Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba mwaka jana tumefanya sensa ya Taifa na wenzetu wa NBS wametoa takwimu nzuri kabisa juu ya mifugo tuliyonanyo katika Taifa letu. Ng’ombe tunao zaidi ya milioni 35, mbuzi milioni 25.6 na wanasema kondoo tunao takribani milioni nane. Hii pee itakusaidia wewe kupanga mipango yako vizuri kama wizara na kuhakikisha tunasaidia Watanzania kuvuka kwa mahitaji ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya ng’ombe na wanyama yameliingizia Taifa hili dola takribani milioni tatu. Hii ni hela ambayo kimsingi ikiongezewa nguvu tutapata zaidi ya hiyo pesa, kuweza kusaidia uchumi wa Taifa letu. Tatizo kubwa lililopo katika Taifa hili ni mipango na utekelezaji. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wengi wameelezea suala hili. Huwezi kuwa na mipango ambayo unaingiza nyama na wakati huo huo una wafugaji wako, na hawa wafugaji hujawajengea uwezo wa kulisha. Wamesema hapa, ng’ombe miaka minne ana kilo 80 wakati wenzetu ana zaidi ya kilo 500. Ni lazima tufanye kazi ya kuwasaidia Watanzania waweze kutoa bidhaa bora kuweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa Tanzania ni nchi ya pili kati ya nchi zenye mifugo mingi. Kwa nini sisi tusizalishe zaidi ya wenzetu ambao wanafanya vizuri, kama vile Botswana na nchi zingine? Mimi ninafikiri Waziri wa Fedha anahusika zaidi kutoa fedha kwenye Wizara hii. Nilikuwa nikiongea na Naibu Waziri anasema tukipata fedha tuna uwezo wa kufanya maajabu katika wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakaa hapa kama Bunge tukipanga mipango mingi lakini kutoa fedha hatuwezi kuwasaidia. Wataalam tunawalaumu, kwamba wapo, wamesoma na wapo ofisini wanalipwa mishahara, lakini usipowapa fedha hawawezi kufanya yale ambayo tumewapa, mwisho wa siku bajeti inakuwa ndogo. Tunakubaliana hapa kama Wabunge mwisho wa mwaka wanafanya fedha asilimia mbili, asilimia tatu; hatujafahamu ni nini mnakifikiria ilhali mnajua kabisa wizara hii ina wakulima na wafugaji wengi. Hao ndio wanaoweza kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ukosefu wa miundombinu, lakini pia miundombinu si salama na si rafiki kwa ajili ya wafugaji. Tunazungumzia maziwa kwa mfano, jana tumepata maziwa hapa kama Wabunge, lakini bado mfugaji amekuwa mtumwa wa ng’ombe au wa mifugo yake. Kwa mfano kule kwetu Rungwe lita moja ya maziwa ni shilingi 600; leo hii maji yana thamani kubwa kuliko maziwa. Mfugaji analala na ng’ombe anaamkia ng’ombe, akifiwa anamuwaza ng’ombe kwanza kuliko ndugu yake aliyefariki lakini mwisho wa siku lita moja shilingi 600; hatuwatendei haki wakulima. Tunaomba bei ya maziwa iongezeke. Maziwa ni chakula, huwezi kuuza maziwa lita moja kwa 600, maji madogo ya chupa nusu lita shilingi 1,000, hii si sawa kabisa. Inabidi kujipanga viongozo ili tuhakikishe tunawatetea wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa masoko, tulikuwa na kombe la dunia, tulipatapata kidogo masoko ya nyama, lakini mwisho wa siku, wamesema Waheshimiwa Wabunge waliopita; thamani ya nyama yetu miundombinu inayotengenezewa inafanya sisi tusipate soko la dunia kwa vizuri zaidi. Amesema hapa Mheshimiwa Mhagama, kwamba anayetoa nyama kutoka Afrika kuipeleka Dubai ni karibu zaidi kuliko anayetoka Brazil kuileta pale Dubai. Inabidi tukae chini na tujitafakari ili tuone nanma gani tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mlipuko wa magonjwa wananchi wenyewe wanaamua kujitetea. Magonjwa ya mifugo yanapokuja wao wenyewe wanaamua kuona namna gani wanadhibiti. Tunaomba Serikali isimamie. Maafisa Ugani ni wachache mwisho wa siku wananchi wenyewe wanaamua kujisimamia badala ya ninyi kufanya kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwekezaji mdogo, nimesema kuna viwanda vya uwekezaji, tuna machinjio ambayo kiukweli mengi; unajua nchi za kiarabu ndio wananunua zaidi nyama. Kwa hiyo ni lazima tuwahakikishie wenzetu waarabu ambao wao wanapenda nyama halali, kwa hiyo tuwahakikishie kwamba nyama yetu ni salama ili wawe huru kuja kununua nyama kutoka kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna nguvu zaidi inabidi kuongezeka. Tuna tani zaidi ya laki saba za nyama ambazo zinavunwa, lakini kwa jinsi tulivyo tunahitaji kupata nyama zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wafugaji na ufugaji wa kuhamahama. Ninajua wenzangu ambao wanatoka maeneo ya wafugaji watalalamika, lakini tufike mwisho, tupande majani kwa ajili ya wanyama wetu waweze kula katika maeneo yetu kuhamahama kupungue ili tuweze kupata nyama iliyo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia suala herein, nashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu jana ametolea maagizo kwa Mheshimiwa Waziri; tunaomba alifanyie kazi haraka, kwa sababu tunatoa matamko; leo anapigwa chapa kesho mnasema herein, lakini mwisho wa siku utekelezaji unachelewa. Ninaomba sana uyasimamie aliyoyasema Mheshimiwa Waziri Mkuu jana ili yaweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo tunaomba Waziri wa Fedha pamoja na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ongezeni fedha kwenye wizara hii, ili Watanzania waweze kunufaika na Wizara yao. Baada ya kusema hayo nasema ahsante. (Makofi)