Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna alivyokuja na mpango wa kuhakikisha kwamba tunawekeza sana katika Wizara hii, pia niwapongeze Waziri pamoja na Naibu kwa kazi kubwa ambayo mmeonesha kuanza kuifanya, pia nimpongeze sana Katibu Mkuu Shemdoe kwa kazi ambayo anaendelea kuifanya, akili kubwa aliyoitumia TAMISEMI basi akaendelee kutumia akili kubwa hivyohivyo kwenye Wizara ya Mifugo ili tuweze kupata pato kubwa kutokana na mifugo tuliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema mchango wa mifugo pamoja na uvuvi kwenye Serikali yetu ni asilimia saba ya pato la ndani, asilimia hizi ni chache sana ukilinganisha na idadi ya mifugo tuliyonayo. Ukichukua tu mifugo tuliyonayo inatosha kabisa kutupa pato kubwa ikilinganishwa na pato ambalo tunalipata sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo pia imekuwa ikiongezeka mwaka kila mwaka lakini pato ambalo linachangiwa kutoka kwenye Wizara hii linateremka kila mwaka. Kwa mfano, ukichukua 2016/2017 mchango wa pato ulikuwa asilimia 7.6, ukienda mwaka 2017/2018 asilimia 5.4, ukienda mwaka 2018/2019 asilimia 7.2, ukienda mwaka 2019/2020 asilimia 7.4, 2020/2021 asilimia Saba na 2021/2022 asilimia Saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi kuchangia asilimia Saba peke yake kutokana na mifugo pamoja na uvuvi, tunatamani kuona mwakani mchango wa Wizara hii unafika angalau asilimia 10, asilimia 12 mpaka asilimia 15 tuwekeze kwenye mifugo ni sehemu mojawapo pia ambayo tunaweza kupata rasilimali nyingi za fedha kutokana na Wizara hii ya Mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana Waziri angalia hili ni jambo ambalo tunatakiwa sasa tuwekeze kama ambavyo tumewekeza kwenye kilimo pia tuwekeze kwenye mifugo ili tuweze kupata pato kubwa litokanalo na mifugo. Kama walivyosema wenzangu pia hakuna tutakapokwepa kuwatambua wanyama, haiwezekani tukaacha kuwatambua wanyama halafu tunategemea kuongeza pato katika nchi yetu haitawezekana! Ili tuongeze pato katika nchi yetu ni lazima tuwatambue Wanyama, ni lazima tuwasajili Wanyama, pia ni lazima tuwafuatilie kwa sababu hatutaishia kwenye kuwatambua, unawatambua so what? Hatutaishia kwenye kuwasajili, unawasajili ili iweje? Tunatakiwa twende mbele zaidi kuwafuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta Afisa Mifugo yupo ofisini anaamka asubuhi hajui wala ratiba yake, hajui aende wapi, hajui aende kwa nani, hafahamu! Inatakiwa ifike sasa sehemu Afisa Mifugo akiamka asubuhi anajua kabisa kwamba naenda kwa mfugaji Songe ana ng’ombe 200, naenda kufanya kazi moja, mbili, tatu nne, tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuwape elimu kwa sababu kama watakuwa wanafuga bila elimu, tutafuga ng’ombe 10,000 lakini mwisho wa siku tutaenda kwenye ‘inversely proportional to x’ tulikuwa tunasoma kwenye hesabu miaka fulani hivi kwamba x is inversely proportional to y, yaani kadri speed ya gari inavyoongezeka na muda unapungua. Kwa hiyo, kadri ya ng’ombe wanavyoongezeka wengi na pato nalo linapingua so what? Tunategemea ng’ombe wakiongezeka na pato liongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna muda mwingine lazima tuwasaidie hawa wafugaji, Mheshimiwa Waziri tuangalie sana kuwasaidia wafugaji, Maafisa Mifugo walioko huko wawe na ratiba ya kuwatembelea wafugaji ili wawasaidie, hata hili suala la hereni limefeli kwa sababu mwananchi anasema, so ukinivalishia hereni inakuwaje sasa? Wakipata Elimu mimi nafikiri ni jambo jema lakini kwa sababu hawajapate Elimu hawajui kwamba ukimvalisha heleni ng’ombe wake halafu mwisho wa siku inakuwaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza anatakiwa aambiwe tunataka tuwafahamu lakini pia tunataka tujue eneo hili kuna mifugo mingapi ili tuweze hata kuweza kutengeneza mabwawa kwa ajili ya maji, anajua oooh! Kumbe kutakuwa na faida, anajua kabisa kwamba hata yakitokea magonjwa anakuwa anafahamu kwamba eneo hili kuna ng’ombe kadhaa tupeleke dawa kadhaa, Hiyo ndiyo maana ya kuwatambua ng’ombe wetu ndiyo maana ya kutambua mifugo tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tuangalie, tuje na mpango ili tuweze kuwatambua. Niwaambie Watanzania wenzangu kama tunataka Pato la Taifa liongezeke kutokana na mifugo ni lazima tukubali kuwatambua mifugo, lazima tukubali kuwasajili mifugo, lazima tukubali kuwafuatilia mifugo bila hapo hatutapandisha pato kutokana na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie kidogo kwenye eneo la uvuvi. Mimi kila siku najiuliza kuna hawa watumishi ambao mmepeleka kwenye Wilaya zetu wanaotoka Wizara ya Uvuvi wako chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi ni sawa kabisa, lakini wakienda huko wanakuwa tofauti kabisa na Maafisa Uvuvi walioko kwenye Halmashauri, kila mtu utekelezaji wake anatekeleza tofauti. Huyu akienda huku anakuwa boss huyu akija huku anakuwa boss haiwezekani tukafika kwa stahili hiyo? Mheshimiwa Waziri liangalieni hili kama inawezekana wekeni agency, hawa waliopo Halmashauri waungane na hawa ambao wanatoka Wizarani wafanye kazi moja. Wanakamata watu, ukimuuliza ambae mimi namuuliza kila siku wa Halmashauri anasema sijui, kwa nini asijue wakati wanatekeleza wote sheria moja? Ni lazima wafanye kazi kwa Pamoja, ni lazima wafanye kazi kwa kushirikiana ili tusonge mbele na kuacha kuwanyanyasa wavuvi na kuwakatisha tamaa, tukitaka wavuvi wafanye kazi ni lazima tukubali kuwasaidia. Tukitaka wavuvi waweze kuleta pato katika nchi yetu ni lazima tukubali kuwapa semina, wamefika huko wanafika kukamata hatuwasaidii, nami nitakuwa wa mwisho kujisifu kuongeza pato eti kwa sababu ya faini, nitakuwa wa kwanza kushabikia kupunguza pato kwa sababu watu wametii sheria bila shuruti, hakuna sababu ya kujisifu kwamba tumekusanya hela nyingi zinazotokana na penalty tumekusanya fedha nyingi zinazotokana na faini maana yake makosa yameongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusiwasaidie wavuvi kuwaelimisha badala ya kuwa na makosa mengi wawe na makosa kidogo ili tuweze kuwasaidia, tunawafilisi bila sababu za msingi. Halafu unakuta ana uvuvi haramu na huyu anaenunua nyavu dukani, hazijawahi hata kusikia mwenye duka kafilisiwa, hatujawahi kusikia mwenye kiwanda kafilisiwa lakini anaefilisiwa ni mvuvi kwani hamjui maduka yanayouza nyavu hizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnayajua maduka haya nendeni mkashughulike nao tuwasaidie wavuvi, tuwasaidie watu wa Busega, tuwasidie watu wa Mafia, tuwasaidie watu wa Mwanza ili waweze kuvua wakiwa na amani kuliko sasa hivi kila siku wamekuwa watu wa kukimbia kimbia, nakumbushwa hapa na Kigoma. Mheshimiwa Waziri tulifanye hili ili tuweze kuwasaidia, hamna sababu ya msingi ya kukimbizana na wavuvi, wanakufa humo ndani ya maji kwa sababu ya kukimbizana, tuwasaidie kuwashauri, tuwasaidie kuwapa semina, tuwasaidie kuwapa elimu, ikifika sehemu ya kumpiga faini basi tumpige faini lakini tuanze kwanza kwa kumsaidia huyu mvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni hilo la mikopo kwa vikundi vya wavuvi. Eneo hili na lenyewe lina ukiritimba mwingi bila sababu za msingi. Hebu Mheshimiwa Waziri angalieni hili, watu wa Busega huko wameomba mpaka wamechoka. Sasa wanaopewa hii mikopo ya vikundi ni watu gani tofauti na Watanzania? Tunaomba kama inawezekana, tu – review namna ya upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya wavuvi wetu ili waweze kupata, kwani wameunda vikundi lakini upatikanaji unakuwa mdogo. Upatikanaji wake unakuwa wa kufuatilia, mwisho unafuatilia mpaka nusu ya gharama ya ule mkopo utakaopewa inaisha. Unafuatilia, unafuatilia, bila sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie hili ili tuweze kuwasaidia wananchi hawa, ambao ni wavuvi ili waweze kuleta tija. Tunatamani mwakani akija hapa aseme mapato yamepanda kutoka asilimia saba ya mchango wa Wizara yake, imefika asilimia 10. Mimi nitakuwa wa kwanza kupiga makofi na wa kwanza kwenda kumpongeza nyumbani kwake, kwa sababu tutakuwa tumeona kweli amedhamiria kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)