Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Awali ya yote, nianze pia na mimi kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Abdallah Ulega, kijana mwenzetu na uzuri namfahamu, alikuwa Youth League, ni committed person, very humble, understanding; kwa hiyo, naamnini hapa Wizara imepata mtu sahihi pamoja Naibu wake. Ni kwamba tunakwenda kutekeleza hivi vitu tunavyovizungumza ambavyo tumeviona kwenye hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata Katibu Mkuu wa Wizara hii, Profesa, tunatarajia tuone mambo mazuri ya kisomi, ya kitaalamu na wayashushe mpaka kule chini ambako wanatukuta sisi wafugaji ambao hatujui kusoma wala kuandika. Kwa hiyo, watafute namna sasa, kutumia elimu zao hizi nzuri waweze ku-match na sisi wanakijiji ili tuweze kwenda sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu ku-declare interest, mimi ni mtoto wa mfugaji, nimesoma kwa kutumia mifugo hii. Kwa hiyo, ni sekta muhimu ambayo kimsingi namwomba sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, waitazame kwa jicho la karibu, watumie nafasi ambazo wamepewa na Mheshimiwa Rais, amewaamini vizuri, nasi tuna imaninao kubwa, kuhakikisha hii Wizara inakuwa na tija kwenye pato la Taifa letu na hasa wananchi walioko kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuzungumzia masuala machache ya jimboni kwangu yanayohusu sekta hii, halafu nitazungumza mambo ya jumla ya kitaifa. Kwenye eneo la malisho pamoja na majosho, hasa majosho; kwa kule jimboni kwangu ninashukuru nilipata miradi katika ule mwaka wa fedha unaoisha, majosho manne katika Kijiji cha Muaghamo, Mangida, Minyenye na Makuro. Kwa masikitiko makubwa, hii miradi haikuweza kutekelezeka kwa sababu ya ule utaratibu wa Wizara, kwamba, wanakuwa na zile fedha, mpaka waone josho limetengenezwa na wakandarasi. Wakandarasi watengeneze kwa kutumia nguvu zao, ndipo waje walipwe. Sasa huu utaratibu umekuwa siyo mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri utaratibu huu, ingekuwa wanapeleka Halmashauri kwa sababu Halmashauri tunazo kila eneo na ni Government entity inayosimamia mambo haya na tunaiamini. Kwa hiyo, fedha hizi ziende pale ili wale wakandarasi waweze kupewa wafanye kazi kuliko kuzi-own huku juu, utaratibu unakuwa ni mrefu na mgumu, na siyo rahisi kufikika. Naomba huu utaratibu urahisisishwe ili nipate haya majosho manne ambayo ilikuwa niyapate. Pia, nashukuru kwa miradi ya majosho mengine manne ambayo naenda kupata kwa mwaka huu unaokuja wa fedha katika Kijiji cha Mukulu, Unyampanda, Ughandi na Mughunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye zile center atamizi. Ofisi ya Waziri Mkuu walikuja wakati ikiwa chini ya Wizara hii ya Mifugo. Ni kwamba, wangetuletea center kwa ajili ya kituo atamizi kwenye Kijiji changu kimoja cha Nkwaye, lakini mpaka sasa sijaona kinachoendelea. Center hii ingekuwa ni nzuri kwa vijana, kwa ajili ya kurithisha mafunzo mazuri, endelevu ya kisasa kwa wenzao wengine. Sasa sijaona kinachoendelea. Naiomba sasa Wizara walichukue hili, ili nione sasa kile kituo cha ufugaji bora utekelezaji ufanyike ili vijana wetu waweze kupata hii elimu, waweze kuwapa na wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu biashara hii inayofanyika ya ng’ombe. Wafanyabiashara wengi walikuwa wanapata leseni na vibali vile vya kusafirishia mifugo kule kule wilayani na wakati mwingine mkoani, lakini sasa hivi Wizara imelimiliki hili zoezi, wafanyabiashara mpaka waje Wizarani. Sasa inawapa taabu, kwa hiyo, ufanyaji wa biashara ya mifugo umekuwa ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, naomba Wizara ibadilishe huu utaratibu ambao upo hivi sasa, irudi kwenye ule utaratibu uliokuwa wa mwanzo, uliokuwa unawawezesha wafanyabiashara wetu wa mifugo ku-access hizi leseni kwenye maeneo yao kuliko kuwapa taabu ya kuwafuata watendaji wetu huku Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la muhimu sasa kwenye sekta hii, katika sekta za muhimu katika nchi yetu huwezi kuiondoa mifugo, huwezi kuondoa uvuvi pamoja na kilimo. Hizi ni production sectors ambazo ndiyo zinatakiwa ziwe sekta za msingi za uzalishaji na zitazamwe kwa jicho la karibu kwa ajili ya kumsaidia Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nchi hii nimeitembea kidogo, kuanzia Bukoba, nimeenda mpaka Zanzibar. Katikati hapo ukipita huwezi kuacha kuona mfugo. Ukianzia Mbeya mpaka uende Arusha, huwezi kuacha kuona mfugo. Sikitiko langu kubwa ni kwenye eneo la bidhaa za mifugo, tumezipuuza. Hakuna viwanda. Hakuna kiwanda cha nyama, wala kiwanda cha maziwa. Vipo vichache. Kwanza tulikuwa na viwanda vile vya zamani; kulikuwa na Tanganyika Packers ambayo leo inatumika kwenye mahubiri. Hivi kweli tunaweza tukafika kwenye point hii ya kuidhalilisha sekta hii ambayo inawasaidia wananchi wa Tanzania zaidi ya milioni 60 leo? Tunaacha mifugo inateseka, ngozi inatupwa. Eti leo sisi tuna- export ngozi kwenda kuliwa Nigeria na Ghana. Ndiyo tumefilisika kwa kiwango hiki! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, watendaji wa Wizara hii pamoja na Serikali, twende tukamkomboe mwananchi wa Tanzania kwa kutumia hii sekta ya mifugo. Nasikitika eti leo naambiwa ni asilimia saba sijui tano, kwenye pato la Taifa ndiyo inatokana na mifugo. This is joking! Hapa tunatania, hatujawa serious bado. Naomba sana, turudi kwenye viwanda vile vilivyokuwepo vya kusindika nyama. Nakumbuka tulikula nyama ya kopo wakati huo, lakini leo hakuna. Nyama ikikaa siku mbili buchani, unakuta imeharibika, ndiyo tunaumwa matumbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tungekuwa tunaweza kuweka viwanda vile vya ku-process nyama, iwekwe kwenye kopo; maziwa, products za ng’ombe, za mifugo; leo hii tungeongeza thamani ya mifugo yetu, tungeingiza pato kubwa la Taifa kwa kupitia mifugo hii. Hata Singida tulikuwa tuna kiwanda cha kusindika nyama ya ng’ombe. Leo hii naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kusimama uniambie, kiwanda cha ng’ombe Singida, status yake ikoje? Naomba hiki kiwanda kirudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sisi tunafuga; tuna ng’ombe wa kutosha, central zone hii kwa ujumla wake tuna mifugo ya kutosha; Shinyanga, na kadhalika, tuweke kiwanda pale Singida cha ng’ombe na mbuzi ili tuweze kuinua kipato cha Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu sana, ni eneo la malisho ya mifugo. Katika eneo ambalo hatujaitendea haki kabisa sekta hii ya mifugo ni eneo la malisho. Naomba sana, tuache kuwadhalilisha wafugaji wetu. Kwa kuwa, tumeshaona wananchi wetu wengi ni wafugaji, nasi tupo kwenye kutengeneza sera na mifumo, tuwatengenezee utaratibu mzuri wa malisho. Majani haya ambayo tumesema ni ya malisho ya mifugo yetu, tuyapeleke mashamba darasa kwenye kila Kijiji, kwenye kila kata. Kwa nini myaache huko Dar es Salaam au Dodoma? Wafugaji hawako Dar es Salaam. Wafugaji na wakulima wako vijijini, tuwafuate waliko tuwapelekee hii huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi suti tuzipeleke kule vijijini ili tukaishi maisha wanayoishi wenzetu kule chini kwenye grassroot. Tutawatendea haki, wakulima wetu wataacha kumangamanga, kutafuta malisho huku na kule. Kila siku tunaona migogoro ya wakulima na wafugaji, haitaisha kama hatujaweza kuwapa wafugaji wetu malisho huko kwenye maeneo yao. Yale maeneo ambayo yalipimwa, Mheshimiwa Waziri mlipima maeneo, mliyarasimisha maeneo vizuri kule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ninayo mambo mengi hapa nitayawasilisha mengine kwa maandishi, lakini naomba sana haya ambayo nimeyazungumza yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)