Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru wewe kwa kunipa hii fursa ya kuchangia. Kipekee sana, niungane na Waheshimiwa
Wabunge wote waliompongeza sana Mheshimiwa Waziri Ulega kwa hotuba yake ambayo imejaa mikakati mingi na mizuri ambayo imekusudia kuikomboa Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi. Vile vile namshukuru na kumpongeza sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde na Katibu Mkuu, Mheshimiwa Profesa Shemdoe kwa ushirikiano wao mkubwa ambao wanautoa kwa wadau wa sekta hii na kwa maandalizi ya taarifa makini na yenye mikakati mizuri na mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba, moja katika mipango au mikakati iliyopo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kuzalisha au kutengeneza ajira milioni nane, kuanzia mwanzo wa Bunge hili mpaka mwisho wa Bunge hili. Mwanzo wa uhai wa Bunge hili mpaka mwisho wa uhai wa Bunge hili, tunatakiwa tuwe tumeisaidia Serikali kutengeneza ajira milioni nane kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo sekta mama mbili ambazo zinaweza kutengeneza ajira hizo milioni nane au zaidi iwapo Serikali itatusikiliza Wabunge, na iwapo Serikali itapeleka kipaumbele kwa mujibu wa ushauri wa Wabunge. Wabunge humu ndani wameeleza mara nyingi, moja katika sekta muhimu ambazo zitapunguza mlundikano wa watu waliokosa ajira, sekta ambazo zitatuwezesha kupata ajira milioni nane, ni Sekta ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mikakati kwenye kilimo, mikakati mizuri ambayo inawapeleka vijana kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo. Kwa upande wa Mheshimiwa Ulega tumeona mikakati yake ya kutupeleka na kuwapeleka vijana wa Kitanzania wakawekeze kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Umewasikiliza Waheshimiwa Wabunge humu, wameeleza mahitaji ya nyama na mazao mengine ya mifugo ndani ya nchi na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale Wabunge ambao wametembelea nchi mbalimbali zikiwemo Ulaya, nchi za Magharibi, waliotembelea nchi za Uarabuni, kote huko wamekiri ndani ya Bunge lako Tukufu Sekta ya Nyama ingeweza kulikomboa Taifa hili. Mahitaji ya nyama nchi za Uarabuni ni kubwa kuliko ambavyo sisi tunaweza kupelea. Nchi yetu imekaa kijiografia, imekaa eneo la kimkakati sana. Kusafirisha ng’ombe walio hai au nyama zenye sifa kupeleka nchi za Uarabuni, kupeleka Comoro ni rahisi kuliko nchi yoyote Afrika ambayo ingeweza kufanya jukumu hilo. Leo tuna maelfu ya Watanzania hawana ajira kwa sababu hatujaamua kuwekeza kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi, pamoja na Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi nyingi ambazo zimejenga uchumi wao kwa kutumia Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Nenda Marekani mkaangalie ni asilimia ngapi ya uwekezaji unapelekwa kwenye ufugaji? Leo sisi tulishwe na nchi za Amerika ya Kusini nyama. Fikiria kusafirisha nyama toka Brazil kupeleka Uarabuni na kusafirisha nyama kutoka Tanzania kupeleka Uarabuni, nani anatengeneza faida kubwa zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe, na niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuongeze nguvu kwenye hii sekta. Nasikitika simwoni Waziri wa Fedha hapa. Waziri wa Fedha apeleke fedha Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Tuahirishe mambo mengine ambayo hayana tija, tupeleke fedha kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Nimeitazama mikakati ya Mheshimiwa Waziri hapa, moja katika mikakati mahususi ni uzalishaji wa malisho na ambari kwa maana ya mbegu bora za mifugo. (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Mheshimiwa Naibu Waziri.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangia hoja na Bunge lako kwamba kuna kikao cha Baraza la Mawaziri kinachoendelea sasa, ndiyo maana Mawaziri almost karibu wote hawaonekani Bungeni hapa, lakini pia yupo Naibu Waziri wa Fedha. Kwa hiyo, anaposema jambo Wizara ya Fedha, maana yake Naibu Waziri yupo, atalichukua na tutakwenda kulifanyia kazi kama Serikali. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mhagama, unaipokea taarifa?

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ninaipokea taarifa ya Mheshimiwa Naibu Waziri, na ninatambua kwamba Serikali ipo humu ndani na inasikia na ninaomba inisikilize kwamba hakuna mapinduzi ya uchumi tutayapata Tanzania kama hatupeleki fedha kwenye mifugo na uvuvi. Mikakati ya Mheshimiwa Waziri ni bayana, ipo very clear, kwamba anahitaji kufanya transformation kwenye Sekta ya Mifugo. Kuna eneo la malisho, kuna eneo la mbegu bora. Ukiangalia takwimu alizozileta Mheshimiwa Waziri, haziendi kujibu tatizo. Mheshimiwa Waziri amependekeza kuzalisha malisho hekta 11,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hekta 11,000 ni sawa sawa na tani 55,000 za malisho kwa maana ya hay. Hizi unalisha ng’ombe 25,000 tu kwa mwaka. Tanzania tuna ng’ombe milioni 36,000. Unaona kwamba Waziri ana hamu ya kusonga mbele lakini sisi Serikali tunamkamata miguu. Kwenye hili nimshauri Mheshimiwa Waziri, kwa sababu tunaanza, aachane na biashara ya kwenda kuzalisha hay yeye mwenyewe, isipokuwa fedha hii akaiwekeze kwenye kuzalisha mbegu za malisho. Akazalishe mbegu za malisho hekta 11,000 tupate mbegu za kutosha. Hizi mbegu tuwawezeshe sekta binafsi kuzalisha malisho wao wenyewe. Kwa sababu hizo hekta 11,000 utaenda kutatua tatizo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu, tuanzie hapo. Peleka hii fedha ambayo utapata kwenye hekta 11,000, peleka kwenye mbegu za malisho. Tumefanya kwenye mahindi, tumefanya kwenye maharage, tumefanya kwenye mazao ya kilimo; tumewekeza kwenye uzalishaji wa mbegu, Serikali ihakikishe tunapata mbegu, lakini sekta binafsi ndiyo izalishe, ifanye multiplication ya hizo mbegu. Kwa hiyo, namwomba sana Waziri, hii fedha atakayoipata aipeleke kwenye kuzalisha mbegu. Tuna mahitaji makubwa sana ya mbegu ya brachiaria, haipo nchini, lakini katika mbegu nzuri sana, hay nzuri sana utaipata kwenye brachiaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shida ya setaria, nimeenda mpaka hapo Iringa, hakuna. Kwa miaka mitatu unasubiri kupata kilo 200 za mbegu. Imagine, nchi hii tupo nyuma sana. Miaka mitatu, minne bado unasubiri upate supply ya mbegu toka kwenye mashamba ya Serikali. Hatuwezi kufanya mapinduzi ya mifugo kama hatutathubutu kuwekeza vizuri kwenye uzalishaji wa mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cenchrus ni mbengu ambayo inafanya vizuri sana hapa Dodoma, lakini nchi hii kuna maeneo mengi yanakuwa makame kama ilivyo Dodoma. Hakuna utafiti uliofanyika Mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine kuhakikisha kwamba hii cenchrus ambayo ni resistance kwa mazingira, inaweza ikafanya vizuri kwa maeneo hayo. Mheshimiwa ilete ukaiwekeze huko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mhagama, muda wako umeisha, naomba umalizie.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilikuwa na mchango kwenye maeneo mengine ya miundombinu na masuala ya chanjo, lakini nitapeleka kwa Mheshimiwa Waziri kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)