Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kunukuu kupitia Karl Marx na Engels wote wanakubaliana kwamba, naomba kunukuu kwamba “Despite the capitalist economy, the economic modes of production define the class structure of the society.” Pamoja na kwamba na mfumo wa kibepari lakini mfumo uliopo wa kiuchumi katika jamii fulani unatoa madaraja ya jamii ile kwamba namna gani ilivyokaa katika uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika nchi yetu tukiweza kuwapanga wafugaji kwenye mfumo wetu wa uzalishaji na mfumo wetu wa uchumi, wafugaji ndiyo wanaotokana katika daraja la mwisho zaidi la uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua kigezo kwamba mfugaji hakopesheki kwenye mabenki na tukianza na wafanyabiashara wakubwa wenye viwanda wanakopesheka kwenye mabenki. Wafanyabiashara wa kawaida wachuuzi wanakopesheka kwenye mabenki lakini siku hizi tumeweka na wajasiriamali na wamachinga humo humo wanakopesheka kwa kiasi fulani kwenye mabenki. Wanakuja wakulima wanakopesheka kwenye mabenki lakini mtu ambaye hakopesheki kwa sababu ya kutokuwa na anwani ni mfugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kwamba tu lakini ni namna gani sisi wenyewe tumemtengenezea mfugaji asiaminike, mfugaji asikopesheke na mfugaji asiwe na anwani. Nataka kusema kwamba nchi yetu tuna mifugo mingi na tuna wafugaji wengi lakini kwenye uzalishaji bado hatambulilki katika mfumo wa kiuzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Serikali ilikuja na utaratibu wa utambuzi wa mifugo ile inaitwa Ear tag Electronic System. Mfumo huu umefanikiwa sana katika Nchi ya Botswana kwamba mifugo inavyozaliwa baada ya miezi mitatu anapewa electronic tag na ile electronic tag inakuwa na habari mbalimbali. Aina ya mifugo, inamilikiwa na nani lakini vilevile kwa ajili ya kupata dawa, traceability na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosababisha wafugaji wetu wasiweze kukopesheka ataenda benki anataka kukopa lakini benki wanataka wajue ana mifugo kiasi gani? Sasa mifugo kiasi gani ni lazima kuwe na mfumo ambao unatambua kwamba ana mifugo kiasi gani ambayo imethibitishwa na mfumo halali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mfugaji huyu akienda kutaka kukopa baada ya siku mbili, tatu anahama kutoka Shinyanga anaenda Mtwara kwa hiyo hata benki haiwezi kumkopesha. Kwa hiyo, nilichotaka kusema ni kwamba Serikali mfumo huu ni lazima kama ilivyousitisha iurejeshe. Jambo la msingi Serikali iongeze ruzuku kwenye zoezi ili kwamba wafugaji wetu waweze kusajili mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni zuri kwamba Serikali itakuwa inapata mapato kwa sababu mfugaji anavyoenda kuuza inawezekana kukawa kuna namna gani anaweza kuchangia katika kulipia ushuru mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, jambo hili limezungumzwa kwamba katika mwaka 2025 kutakuwa na utambuzi wa mifugo. Kwa hiyo, jambo hili lipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kwa dhati niipongeze Wizara ya Mifugo. Wizara hii imekuwa haipati fedha za kutosha. Bajeti ya mwaka huu ina bilioni 290 tu, ambayo ni kidogo sana. Ukienda Taasisi ya Utafiti wa Mifugo TALIRI ina fedha haizidi bilioni moja; yaani taasisi ya kufanya utafiti wa mifugo haipati fedha, hata bilioni moja haifiki. Kwa hiyo naomba Serikali iangalie sana, kwamba sekta hii ya mifugo iweze kutoa fedha. Na nataka niipongeze Wizara hii, imefanya kazi kubwa ambazo pamoja na kupata hela kidogo lakini wameonesha uwezo mkubwa wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kinachowaangusha wafugaji wetu ni kwamba maeneo ya malisho hayajapimwa, na tukiri kwamba Wizara ya Ardhi ina sura ya Wizara ya migogoro ya ardhi, si Wizara ya kupima maeneo. Sasa kama inawezekana itengenezwe mamlaka kwa ajili ya upimaji wa maeneo ya mifugo, mamlaka ambayo itashirikisha kati ya Wizara ya Mifugo na Wizara ya Ardhi ili kwamba wafugaji wetu waweze kupimiwa maeneo na waweze kuweza kulisha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie jambo hili limeshuka hata maeneo yetu tunayokaa; wafugaji wanaishi kwa kutangatanga. Njia ya wafugaji kiasili zilikuwepo tangu zamani, siku hizi watu wanaamua kulima hata njia za wafugaji, tunaita mapalio, hamna mapalio sasa, kwa hiyo mfugaji anaishi kwa kutangatanga, naomba jambo hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu suala la majosho na maji, mabwawa, malambo, jambo hili nalo liangaliwe. Mimi Kata yangu ya Chifutuka ina ng’ombe zaidi ya 2,500 lakini hakuna sehemu ambapo mifugo inaenda kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongea sekta hii lakini hii ni sekta ambayo kwa kiasi kikubwa tumeitelekeza. Bado tunachukulia kwamba mfugaji ni mtu ambaye yuko kienyeji na Serikali bado haijaangalia suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, kwanza kwa kuanza kiufufua Ranch ya Kongwa na mwaka jana kulikuwa na tatizo la kutaka kuibadilisha ranchi yawe mashamba ya alizeti. Kwa vitendo amefanya, amepeleka matrekta matano, amepeleka ng’ombe 1000 kwa hiyo huko ndiko tunakoelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri na nataka niseme nchi yetu ina utajiri mkubwa wa mifugo, masoko yameshafunguka sasa, kama vile Saudi Arabia, Vietnam na kwingineko, tutumie fursa hii. Ng’ombe wa Tanzania walikuwa hawauziki kwa sababu hatuna traceability, kwamba huyu ng’ombe ametibiwa haijulikani, na ndiyo maana wenzetu wanaangalia namna gani nyama yetu inavyokuwa. Kwa hiyo tayari tuko katika nafasi nzuri kuendelee kuipatia fedha Wizara hii ili iweze kujiendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu migororo ya wafugaji na hifadhi zetu. Mimi wiki iliyopita ng’ombe 191 walikamatwa wameingia kwenye hifadhi, na bahati mbaya walivyokamatwa inatakiwa ng’ombe mmoja alipiwe laki moja. Sasa utaona kiasi gani mkulima huyu mfugaji anaweza kutoa. Lakini chanzo cha kwenda kwenye hifadhi ni nini? chanzo cha kwenda kwenye hifadhi ni kutafuta malisho. Kwa hiyo Serikali iangalie, kama nilivyosema mwanzo, namna gani inaweza kudhibiti tatizo hili la wafugaji kupeleka ng’ombe kwenye hifadhi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana.