Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja hii ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo. Napongeza kazi kubwa iliyofanyika na Wizara hii, wametuletea bajeti nzuri na kutuonyesha maeneo muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kama kuna maeneo Tanzania hatutajutia kuwekeza maeneo yenye risk ndogo, basi ni Sekta ya Mifugo. Ukiwekeza katika Sekta ya Mifugo siku zote ujue kwamba risk ni ndogo unaenda kuwekeza na unapata faida ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa mfano, tukanunua meli tukafanya Uvuvi wa Bahari Kuu, si tunanunua, tunavua, tuna- export Samaki, tunapata kipato au tukaamua kunenepesha mifugo, tunanenepesha tunawauza tunapata fedha. Kwa hiyo Sekta ya Mifugo ni sekta ya kuleta uchumi, lakini ni sekta ambayo tukiwekeza hatutajutia. Mheshimiwa Waziri ametuonyesha maeneo ya kuwekeza katika sekta hii ili kuweza kuleta mapinduzi makubwa katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji transformation katika Sekta hii ya Mifugo, lakini sasa sijui kwa nini anafanya vidogo vidogo, pengine na bajeti hii ni ndogo, maana na bajeti ametengewa bilioni 295.9. Kwa mfano, ameeleza kabisa kwamba, tija ni ndogo kutokana na mifugo. Tunaona kwamba pato la Taifa bado limebaki kuwa kwa asilimia saba na sekta inakua kwa asilimia kidogo na tija ni ndogo, tumeona sababu mbalimbali, lakini mojawapo ni hili la kwamba aina ya mifugo yetu tuliyonayo hata tungefanya nini bado watakuja na tija ndogo. Aina ya mifugo tuliyonayo ambayo ni mbari za mifugo na kosafu. Kila siku nazisema, hata ungemlisha ng’ombe wa kienyeji namna gani, bado utakamua nusu lita mpaka lita mbili ya maziwa. Tunahitaji kubadilisha aina hii ya kosafu za mifugo yetu, hata ukimlisha namna gani ng’ombe huyu wa kienyeji ataishia kwenye kilo mia, mia na hamsini hazidi mia mbili, hata huwezi kumchagua kwenda kunenepesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naona mpango wa Waziri hapa ni kufanya uhamilishaji katika kubadilisha kosafu za mifugo, lakini analenga mifugo laki moja tu, sasa najaribu kuona kwa nini laki moja tu? Laki moja ni kidogo sana, tena na anataka kufanya katika mikoa 26 ya Tanzania. Ukilinganisha na mifugo tuliyonayo milioni 36, laki moja ni wachache na trend ya uhamilishaji naona inazidi kushuka, sijaelewa ni kwa sababu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu imeonesha kwenye jedwali la Waziri mwaka 2019/2020 alihamilisha mifugo elfu sitini na saba na pointi. Mwaka 2021 alihamilisha ng’ombe 77, lakini mwaka uliopita alihamilisha ng’ombe 60,600. Sasa trend ya Waziri inazidi kushuka. Nafikiri kuliko kutawanya hizi nguvu ndogo katika mikoa yote 26, ni kwa nini wasifanye kampeni, akafanya uhamilishwaji kwenye mikoa miwili au mitatu wakaboresha mifugo ya pale, kwa sababu kuboresha mifugo ni kumbadilisha mfugaji kwenye mitazamo yake. Tukambadilisha mfugaji akaona ubora na wafugaji wenyewe wataazimana, akiona sehemu ambayo mifugo imekuwa bora, wataazimana mbegu, wataazimana madume. Kwa hiyo hili ni muhimu sana na hii ni pointi ya kuleta transformation katika ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema tu kwamba mifugo imeongezeka, kuna mmoja amesema mifugo ni kero, mimi sitaki kusema mifugo ni kero. Mifugo ni benki kwa wafugaji, lakini tujue tu kwamba Tanzania ardhi yetu ni ile ile tuliyopewa na Mungu na sisi tunaongezeka na nyanda za malisho haya ndiyo hizi hizi kila siku zinasogezwa zinakuwa maeneo ya kilimo, ndiyo hizi tunaendeleza maeneo ya makazi na zinazidi kupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukisema tu kwamba tuko proud pengine na mifugo kuongeza ni nzuri na nakubaliana, lakini bado haijawa mifugo yenye tija na sababu ndiyo hizi hizi. Kwa hiyo kuwabadilisha mitazamo wafugaji ni muhimu, wanatakiwa kuona kwamba watoke kwenye mifugo hii ya kienyeji ambacho kipato chake ni kidogo, waende kwenye dume ambalo wataliona ni zaidi ya kilo mia nne au mia sita kama wanavyoweza kuiona Nane Nane ndiyo watabadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo efforts ziongezwe kwenye uhamilishaji kubadilisha kosafu za mifugo, hili ni muhimu sana na nalirudia, lakini pia Waziri ameeleza kwamba atanunua madume 200, sasa madume 200 ni wachache sana. Haya madume 200 kama atagawa tena kwenye mikoa 26, ina maana kila mkoa utaenda na madume saba saba. Hata kama ni Manyara ina maana kila Mbunge ataondoka na dume moja, sasa kweli mpaka hii mbegu ienee ni leo? Hawa wafugaji wakiweza kuwaelekeza ni wapi madume bora wanapatikana na wakawapelekea watakuwa tayari wao wenyewe kuwanunua at least kubadilisha. Pia nimeona kwamba Waziri anaongeza mitamba 1,200, nami natamani Mradi wa Ng’ombe wa Maziwa ungewasaidia sana akinamama waweze kusambazwa, wauze maziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mwenyewe umetoa kibali cha kuingiza maziwa kwa kipindi kilichopita lita milioni 11.6 kwa fedha za Kitanzania bilioni 22. Hii inaonyesha kabisa tu kwamba uzalishaji wa maziwa katika nchi yetu ni mdogo na ndiyo maana tuna-import maziwa, ya kwetu yenyewe hayatoshi kwenye viwanda vya usindikaji, lakini tuna fursa kubwa sana ya kuzalisha maziwa ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mtanzania unatakiwa unywe maziwa hata lita 200 kwa mwaka, lakini tunakunywa chini ya kiwango na watoto wetu wanapata udumavu, ujue Tanzania nayo iko kwenye orodha ya udumavu. Tunapaswa kuongeza uzalishaji kwa kuleta madume bora, mitamba bora, lakini pia kwa kufanya uhamilishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni kwamba changamoto nyingine iliyoko kwenye mifugo ni hii ya magonjwa. Magonjwa ni mojawapo ya sababu inayorudisha nyuma Sekta hii ya Mifugo. Tunashindwa kuuza mifugo yetu nje kwa sababu wanahitaji kujua background, hii mifugo iliwahi kuugua labda magonjwa ya mdomo na miguu (FMD) na vitu vingine. Mifugo inayoumwa siku zote quality yake ni ndogo, nyama yake ni ndogo, maziwa yake ni kidogo. Sasa inatakiwa kukomesha kabisa au kupunguza magonjwa haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea kabisa tu kwamba wataalam hatuna. Kwa mfano, kwenye wilaya nzima hatuna Madaktari wa Mifugo, wale wa veterinary per se, kuna kada za mifugo huko ziko za Animal Production, Range Management na zingine, lakini hawa wa veterinary hawapo. Ndiyo maana wafugaji wetu siku zote wanapata shida. Nimeona wafugaji wakihangaika kutibu mifugo yao wenyewe, yaani kwa ugonjwa mmoja mfugaji anatumia uzoefu wake, atatumia aina tatu za dawa, atanunua oxytetracycline (OTC), penicillin, sijui gentamicin zote anakwenda kumdunga ng’ombe mmoja kwa dozi anayoijua kwa sababu hana sehemu ya kupata utaalamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeua Veterinary Centers, hata kama haiwezekana kwenye kata, hizi Veterinary Centers ziwepo basi kwenye halmashauri ili tuweze kuchunguza magonjwa hasa ya mlipuko. Ugonjwa wa mlipuko ukitokea katika halmashauri mpaka sample ipelekwe mkoani na ilete majibu ndiyo ianze kushughulikiwa, hebu tuboreshe kwa sababu tatizo limekuwa kubwa. Kwa sababu wataalam hawa ni wachache kwa nini Wizara sasa isifikirie kuwafundisha ma-para professional wengine kwa kila kijiji ili waendelee kusaidia wafugaji, wasiendelee kuhangaika na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili la majosho ili kuweza kupunguza magonjwa ya mifugo. Nampongeza ameweza kujenga majosho ya kutosha na kuwa na majosho ni jambo jema, naomba aongeze majosho kwa sababu ng’ombe hawatakiwi kutembea mbali na maeneo yote ni mashamba, ingewezekana hata kila kijiji kikawa na josho kama siyo kila kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu majosho kuwepo ni jambo moja bado matumizi ya josho hayajawa mazuri, majosho yapo lakini watu hawaogeshi, naomba Mheshimiwa Waziri afanye utafiti tatizo ni nini? Wakipewa dawa ya ruzuku pengine kwa mara ya kwanza wataogesha, baadae wanaacha kwa sababu kuogesha ni kwenye majosho na majosho ndiyo namna nzuri ya kuweza kupambana na magonjwa ya kupe, tujue sababu ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo sheria lakini sheria zetu zimekaa kwenye vitabu, mara pengine ni vizuri kutumia sheria kuogesha ili watu wakaogeshe mifugo, kwa sababu kama nyumba moja inaogesha nyingne haiogeshi na sehemu ya malisho ni moja bado mzunguko wa kupe utaendela kuwepo pale, kwa hiyo hilo mimi naomba uliangalie.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine labda ni ubora wa madawa. Hebu tuangalie ubora wa madawa, kwa sababu mifugo hii inaogeshwa ile ratio ya dawa ya kuogesha hii, unaweza ukasema CC Mbili labda kwenye lita moja ya maji, lakini unaogesha ng’ombe au unampeleka kwenye deep anatoka pale bado ana kupe. Tujue tatizo ni nini? Ndiyo maana ukiona kwenye dawa pengine maelekezo ni kuchoma CC 10 kwa ng’ombe, wafugaji wananchoma mpaka 20 na 30 kwa sababu akichoma hiyo 10 kama ilivyo kwenye maelekezo anaona ugonjwa huo hautibiki. Pengine kuna uchakachuaji kwenye madawa haya ya mifugo naomba ufatilie.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Yustina.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga hoja mkono. (Makofi)