Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa hii nami niweze kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nachukua nafasi hii kumpongeza Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuleta maendeleo kwa wananchi. Nampongeza zaidi kupitia hizi fedha za mafunzo kwa vijana. Kwa kweli mama anafanya kazi kubwa katika kuhakikisha kwamba anatengeneza vijana matajiri katika sekta hii ya mifugo na uvuvi. Nadhani sote tunatambua kwamba, ni moja kati ya sekta ambayo wananchi wetu wengi wamejiajiri katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara inayoongozwa na mtani wangu, Mheshimiwa Abdallah Ulega, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa na mambo mawili ya kuzungumza. Jambo la kwanza ni vijana wanaopatiwa mafunzo ya unenepeshaji mifugo. Naunga mkono kupitia mzungumzaji aliyemaliza kuongea kwamba, ipo haja kubwa sana ya kuongezewa fedha kwenye huu mradi ili uweze kusambaa nchi nzima na uweze kuwanufaisha vijana wengi kupitia mradi huu. Ni mmoja wa miradi ambao una matokeo ya haraka kama ambavyo tumeona, unenepeshaji wa ng’ombe unahitaji miezi mitatu na ndani ya miezi mitatu unaweza kuuza ng’ombe kwa kuhakikisha kwamba tunapata fedha katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Wizara kwamba vijana kama ambavyo tumeona wanahusishwa kwenye jambo hili la huu mradi wa unenepeshaji wa ng’ombe, ipo haja kubwa sana tuweze kuona uwazi wa vijana hawa ambao wanachaguliwa kwenda kwenye haya mafunzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye hotuba kwamba tuna vituo nane na viko katika mikoa mitatu; Tanga, Mwanza, na Kagera. Bado vituo hivi ni vichache na havijasambaa nchi nzima, na vijana wengi wanahamasika katika eneo hili ili waweze kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema, hadi kufikia Machi, 2023 vijana 238 wako kwenye huu mradi. Bado hii idadi ni ndogo sana, na kwa mwenendo huu, tija yake haiwezi ikaonekana kwa haraka. Hivyo basi, nashauri ushirikishwaji, ama waongeze idadi ya vijana wengi waweze kuwa-recruit kwenye huu mradi ili basi tuweze kuona tija yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema kwamba mnufaika atapewa ng’ombe 10 wa kunenepesha na kuwauza kila baada ya miezi mitatu, basi Wizara iongeze fedha za kutosha ili basi vijana wengi waweze kuhusishwa katika mradi huu. Nashauri Waziri wa fedha aongeze fedha katika mradi huu uweze kuinua vipato vya vijana wengi na kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo kwenye ufugaji wa vizimba, tunampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akizungumzia mara kwa mara juu ya mradi huu, mradi ambao utawanufaisha vijana wengi. Nasisitiza zaidi kwamba Wizara iweke mpango mzuri ambao utawasaidia vijana wengi waweze kujiajiri katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo napenda kuzungumzia ni zoezi la utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake, ukurasa wa 27, nanukuu: “Aidha tarehe 3 Novemba, 2022 Serikali ilisitisha zoezi la utambuzi wa mifugo kwa muda ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza hapo awali.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri hajatupatia way forward, baada ya haya yote, nini changamoto waliyoiona? Wamejipangaje hususan katika ku-resume jambo hili ili liweze kufanukiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba ni takwa la kisheria kuweza kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Mifugo ya Mwaka 2006 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba jambo hili ni muhimu ili tuweze kuwa na taarifa sahihi ya mifugo katika maeneo yetu. Pia, Serikali iweze kuboresha sera ama kuweza kuwa na idadi kamili ya mifugo tuliyonayo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba, zoezi hili lilikuwa lina changamoto mbalimbali kama malalamiko katika ada, upungufu wa kanuni, usimamizi, na utekelezaji wake. Sasa tungependa kufahamu ama kusikia wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha hoja yake tuweze kujua wamejipangaje katika zoezi hili ili kusaidia wafugaji wetu? Ama Serikali yetu kumsaidia mfugaji na kuboresha miundombinu ya wafugaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la kuhesabu mifugo ni muhimu sana. Baadhi ya wananzengo ama wananchi, wamekuwa wakilitafakari na wakihoji kwamba mwaka 2022 tumetumia zaidi ya Shilingi bilioni 200 katika zoezi la sensa, na zoezi hili lilifanikiwa kwa asilimia 100. Sasa kwa mwananzengo wa kawaida, anajaribu kufikiria kama katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi tumehesabiwa bila kutoa chochote, iweje sasa unakuja kuhesabu mifugo unaanza kuweka mambo ya ada?
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali, kwa sababu hii imekuwa ni kero kubwa kwa wafugaji, Serikali iweze kuona ni namna gani itaendesha zoezi hili ili kila mfugaji aweze kuondokana na changamoto hiyo ya ada mbalimbali ambazo zimekuwa zikitozwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhesabu mifugo ya mwananchi na kuweka ada ni jambo ambalo limekuwa kikwazo sana kwa wananchi na Serikali inatakiwa ije na mpango mzuri ambao utawasaidia wafugaji waweze kutoa ushirikiano mzuri. Kwa sababu, kama zoezi hili litaendeshwa bure, nina imani wafugaji wote; sioni kama kuna mfugaji yeyote ambaye hatatoa ushirikiano kwenye zoezi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasisitiza Serikali iandae utaratibu mzuri, na sidhani kama kuna mfugaji yeyote ambaye hatatoa ushirikiano kwenye zoezi hili kwa sababu, ni zoezi ambalo lina manufaa kwao kuweza kutengenezewa mazingira mazuri katika maeneo yao ya mifugo na suala zima la utoaji wa chanjo, na udhibiti wa magonjwa mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo napenda kuzungumzia, naishukuru Wizara kwa kuja na mpango mzuri wa kuzalisha nyasi kwenye mashamba makubwa kama ambavyo Mheshimiwa Waziri katusomea kwenye hotuba yake. Jambo hili ni zuri sana na litasaidia kuondokana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kama endapo tutakuwa na maeneo makubwa ambayo nyasi zinazalishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kufanikisha jambo hili, ipo haja ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na Wizara ya Kilimo, waone namna gani ambavyo watashirikiana kupitia vijana ambao wanafanya ule mradi wa Jenga Kesho Bora wa BBT, ili kuwe na coordination nzuri ambayo itasaidia Wizara, vijana hawa kupitia mafunzo wanayoyapata waweze basi kupatiwa na namna gani wanaweza…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)