Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kupata nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri. Nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa uteuzi wao katika nafasi hiyo nyeti sana katika uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Mawaziri nawaamini na hii nafasi waliyopewa ni nafasi yao kubwa sana katika icon ya nchi hii lakini nawapa pole pia kwa nafasi hii kwa sababu wengi wamepita sana katika Wizara hii baada ya kutokuitendea haki. Naamini safari hii Mheshimiwa Ulega kwa sababu alikuwa ni mchezaji wa akiba yaani Naibu Waziri kwa Mawaziri wawili waliopita sasa leo amepewa zigo hili yeye mwenyewe. Ninaimani atalitendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya wavuvi, matatizo ya wafugaji, Mheshimiwa Ulega anayajua lakini ni watoto wa wavuvi na mmoja yule ni mtoto wa mfugaji; Mheshimiwa Silinde. Kwa hiyo ninaamini watatenda haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja katika suala la hereni, suala la hereni hili limekuwa ni tatizo katika nchi hii. Wajikite sana katika kuleta sera ya namna gani tutaweza kuboresha mifugo yetu wakaacha kupambana na wafugaji kuhusiana na suala la hereni. Huu ni ulaji tu wa watu wametengeneza wajamaa wakaleta hapa wanataka kuja kusumbua nchi na hili litaleta hatari kubwa sana.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jackson Kiswaga taarifa.

TAARIFA

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru mchangiaji anachangia vizuri lakini napenda nimpe taarifa kwamba katika nchi hii inasemekana kwenye mapori yetu kuna mifugo mingi sana ambayo siyo ya kwetu. Hereni ina nia nzuri kabisa ya kutaka kutambua mifugo tuliyonayo nchi hii kwamba ni mingapi na ni ya nani? Hakuna upigaji hapo. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Tabasam taarifa unaipokea?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, haina nafasi ya kukubaliwa. Huyo ni mchana mbao hawezi kujua habari ya ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamuona anaondoka na kuondoka kwa sababu ni mchana mbao. Naomba uendelee kunipa nafasi ni kwamba kama ni nchi huru ambayo tayari inalindwa na mipaka yake na Mheshimiwa Rais kishaapa kwamba atalinda wananchi, atalinda nchi na mipaka yake, hao ng’ombe wamepitia wapi? Haya ni maneno ya watu wapigaji baba. Njaa inasumbua sana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuja kuharibu heshima ya nchi yetu sisi kama ng’ombe wanajulikana, wananchi wanajulikana wafugaji wa ng’ombe, Tabasam ana ng’ombe kadhaa, kule chini tuna mabalozi, tuna Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Wajumbe. Hakuna mtu ambaye hajui ng’ombe wa fulani wako kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata buchani ukienda huwezi ukakuta ng’ombe yaani katika label ya ng’ombe pale buchani mguu unawekwa ulionona. Hatujawahi kuona kichwa kimewekwa kina hereni kuonesha kwamba ng’ombe unayenunua nyama hii ina hereni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja na mpango wa kuzalisha majani. Huu mpango wa kuzalisha majani Mheshimiwa Waziri usiupeleke tu kwenye mashamba yenu. Huu iwe ni Sera ya Serikali kila mfugaji awe na shamba la ekari moja au mbili na tuleteeni mbegu. Kama Serikali imeweza kwenda kupeleka ruzuku katika mbolea, haiwezi Serikali kushindwa kuleta ruzuku ya majani. Kwa sababu majani yale watu wakishaona faida yake, tayari watu wataendelea kulisha mifugo yao bila hata wasi wasi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litapunguza habari ya kusafirisha ng’ombe kuwatoa Sengerema kuwapeleka Mtwara, kuwatoa Sengerema kuwapeleka Mbeya. Sisi tutabaki na ng’ombe wetu kwa sababu tayari tumeshafundishwa namna ya kufuga kisasa. Haya masuala mbona yanawezekana? Unao wataalamu, wataalamu tunao mpaka ngazi za wilaya. Tutengenezeeni sera nzuri, wafugaji tuwe huru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya kutuletea habari ya muda wote tukifikiria hereni, kesho chanjo, kesho chanjo ya miguu, chanjo ya midomo na bado tena mtatuletea zigo jingine la hereni, hili haliwezi kukubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu nina malambo. Mimi nina malambo ambayo yamepasuka na haya malambo umekuja kuyaona wewe mwenyewe ukiwa Naibu Waziri na leo wewe ni Waziri. Sasa Mheshimiwa hivi tunavyozungumza hili jambo la Mheshimiwa Waziri la malambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Lambo mimi la Nyanchenche unajua lina kata tatu. Nina Lambo la Bitoto, hili Lambo la Bitoto Mheshimiwa Ngeleja lilimuondoa kwa sababu ndiyo nyumbani kwao. Sasa siwezi kukubali niondolewe na Wananchi wa Bitoto. Malambo yako tisa, haya malambo sisi kwetu ni kitu adimu, kitu cha thamani sana. Nakuomba Lambo la Nyanchenche umekwenda umeona, Lambo la Kishinda, Bitoto, Nyampande, Kasungamile, Buzirasoga, Sima. Haya malambo yote yamepasuka. Lambo liko Nyamizeze, ndugu yangu nisaidie sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ni kwamba miradi yenu yote ya uvuvi na mifugo hebu ileteni wilayani. Ninyi mko watumishi wachache. Nimekuja ofisini kwenu kaofisi kako hapo NBC wamebanana mle wataalamu hata hewa hawana bado mnang’ang’ania miradi ya nchi nzima mkae nayo mtaweza wapi? Tuleteeni hizi fedha wale wataalamu mlionao ninyi muwaweke huku lakini pia zile ofisi zako siyo nzuri sana kwenye suala mtu akija pale ofisini anashangaa kwamba humu ndiyo kuna wataalamu ambao wanasimamia Sekta ya Uvuvi? Sekta ya Mifugo kuna watu wengi sana ambao wameajiriwa katika mifugo na uvuvi. Ndiyo sekta pekee katika nchi hii ambayo ina ajira ya moja kwa moja. Hebu ilindeni hii sekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ng’ombe, hawa ng’ombe mnaowaona ninyi tunawafuga sisi miaka minne ndiyo anakwenda kuuzwa mnadani. Nendeni mkaangalie Argentina. Ng’ombe wa miaka minne ana tani 1.5. Sisi ng’ombe wa miaka minne ana kilo 88, kilo 110, mnafeli wapi? Mbona wataalamu mko wengi, hicho Chuo cha SUA kimekuwa ni chuo cha nini? Maana yake sielewi. Hebu pelekeni hao wataalamu waende field waende na Argentina. Hawezi kusoma SUA akaja field Sengerema kwenye ng’ombe wa kilo 80 wa miaka minne. Mpeleke akaone ng’ombe wa miaka minne Argentina na Brazil kule. Hata wewe angalia uwezekano wa kusafiri sasa kwenda kule, Mama ata toa kibali nchi imefunguka hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uvuvi. Mheshimiwa Ulega suala la uvuvi angalia sana hizi taa za solar. Hizi taa za solar zinapiga mpaka chini. Ziwa letu Victoria halina urefu mkubwa, kuna mita tisa, mita 20, mita 90. Sasa hizi taa zinapiga mpaka chini kwenye mazalia ya samaki. Litabakia ziwa la maji ya kunywa. Sisi tunakula samaki hawa kuanzia furu, nembe, gogogo, ngere yaani hatuna mahali chakula kingine sisi zaidi yetu hapo. Mmeona wenzenu sasa hivi wa Wizara ya Mambo ya Ndani. Anayetaka kuendesha pikipiki anapata leseni. Sasa sisi wavuvi suala la leseni.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Tabasam malizia mchango wako.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie.

MWENYEKITI: Haya malizia.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la hawa wavuvi. Mtu anakuwa ana kambi ya watu 120 hana hata mtaalamu mmoja kwenye kambi yake. Kwa nini msifanye na wenyewe mtu anayepata leseni apeleke siku saba aende Chuo cha Uvuvi Nyegezi pale anakaa siku saba anafundishwa namna ya uvuvi anakwenda kuwafundisha watu kambini. Hakuna mtu anayeendesha chombo halafu akakosa kuwa na taaluma.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam ahsante sana.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana naunga mkono hoja lakini nakuomba hawa watu wetu wa Wizara ya Uvuvi waangalie Ziwa Victoria sasa linabakia kuwa la maji ya kunywa, samaki wanaisha kwa ajili ya uvuvi haramu, 75% ni wavuvi haramu.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tabasamu muda wako umeisha.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi katika Ziwa Victoria. Ahsante sana Mheshimiwa Ulega nakutakia kazi njema. Mungu akujalie sana na watu wako wamekuja Sengerema nimeona nategemea Soko, kwenye soko la Samaki Nyapukalo na cold room, ahsante sana. (Makofi)