Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukushukuru tena kwa kunipa nafasi hii kwa ajili ya kuhitimisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Wizara imepokea michango ya Waheshimiwa Wabunge waliyoitoa kwa kuzungumza na walioandika. Tumepata ushauri na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ni muhimu kwetu katika utekelezaji wa majukumu yetu kama Wizara na katika usimamizi wa Sekta yetu ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla ushauri na maoni yaliyotolewa au mapendekezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni ya muhimu sana kwetu na yana lengo moja tu kuimarisha Sekta ya Madini na kuifanya sekta hii ichangie zaidi kuliko inavyochangia hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliyopata nafasi ya kuchangia Hotuba yangu. Jumla ya Wabunge 30 wamechangia Hotuba hii kwa kusema na kwa kuandika, ambapo Waheshimiwa Wabunge 29 wamechangia kwa kuzungumza na Mbunge mmoja amechangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii vilevile kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba hoja zote zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye mjadala uliokuwepo hapa toka jana, Wizara tumezichukua kwa uzito wa aina ya pekee na kwa kweli hakuna hoja hata moja tunayoipuuza au tunayoifanya kuwa ndogo, zote tumezichua kwa uzito wake na kwetu sisi wametupa kazi ya kwenda kufanya katika kipindi hiki cha mwaka fedha ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda sitaweza kuzitolea ufafanuzi hoja zote kwa sababu iliyo dhahiri kwamba muda hautoshi, hoja ni nyingi na maelezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge yote ni ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ufafanuzi mchache kwa mambo ya jumla na mambo mahususi pengine kwa mifano tu. Kabla sijafanya hivyo naomba tena nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kunipa jukumu la kusimamia Sekta hii ya Madini. Nimshukuru sana Dkt. Philip Isdori Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakituelekeza kutekeleza mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata pongezi nyingi katika michango ya Waheshimiwa Wabunge. Tunazichukua pongezi hizo kwa tahadhari kubwa ya mgema kusifiwa tembo asije litia maji, lakini kuwaeleza tu Waheshimiwa Wabunge, kama kuna watu wanastahili pongezi ya mafanikio ya Sekta hii ya Madini, wa kwanza ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; wa pili ni Dkt. Philip Isdory Mpango, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; na wa tatu ni Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu kazi zote tunazozifanya zinatokana na maelekezo ya viongozi hawa ambayo nia yao ni kuiona sekta hii inakwenda mbele na sisi tunafanya kazi ile ambayo wametutuma. Kwa kweli naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi hizo. Nataka niwahakikishie kwamba pongezi walizotupa na changamoto walizotupa zitatuongezea nguvu zaidi ya kufanya kazi ili tutakaporudi hapa mwakani Mungu akipenda, basi sekta hii ije ieleze mambo yaliyo bora zaidi ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyashauri katika michango yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nisije nikasahau kuwashukuru sana sana wasaidizi wangu Wizarani. Nikianza na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kiruswa, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Naibu Katibu Mkuu, Kamishna wa Madini, Watendaji wote wa Taasisi za Wizara zilizoko hapa ambao kwa kiwango kikubwa wao ndiyo wasimamizi wakuu wa mambo yote ambayo tumeyafanya Wizarani. Naomba niwashukuru wafanyazi wote wa Wizara kuanzia kada ya chini mpaka ya juu kwa kuwa naamini bila wao tusingefika hapa. Nawashukuru sana kwa support wanayonipa Wizarani na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki sana wao na familia zao ili waendelee kuchapa kazi hii kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wameendelea kutamani itokee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee mambo ya jumla machache. Jambo la kwanza limeelezwa na Waheshimiwa Wabunge wengi. Kwanza, tunapaswa kufanya zaidi ya hiki tunachofanya, wote tunakubaliana, ni kweli tunaweza kuhubiri kwamba tuna mafanikio, lakini maoni ya Waheshimiwa Wabunge na Watanzania ni kwamba bado hatujafanya vizuri zaidi. Tufanye vizuri zaidi kwa kuongeza mchango wa Sekta ya Madini, lakini tuwasaidie wachimbaji wadogo na tuvutie uwekezaji mwingi zaidi nchini ili tuweze kupata zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameenda mbali zaidi, wamekuja na mfumo mwingine wanaopendekeza na nakubaliana nao kwamba ni muhimu sasa Serikali na yenyewe iwe mwekezaji. Tukubaliane hapa jambo moja ile dhana ya zamani ya kuwaona Watanzania wao kazi yao ni kuuza vitunguu, juisi, madini ni ya watu wengine Bunge hili leo limethibitisha tumehama. Wote tunawaona Watanzania kama watu wanaostahili kupewa fursa na wakipewa fursa tutapata mapato kutokana na wao na hiki ndicho kinachotupa ujasiri wa kusimama hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona watu wanasema leseni zisizoendelezwa zifutwe wapewe watu wengine, hiki ndicho tunachotaka ku–empower watu wetu na leo nawaambia wenzangu pale Wizarani kwamba ni vizuri tukaweka maono makubwa hadi tuogope if you have a vision that doesn’t scare you hiyo vision ni ndogo sana. Tuwe na maono makubwa yatutishe wote mpaka tufike mahali tuseme hili ninaloliweka kweli nitalifikia? Ili litupe kazi ya kwenda kulisimamia kwa nguvu zote bila kupumzika na nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge sekta hii kama Wabunge wanavyosema, itachangia zaidi kwa sababu potential ipo na nitawaambia baadhi ya maeneo ambayo tunayaona ni potential yapo kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 iliyopita hatukuwahi kufungua mgodi mkubwa, tunaingiza kwenye pipeline migodi mipya mingine ambayo Wabunge wameona tumesaini mikataba na niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge wale wanaosema kwamba tumeingia mikataba, free courage interests hatuwezi kupata, nataka niwaambie iko migodi imeanza kulipa free courage interests hapa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie pia kwenye Bodi ya Makampuni yote tuliyoingia ubia siyo kweli kwamba hatuna Wajumbe kwenye Bodi. Tunao kwenye bodi na kwenye mikataba ile hata kwenye management kuna watu tunateua kuwaingiza na kuna baadhi ya watu ili mgodi uweze kumteua ni lazima awe approved na Serikali, huko nyuma haikuwa hivyo, ilikuwa mtu mwenyewe mwenye leseni anateua watu wanaendesha shughuli halafu wewe huwezi kujua. Hata financial model tunafanya joint financial modeling hafanyi peke yake mwekezaji, tunajua kila aina ya madini, kila aina ya kitakachochimbwa na faida tutakazozipata ndiyo maana tunaweza tuka-project tutapata kiasi gani. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iko makini sana kulinda mali za Watanzania, kuhakikisha kwamba hatuwezi kuona tunapoteza hata milimita moja. Nafahamu yako mambo mengine ambayo kadri tunavyoendelea tutaona tuna mahali fulani pa ku– improve. Hili nilieleze kurekebisha sheria kwa maoni yangu mimi si dhambi, kurekebisha sheria ni uungwana, kwamba huwezi kukomaa na jambo ambalo practically halifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tukiliona jambo ambalo tukienda site halifanyi kazi tunarudi hapa kwa wale wanaotunga sheria tunawaambia jamani mtusaidie hili jambo huko site halifanyi kazi na tunazungumza kwa haki kabisa na Waheshimiwa Wabunge wamekuwa rahimu wanatukubalia, tunarekebisha. Lengo ni kuifanya sekta hii ikue, hatufanyi jambo lolote la kuonyesha kwamba Serikali ina mabavu zaidi tufahamu Waheshimiwa Wabunge, asilimia kubwa ya Sekta ya Madini inaendeshwa na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi ili iweze kufanya kazi, ni lazima uiwekee mazingira rafiki ya kibiashara, upunguze userikali, uwe mfanyabiashara na wewe, STAMICO yuko hapo anafanya kazi ya kuwekeza kwa niaba ya Serikali, anafanya biashara kwa niaba ya Serikali, lazima akili yake na yeye afikiri kibiashara. Leo tunapata kandarasi kwa mara kwanza toka tumepata uhuru, STAMICO anapata kazi za kufanya uchorongaji anapambana na makampuni makubwa ya nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huku ndani ukija STAMICO anataka kununua kipuli kwa mfano rig machine imeharibika kitu kidogo kinahitaji labda dola laki moja spea. Wewe ukirudi huku ndani unataka ufate Sheria ya Manunuzi ambayo itatangaza tenda siku 14, wakati kuna mkandarasi mwingine kifaa kimeharibika leo, kesho saa tisa kimekuja amefunga, biashara inaendelea, hawezi kufanya biashara, ndiyo maana Mheshimiwa Rais akasema tuiangalie na Sheria ya Manunuzi ile ambayo inazuia biashara, tuirekebishe. Nataka niwahakikishie Wizara ya Fedha wanafanyia kazi hiyo ili tuwe na sheria ambayo ni rafiki itakayoruhusu biashara hapa nchini ili mwisho wa siku sekta hii iweze kukua. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, kwa habari ya GST, asingeweza kufanya utafiti kwa sababu ya sheria aliyokuwa nayo, kazi yake ilikuwa ni ku– rospect peke yake anaishia hapo, explorations haikuwa kazi yake, tulikuja hapa baada ya maoni ya Waheshimiwa Wabunge, tukaleta hoja wakatukubalia, tumebadilisha sheria tumempaka Mamlaka GST, sasa kwa Bunge hili aweze na yeye kufanya utafiti hasa kwa madini mkakati kwa sababu lazima tukubaliane dunia inaelekea huko. Sasa hivi GST anafanya explorations na ataingia mikataba na makampuni mengine binafsi na Serikali itaweka fedha pale kwa ajili kuweza kumpa mamlaka zaidi ya kufanya utafiti. Nataka niwaambie hili jambo ni jipya, twende nalo taratibu, lakini mwisho wa siku tutaona kile tulichokusudia kukipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Gambo na wengine wamezungumza juu ya minada, naelewa concern ya kubadilisha kanuni ile ya Mererani controlled area ni ya kuzuia madini yote kuuzwa nje ya Mererani. Lengo lilikuwa ni kufanya Mererani uwe Mji wa kuchangamka. Mheshimiwa Rais ameshatupa maelekezo na tumelifanyia kazi. Nataka niwaambie tunarejesha minada ya madini, tunarejesha maonyesho ya madini ya vito hapa nchini kama ilivyokuwa huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliacha kufanya hivyo nadhani ilikuwa mwaka 2017, tunarejesha sasa na tunaweka utaratibu na hivi ninavyozungumza tuna timu ya wataalam ambayo imekwenda kuangalia minada mingine inavyofanyika Thailand, India ili tuweze kufanya jambo hili na wale wote wanaoendesha minada huko duniani wako wengi wamekubali kuja kutuendeshea minada hii ili tuweze kuwapa bei nzuri zaidi wachimbaji wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusilaumiane, tuamini kwamba kila jambo tunalolifanya nia yetu ni njema kuifanya sekta hii ikue. Nataka niwahakikishie Wabunge kwamba mambo yote haya yatakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja limezungumzwa la migogoro na kwamba Wizara kunapotokea mgogoro hatua ya kwanza tunaenda kuwafukuza watu na kwamba kuna mahali pengine wachimbaji wakipata madini wanakwenda kuwafukuza. Tuweke rekodi sahihi, toka Serikali ya Awamu ya Sita sikumbuki eneo lolote ambalo wachimbaji wadogo wamefukuzwa. Nataka niwaambie eneo ambalo wachimbaji wadogo wanaweza kusimamishiwa biashara ya uchimbaji kunakuwa na sababu za kiusalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Getere amezungumza hapa Kinyambwiga, Kinyambwiga usingeweza kuruhusu waendelee kuchimba kwa sababu ni eneo ambalo watu wenyewe walitaka kuonyesha wana nguvu kuliko hata wasimamizi wenyewe. Tumepeleka Polisi pale, Polisi amepigwa, tumepeleka walinzi, walinzi wamepigwa. Hatua ya kwanza, ni ku–restore peace ili uweze kuchimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuchimba mahali penye mapigano na lazima niwaombe wachimbaji wetu nchini waelewe kwamba Serikali hii inatoa mazingira yote ya kuchimba, tunafuta maeneo mengi ambayo Serikali inalaumiwa tuwapatie wachimbaji wadogo, haiwezekana tena hata wale wanaokuja kusimamia pale na wao waweze kufanyiwa vurugu. Tulifanya hivyo kwa sababu moja na baada ya amani kurudi mgodi ule tuliufungua na biashara inaendelea. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuendelee kutoa elimu kwa wachimbaji wetu kwamba, madini haya ni yetu tuyachimbe kwa amani yaweze kutupatia manufaa na mwisho wa siku tuweze kupata faida ambayo tunakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie jambo la refinery kwa sababu ni jambo kubwa. Katika Sheria tulizorekebisha mwaka 2017, Serikali ilielekeza au Bunge lilielekeza kwamba sasa madini yote yaongezwe thamani hapa nchini. Kazi ya kwanza ilikuwa ni kuvutia watu waje wajenge mitambo ya kusafisha dhahabu ili tupate refinery. Refinery ili uweze kupata certifications process yake ina inachukua muda mrefu, wako waliyofikia hatua ya ISO, wako wengine wanakamilisha taratibu ili mambo haya yaweze kufanyika. Sasa tumefanya nini sisi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichoamua na Benki Kuu walikuja kwenye Kamati ya Mheshimiwa Kitandula, wakatoa taarifa, kanuni ya kununua dhahabu tayari imekamilika na wameanza kununua dhahabu na hivi ninavyozungumza wameshanunua kilo mia nne kama Benki Kuu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka sasa tunakamilisha taratibu zilizoko kwenye refinery ili tuweze kuanza kununua dhahabu kama Serikali na kuanzisha hicho kinachoitwa National Gold Reserve kwa ajili ya kuhimarisha currency yetu. Tutaenda taratibu lakini tunataka twende kwa uhakika ili makosa yaliyotokea huko nyuma yasije yakajitokeza. Wale wenye refinery nawaomba wenye mabenki wawape muda, kwa sababu kuna mambo mengine ambayo ni kisera ambayo bado tunayarekebisha. Kwa mfano ni lazima kwenye refinery uweke incentive, tumepunguza kupitia Bunge hili mrabaha kwa wale wanaouza dhahabu kwenye refinery kutoka asilimia sita hadi asilimia nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaangalia gharama ya ku– refine, isiwe kwa mchimbaji iwe kwa BOT na Benki Kuu wamekubali kuchukua gharama, lakini tunaangalia vile vile kama inspection fee tunaweza tukaona kiasi fulani kibaki kwa ajili ya refinery ili mchimbaji anapopeleka madini yake asipate gharama yeyote. Kwa kufanya hivyo dhahabu itakuja. Mwisho wa siku kwa sababu sheria inaturuhusu, tutazuia kabisa kama nchi nyingine kusafirisha dhahabu ambayo haijasafishwa kwa sababu viwanda vya kufanya hivyo viko hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nirudie tena kuwashukuru sana sana Waheshimiwa Wabunge wote kwanza kwa namna wanavyotusaidia kusimamia Sekta ya Madini. Mimi huwa nawaambia wenzangu sekta hii hatusimamii Wizara, tunasimamia wote, maoni na michango ya Waheshimiwa wabunge ndiyo inayotufanya sisi twende kwenye drawing table tuone jambo gani turekebishe na jambo gani tulifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata haya mambo mengine, Mheshimiwa Hassan amezungumza habari ya cyanide na mercury, nilieleze tu tulishapitisha azimio hapa la kupiga marufuku matumizi ya mercury na matumizi ya cyanide na mercury ni tofauti, lakini vile vile recovery ya dhahabu labda tu kwa taarifa ya faida ya Bunge, recovery ya mercury ni ndogo ni chini ya asilimia ishirini wakati cyanide hutumii kwa mkono kama unavyotumia mercury, yenyewe unatumia either kwa VAT leaching au kwa CIP au CIL. Hii ni ya kiwanda kabisa siyo uchenjuaji wa kawaida kama wa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe nchi nyingi sana na wanaotuzunguka wamehama kwenye matumizi ya zebaki kwa sababu ni hatari zaidi kwa afya za watu, tuwa-support watu wetu kwamba waanze kutumia teknolojia ya kisasa kwa ajili ya uchenjuaji wa dhahabu badala ya kutumia kemikali ambayo ina athari kwa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kusema maneno hayo nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi, lakini vile vile nikushukuru sana kwa namna ulivyotusimamia pamoja na Mheshimiwa Spika, Naibu Spika kwa namna ambavyo mnatuongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba sasa Bunge lako likubali kutupitishia fedha hizi ili tuweze kwenda kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.