Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii kuweza kuchangia kwenye hoja iliyoko mezani ya Bajeti ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na wenzangu wote kwa pongezi walizotoa kuanzia kwa Mheshimiwa Rais wetu pamoja na viongozi wetu kwenye Wizara. Babu yangu Tabasam ametangulia kumpa angalizo Mheshimiwa Ulega kwamba yeye ni mzoefu kwenye Wizara hii na siyo mgeni na sasa ana mamlaka iliyokamilika kwa hiyo tunategemea makubwa sana na wewe ni kijana mnyenyekevu msikivu. Kwa hiyo, natumai hata Mheshimiwa Mhagama amekwambia ukitusikiliza Wabunge basi haya mambo uliyoyapanga yatafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwenye maeneo machache; la kwanza ni takwimu. Hivi tunavyoimba kwamba tuna ng’ombe milioni 32 tuna bata 10,000. Ni mfumo gani ambao umeutumia kutupa data hizi? Sitaki kuongea sana kwa undani lakini ushauri wangu sijui mfumo gani maana yako hayo mambo ya hereni na nini yanapigiwa kelele. Kama nia ni njema lakini huo utaratibu kidogo una ukakasi rudi nyuma kwa sababu huwezi kukamilisha mipango yako kama huna takwimu sahihi. Huwezi kwenda huko unakotaka kwenda kama hutokuwa na takwimu sahihi, una kaya ngapi zinazojihusisha kwenye mifugo na aina ya mifugo kwenye kaya hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwa kweli kwenye mipango yote anza na takwimu ndiyo itakuwa ufunguo mzuri wa wewe kwenda mbele kwenye mipango yako. Mheshimiwa Waziri kwa kweli hebu pitia upya sera zako pamoja na sheria mbalimbali kwenye mifugo na uvuvi. Leo hii kelele zote tunazopiga Waheshimiwa Wabunge kumshauri huyu anatumia Sera ya Mifugo ya Mwaka 2006, kweli Mheshimiwa Waziri? Tuko mwaka 2023 Sera ya Mifugo tunayotumia ni ya 2006. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii unatumia Ilani ya Uchaguzi ya 2020/2025, unatumia Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2021/2026. Kweli hii sera yako ya mifugo ya 2006 itakupeleka unakotaka kwenda? Kwa hiyo, ni vyema hebu tuweze kupitia hizi sera zetu. Pia kuna sera nyingine kati ya chache ambazo nataka kutolea mfano, kuna policy inaitwa disease control policy (Sera ya kupambana na kudhibiti magonjwa yatokanayo na mifugo na mazao ya mifugo). Kama hatutoweza kuipitia hii kitu kwa kweli ndoto ya sisi kuuza bidhaa zetu kwenye soko la kimataifa tulifute.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano ambao uko hai. Kuna kampuni siitaji jina ilipata soko kubwa la nyama ambayo imechakatwa kwenye thamani mbalimbali kule Afrika Kusini pamoja na Nchi ya Msumbiji. Walikwama kwenye soko hilo kwa sababu leo hii nyama yetu hairuhusiwi kuuzwa kwenye nchi za SADC kwa sababu tunao ugonjwa wa foot and mouth disease. Siyo kwamba huo ugonjwa hamuufanyii hatua za kuudhibiti lakini policy yetu ya disease control haiko wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wafanyabiashara wengi hawasemi tu, hata hao wanaotafuta soko la maziwa, soko la nyama za kuku huko nje, mayai wanakutana na hichi kitu. Maswali wanayoulizwa hawana majibu sahihi. Kwa hiyo mimi naomba sana Mheshimiwa Waziri hebu hizi sera zetu twende tukazipitie, sheria zetu lete hapa zifanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaongelea blue economy lakini nautical miles zinazoruhusiwa kuvua samaki haziwezi kuleta tija siyo tu kwa wavuvi wadogo, hata kwa wawekezaji wakubwa wenye viwanda vya samaki haiwezi kutuletea tija Mheshimiwa Waziri. Naomba hizi sheria kaa uzipitie na wataalamu wako, tuletee hapa Bungeni tuweze kuzirekebisha na kuzipitisha ili hicho unachopanga kwenye mafanikio yako iweze kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri unataka kwenda kuongeza kipato kwenye sekta hii na wako Waheshimiwa Wabunge waliotangulia wanashangaa Sekta ya Uvuvi siyo ya kuchangia 1%, hiyo ni aibu. Hebu jiulize leo nchi zinazotuzunguka tunawapelekea mahindi na bidhaa za kilimo kwa nini siyo bidhaa za uvuvi ama za ufugaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwennyekiti, tuna ng’ombe wengi kuliko nchi za jirani. Leo hii Tanzania tumezungukwa na land locked countries ambazo hawana bahari lakini kwenye maziwa matatu tuliyokuwa nayo, Victoria, Tanganyika na Nyasa sisi ndiyo wenye share kubwa ya hayo maziwa kuliko nchi jirani. Kwa nini sisi tunashindwa kutumia hii kama fursa ya kuweza kujiongezea kipato lakini kuna mambo ambayo yanakuwa kikwazo kwenye hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni biashara ya haya mazao yetu mengi yanafanyika kwenye mfumo usio rasmi. Mfano, soko la maziwa, 97% ya maziwa yetu yanauzwa kwenye mfumo usio rasmi, ni 3% tu sasa hapo utaonaje tija ya biashara ya maziwa kama haujaimarisha kwamba haya maziwa yanayozalishwa na wafugaji wetu yakauzwa kwenye mfumo ambao ni rasmi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Tabasam ametangulia kusema anasikitika Ziwa Victoria lile tunaenda kuwa nalo ambalo halina tena mantiki tena babu zangu Mwanza kule bahati nzuri zamani walikuwa na dhahabu, sasa hivi dhahabu imehamia Geita. Sasa Mwanza hii miaka kumi na kitu iliyopita tulikuwa tuna viwanda zaidi ya 10. Leo Mwanza vimebaki viwanda vitatu tu vya kuchakata samaki.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Amar.
TAARIFA
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hatuwezi kuwa na tija kwa wafugaji wetu kupata maziwa yaliyo mengi kwa sababu tuna maafisa ugani wachache. Mfano Nyang’hwale tuna maafisa ugani wako wanne na tuna kata 15 na kuna wafugaji unamkuta ana ng’ombe 100 lakini hata lita tano za maziwa hazipati. Hatuwezi kufanikiwa kwa mtindo huu. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Mariam taarifa unaipokea?
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea na pia niunge mkono hoja ya Waziri ya kutaka kuanzisha hizi mamlaka maalum ili zitamuongezea rasilimali watu lakini na rasilimali fedha. Kwa hiyo rai yangu kwa Serikali hii mipango ya Waziri basi wakaipokee na waweze kumpa fedha ili aweze kuikamilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii niwaambie hatuwezi kuona tija na thamani ya sangara kama hatutopeleka sangara kwenye Soko la Dunia. Sangara akiuzwa kwa mama ntilie hapa ndani ya nchi hana tija na Waziri unajua. Sangara ana vitu viwili; ana mnofu, ana kitu kinaitwa mabondo (fish morse) lakini nisikitike leo viwanda vimeenda kufa ajira zimepungua kwa sababu tu hii biashara ya mabondo inafanywa kiholela. Unapoteza mapato Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikwambie hebu kunja moyo fanya maamuzi magumu. Hebu tuombe ndani ya miezi mitatu au miezi sita, rasimisha hii biashara, mtu hakatazwi kuuza mabondo yake lakini aende akauze kwenye sehemu ambazo zimeidhinishwa na wizara, kama viwandani na center zingine za kupokea kwanza utafanya udhibiti wa thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu hakatazwi kuuza mabondo yake lakini aende akauze kwenye sehemu ambazo zimeidhinishwa na Wizara, kama viwandani na center zingine za kupokea. Kwanza utafanya udhibiti wa thamani; leo hii hayo mabondo yenyewe siyo kwamba yana grade moja, mabondo yana grade A, B, na C. Leo hii wewe huna hiyo takwimu, mabondo unauza tu kama bondo, leo hii mimi najua…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mariam.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo una mipango mikakati mizuri ya kuzalisha sato. Leo hii sangara ana bei ndogo kuliko sato. Hao sato unaowazalisha watakosa soko kwa sababu sangara yuko humu ndani, wakati sangara tukimtoa nje ataleta tija kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumalizia, ninao ujumbe kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini, wanakusifu sana Mheshimiwa Waziri unafanya kazi kubwa wana maombi mawili. Machinjio yetu kule…
MWENYEKITI: Muda wako umeisha.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: … kwa kweli yamechoka na hayakidhi usalama wa ng’ombe wanaochinjwa pale pia ni wafugaji wakubwa wa kuku wa kienyeji. Faida za kuku wa kienyeji tunazijua, tunaomba utuletee wawekezaji ili…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: … ufugaji ule wa kuku wa kienyeji uweze kuwaletea manufaa wananchi wa Kondoa Mjini, ahsante sana. (Makofi)