambo ya miradi ya CSR. Kwa hiyo, tunamshukuru sana kwa sasa kwa kweli siyo kama hali ilivyokuwa hapo awali, kuna mabadiliko makubwa sana katika miradi hii ya CSR. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana niseme tu kwamba ule Mgodi unaitwa Barrick North Mara na mgodi huo ume-take over kutoka Acacia tangu mwaka 1995/1996. Kwa hiyo, ilirithi madeni pamoja na mkataba na uchimbaji na kila kitu. Kile ambacho wananchi walikuwa wanadai kutoka nyuma maana yake Barrick kwa sasa wanawajibika kulipa kwa sababu ilikuwa kwenye mkataba na walikubaliana. Nilitaka niweke maelezo very clear. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaipongeza Barrick pamoja na mvutano ambao ulikuwepo tangu nimekuwa Mbunge katika jimbo lile 2020 mpaka leo kuna mabadiliko makubwa sana. Barrick zile ajira 46% wanatoa katika vijiji 11 pale pale kwenye Mgodi wa Barrick North Mara. Vilevile hata bidhaa ilikuwa inatoka nje ya hata ya nchi. 80% ya bidhaa pale mgodini inatoka ndani ya nchi na wengi akina mama na vijana wana-supply katika Mgodi wa Barrick North Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile walikuwa wanamsikia Rais wa Barrick, leo navyozungumza anakaa na wale wananchi wanazungumza na viongozi wa vijiji wanapanga mipango pale mtaani kabisa katika jengo la sekondari na wanazungumza na wanapeleka maombi kadhaa ambayo mgodi umepokea na wanaendelea kuyafanyia kazi. Hayo ni maendeleo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kwenye miradi ya CSR kuna mambo mawili hapa; la kwanza kuna fedha ya kwanza ambayo ilienda Barrick wameweza kutoa fedha mara mbili tu. Mara ya kwanza ni mwaka 2019/2020 wakati huo nilikuwa Mbunge wa Ukonga. Katika fedha hiyo ililipwa shilingi bilioni 5.7. Nimelalamika hapa Bungeni na ningeomba Mheshimiwa Waziri hili jambo la miradi ambayo fedha ilipelekwa kwenye miradi mbalimbali. Miradi mingi imekuwa viporo, nondo zimekuwa stranded, ma-cement yameharibika mpaka leo. Ripoti ya CAG haijatoa taarifa nani mhusika, hiki kitendo kimekwaza Wananchi wa Tarime na kama Mbunge sifurahii. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri asimamie jambo hili ile ripoti itoke fedha hazikutumika vizuri miradi haikukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ya awamu ya pili ambayo tumepokea mwaka jana yaani 2022/2023 navyozungumza shilingi bilioni 7.3 ipo kwenye miradi mbalimbali ya Halmashauri ya Tarime Vijijini na tumebadilisha utaratibu, hii miradi ipo kwenye kata 26. Mheshimiwa Naibu Waziri amekuja tulizungumza vikao mbalimbali tunamshukuru mabadiliko ni makubwa sana. Kilichotokea kwamba fedha hii Kamati ya TAMISEMI ambayo ni mjumbe ilikwenda pale ni kwamba kwa kuwa kuna changamoto nyingi hakuna madawati, hakuna visima vya maji, hakuna zahanati, watoto wanakaa chini. Kwa hiyo, tulikubaliana kwamba fedha ile ukiipeleka kwenye kata, Diwani wa kata husika kupitia WDC wanaangalia wenye kipaumbele ni kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini baada ya batch hii kwenda tumejenga madarasa ya kutosha, tukaweka madawati, tukachimba visima, tukajenga majengo ya mama na mtoto, tukapeleka hata vitanda tu vya kina mama kujifungulia, ina maana awamu nyingine ijayo tunaenda kuteua miradi ya kimkakati ambayo sasa itaonekana kwa macho na kwa sababu Barrick wamekubaliana kuwachukua baadhi ya viongozi kutoka Nyamongo, kutoka katika Halmashauri yetu ya Tarime DC wataenda kujifunza wenzetu wa Msalala kazi ambayo imefanyika na pale Kahama. Tunaamini kwamba tunaendelea vizuri kwa maana ya Mgodi wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wameahidi kujenga uwanja wa mpira pale, wana-supply maji katika vijiji 11 kwenye kata tano kutoka kwenye chanzo chao ili kuondoa sintofahamu kwamba maji yale ni ya sumu walikuwa hawawezi kuyaamini kuyatumia lakini Mheshimiwa Waziri yako mambo ya Wizara kufanya katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano amezungumza mwenzangu kwamba kuna watu wana dai. Kule kulikuwa na vijiji vitano ambavyo viliingia mkataba na Mgodi wa Barrick kutoka Acacia kwamba katika uzalishaji watapata 1%. Hiyo fedha mara ya mwisho wamelipwa mwaka 2012. Mpaka leo fedha haijwahi kulipwa, ni mgogoro mkubwa kwa sababu kila wakikutana wanajadiliana walipwe fedha zao. Hili ni Wizara isimamie lipo kwenye mkataba na hiyo fedha walilipwa dola milioni mbili mpaka walienda mahakamani na jalada lipo. Waliambiwa msiende mahakamani, msigombane na mgodi mulipwe fedha. Kwa hiyo, naomba jambo hili litekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ile ikienda kuna wananchi wanadai maduara 360 mpaka leo. Wamezunguka sana wamesaga lami. Wameenda kila mahali mpaka kwa Rais na Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja pale. Kama vijiji vile vitano vikilipwa 1% ndiyo watalipwa wenye maduara. Hawawezi wenye maduara yakalipwa fedha ambayo haifiki. Kwa hiyo, kama kweli tunataka kuwasaidia wale watu.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita kuna taarifa.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa muongeaji taarifa kwamba tena kati ya hao ambao hawajalipwa mpaka sasa hivi kuna baadhi yao wengi wao wamekwisha fariki. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita unapokea taarifa?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni wengi wamefariki dunia na wameacha haki zao zinapotea. Kwa hiyo, nasema kwamba wale watu wakilipwa vijiji vile vitano vikilipwa 1%, watafanya miradi ya maendeleo lakini watu wa maduara watalipwa lakini kwa sasa ilivyo wale watu wanagombana wenye maduara ndiyo fedha yao kwa sababu waliwekeza hawajalipwa, vijiji vinasema hatuwezi kulipa kwa sababu hatujalipwa. Mgodi unasema kwamba wao hawajaendeleza maeneo yale, kama hawajaendeleza maeneo warudishe kwenye vijiji, vijiji vitafute muwekezaji mwingine watachimba ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine ambalo nataka niseme hapa. Kuna mgogoro mkubwa katika eneo langu na hili jambo mlisikilize vizuri. Mgogoro uliopo ni kwamba mgodi unafanya evaluation ya kutoa maeneo ya watu. Tuna maeneo kama Nyamichere tangu mwaka 2012 maeneo kama Murwambe yamekuwa mabovu majengo ya watu, maeneo kama Kewanja, Komalela, Nyabichune. Hapa tunazungumza kata tano zinazozunguka ule mgodi. Watu hawa wamefanyiwa tathmini lakini mpaka leo hawajalipwa. Sasa kuna ugomvi pale, ukienda kwenye mgodi wanasema sisi tunalipa tulichoambiwa tulipe, mdhamini mkuu yupo Wizara ya Ardhi kwa Mheshimiwa Angeline Mabula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wanavutana, ningeomba Mheshimiwa Waziri wa Madini usimame katikati. Kitendo cha watu wale kutolipwa fedha zao na tena wanalipwa kiasi kidogo, ekari moja ya ardhi ambayo ina dhahabu chini wanalipwa shilingi milioni tano tu. Ndiyo maana umasikini hauwezi kwisha, unachukua ardhi, ulipe shilingi milioni tano aende atafute eneo lingine ajenge, aanze kuwekeza, na ana familia kubwa, extended family pale. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili jambo limeleta taharuki. Kuna ugomvi ambao siyo wa lazima. Kama Wizara ya Ardhi itafanya tathmini vizuri, ikapandisha bei ya ardhi, ikafanya tathmini kwa wakati, mgodi wanasema tukiambiwa na Serikali lipa shilingi milini 10 tutalipa. Tumeambiwa tulipe shilingi milioni tano ndiyo tulichoambiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba mtanzue huu mgogoro ili wale watu wafanye kazi ya uwekezaji wapate ushirikiano na wananchi wale, wafanye kazi nzuri. Mgodi wa Barrick ndiyo walipaji wakubwa wa kodi kuliko migodi yote hapa Tanzania. Lakini malalamiko ni mengi kwa sababu wale watu wanatambua haki zao. Wanajua chini ya ardhi kuna dhahabu, kuna matrilioni lakini hizo fedha hazilipwi zinalipwa kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mgogoro ule kati ya Barrick na wananchi niutanzue, na hii ni kwa Wizara ya Madini na Wizara ya Ardhi kufanya kazi pamoja ili watatue jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine, migogoro mingi iliyopo katika maeneo yetu ni kwa sababu kwa kweli ukiangalia hali za watu katika maeneo ya migodi, ikiwepo Nyamongo, hasa wale wananchi wa kawaida maisha yao hayafanani. Sasa hivi Nyamongo imechangamka sana, mgodi umetengeneza mahusiano, umewekeza, watu wamepata kazi, lakini wengi ni wageni ambao wamekaa pale. Wananchi wa kawaida wenye ardhi wanalipwa kidogo sana. Kwa hiyo ningeomba jambo hili Mheshimiwa Dotto Biteko…

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MWITA M. WAITARA:…umesifiwa sana kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo kuendesha maisha yao. Sasa njoo Nyamongo nenda maeneo ya machimbo, wezesha wananchi wa kawaida, wale wanaozunguka migodi wapate maisha mazuri, wafanane. Ametuleza Mheshimiwa Salome Makamba, ni kweli kwamba ukimlipa fedha kidogo…

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MWITA M. WAITARA: … anaenda kuanza maisha, lakini akipata hisa, akapata share kidogo maana yake atakula yeye na kizazi chake na ndugu zake na mahusiano
yataimarika. Vilvile nikiangalia bei ya mazao na bei ya ardhi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Waitara muda wako umekwisha nakuongeza dakika moja nyingine malizia hoja yako.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru sana, niombe Mheshimiwa Waziri wa Madini ufanye tathmini nzuri sana…

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. MWITA M. WAITARA:…, je wananchi wale ambao wanalipwa fedha wanaboreshewa maisha au fedha inapita mlango mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nilitaka nikuombe, fanya tathmini, uchunguzi wa kimadini ya Locoba, Kuihanchat, Koronga, Nanungu na Hifadhi ya Serengeti. Migogoro mingi iliyopo pale watu wanaamini pale kuna dhahabu na inafichwa haijulikani. Nenda ufanye uchunguzi mtangaze kuna dhahabu ufanyike uchimbaji halali ili kuondoa migogoro iliyopo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba niunge mkono Bajeti ya Mheshimiwa Dotto Biteko ameiheshimisha amekuja na mambo wakati wa shida, watu wanakusikiliza lakini lile Bwawa la Nyamongo la maji machafu Mheshimiwa Rais aliagiza akiwa Makamu wa Rais kwamba lichimbwe jipya mpaka leo halijachimbwa, tunaomba utekelezaji, ahsante. (Makofi)