Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ulega kwa kuchaguliwa kuwa Waziri wa hii Wizara. Nina matumaini kwamba Mheshimiwa Ulega atakuwa msikivu kwa sababu kama ni mwanafunzi amesoma kama miaka minane hiyo elimu ya Uwaziri, sasa sitegemei kama atatuangusha. Mwanafunzi mzuri ni yule anayesikiliza walimu wake na baadaye anafaulu, tunamwombea sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwa kusema sisi tunatoa tu ushauri kwa Serikali, wanaweza wakakubali au wakakataa, lakini mkikataa mbeleni tutakuja kuulizana maswali. Mwaka 2017/2018 ndugu yangu Mpina akiwa Waziri yeya akiwa Naibu, tulizungumza hapa kuhusu usumbufu waliokuwa wanaufanya Ziwani kwamba madhara yake tutayaona baadaye hawakutusikiliza. Leo tunalia samaki wameisha, wavuvi wamefilisika haya yote Mheshimiwa Waziri ameyapitia sasa tunataka tumpe ushauri atoke hapo alipoikuta Wizara, aende sehemu ambayo Mungu atamsaidia aendelee kubaki kwenye hii Wizara kama Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita tu kwenye suala la herein. Inahitaji kuwa mjinga sana kwa kizungu mnasema you need to be very ignorant kizungu ndiyo mnasema hivyo? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake unatakiwa kuwa mjinga wa mwisho, kutoutambua huu mtego. Hawa wafugaji ni watu maskini na Serikali lazima wasikilize, hii biashara wanayoiweka wanaolalamika ni wananchi, wanaotutuma ni sisi Wabunge. Mwaka 2025 watasimamisha kukitetea chama chetu na kuomba tena nafasi ya kurudi humu kama hatuwasikilizi hawa na kuyaleta malalamiko humu ndani wakayafanyia kazi, wakaanza porojo za kupandishana, kuwekeana maneno mdomoni, haitatusaidia huko mbele tunakoenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, herein, mimi nafuga ng’ombe, watafiti na wataalam, waliosomea mambo ya mifugo, walianza wakaja hapa na mihuri ya kugonga si wao? Wakashauri tukiweka hivi tunapata thamani ya ng’ombe, wakagonga ngozi, wakaja wakavalisha bangiri, sasa wamekuja na hereni nataka niwaulize swali halafu mbaya zaidi tunatafuta takwimu sahihi za mifugo. Unaenda kuchukua wakala akufanyie takwimu ndiyo akukabidhi, hivi hatuna wasomi waliosoma mambo ya TEHAMA, tunasomesha watoto wetu kwa kazi gani? Nataka waniambie tulihesabu binadamu sensa yetu ya mwaka jana, kwa nini hawakuweka wakala? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliingia gharama bilioni 400, wakanunua vishikwambi, watu wakafanya kazi. Watoto wetu wamesoma TEHAMA, hawana ajira, wanaenda kuchukua mabilioni ya hela wanamrundikia wakala yumo humu ndani, ana-lobby lobby eti tufunge herein. Nataka niwaulize swali, sipingani na maagizo ya Waziri Mkuu, tunaboresha wasini-quote vibaya, hiyo hereni wanayoenda kuifunga, sidhani kama wamefuga ng’ombe, hivi ng’ombe wakigombana kule porini ikadondoka herein, wataniambia aliyepigana naye ni nani? Haya ng’ombe waangu wakihibiwa, wakaenda Mtwara kutoka Geita watanipigia Musukuma usiende pPlisi fuata wako Mtwara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni utapeli ambao wanataka kutuingiza kutuchonganisha na wananchi. Mheshimiwa Waziri asikubali huu mtego, Wizara yakw iombe hela Serikalini, aajiri vitengo, katika kila halmashauri na kila kata tuna bwana mifugo ana kazi gani? Kwa nini asimpe takwimu za ng’ombe? Nataka niwaambie tusikubali huu mtego na Bunge likawa wakala wa kupitisha dili za watu humu ndani, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfugaji ni maskini, ili apate laki tano lazima auze ng’ombe, hivi Serikali nataka niwaulize, huyu mfugaji ambaye Tanzania hii hathaminiki anaishi kama mbayuwayu tu yuko huku, yuko huku, unaenda kuhesabu ng’ombe ambao leo wako Geita kesho wako Mtwara, kesho Bagamoyo, yanakoota majani ndiyo mfugaji anaenda. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kama kuna sehemu sasa amewekwa target ni hapa. Najua hili jambo alikuwa ulipendi maana tulikuwa tunateta kantini, sasa nataka nimwone term hii. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu wakala anayezungumzwa humu alishatajwa na Mheshimiwa Shabiby, atusamehe sana, sisi wote ni Wabunge na kila mtu ana neema kwenye jimbo lake. Jimbo la Kibaha linafuga kuku, tuzifunge kuku hereni kwanza kabla ya ng’ombe. Haiwezekani, hata kuku ni nyama na zinaingiza pato la Taifa. nikuombe sana Mheshimiwa Waziri akae vizuri asikubali huu mtego na najua watu tukizungumza humu wanasema huyu kafanyiwa lobbying kapewa hela, hakuna cha kutupa hela mimi ni mfugaji na Jimbo langu lina wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu anayepiga upatu jimbo lake linaongoza kwa mabanda ya kuku, tuanze na kuku, tuone mfano, lakini tukimaliza hapo Mheshimiwa Ulega, najua tena nafurahi jana kulikuwa na wageni mashehe leo hawapo. Mashehe kazi yao ni kuomba na najua na wewe kwako kuna ng’ombe, tujaribie Wilaya ya Mheshimiwa Waziri kwanza hizo herein, zikifaulu ndiyo walete hawawezi kuwa wanafanya majaribio kwa watu maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana hatuna nia mbaya na mategemeo ya Mheshimiwa Waziri, lakini anatuweka kwenye angle ambayo kiukweli siyo nzuri na Serikali yetu imetulia tunaenda kwenye chaguzi, watu wana amani, tumemaliza purukushani za machinga unaingia tena machinga mfugaji, hii kitu haiwezekani. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na hata yule anayepiga dili tuangaliane kwa macho hivi, sijui kaenda wapi? Kahamia wapi? Tusikubali hili suala, najitoa muhanga, tusikubali hili suala likazungushwa humu ndani. Waziri aweke teknolojia, aombe Serikali impe kompyuta agawe kwa kila Bwana Mifugo, Afisa Ugani kule katika kila Kata wapo, leo Maafisa Ugani kule wamekuwa wanywa gongo tu, wanakaa maofisini, ukienda wamechoka hawana hata kazi. Ni watu wa operesheni tu midomo, sijui miguu, hawana kazi za kufanya, Mheshimiwa Waziri apeleke watu, alafu aone maisha yanavyoenda… (Makofi)

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, kuna taarifa.

TAARIFA

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba hivyo anavyozungumza tayari Wasukuma, wafugaji wote wa Mtwara, Geita, Mwanza na Magu wote ng’ombe zao zina herein, je, watarudishiwa fedha?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Msukuma, taarifa unaipokea?

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa mimi ni mfugaji, kwanza ukiacha alizoziona zina hereni, kuna zinazodai yaani hata uwekaji wa hereni unalipa kwanza, unaingiza kwa mtu hela, halafu ndiyo anaenda kutengeneza. Nchi hii jamani inahitaji kusoma kwa mtaa kabisa, tuache shule za darasani. Nakubaliana na yeye kwamba kuna hereni, kuna nini, lakini ni maumivu makubwa ambayo wafugaji wanayo kule kijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao wafugaji wamekuja kusikiliza hii Wizara, tokeni nje hapo muwaulize hii si kitu wala siyo hitaji. Kama hitaji ni la Serikali tengeni bajeti, mbona sisi binadamu wametuhesabu bila kutuomba hela. Hivi binadamu na ng’ombe nani ana thamani unaacha binadamu anayeingiza kipato kumhesabu hata kwa shilingi elfu mbili mbili anatuhesabu bure, halafu ng’ombe wanaomlisha mtu anapata madini mwilini, wanaichaji elfu mbili. Hawana soko, hawana machungio, hawana sehemu ya kunyweshea maji, wagosha wajameni! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana tubadilishe mwelekeo, Mheshimiwa Waziri…

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma kuna taarifa, kutoka kwa Mheshimiwa Emmanuel Shangai.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji, kwenye minada yetu Wizara inapata shilingi 2,500 kwa kila mfugo unaouzwa. Watumie hizo fedha kuwahesabu hao ng’ombe.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana nayo. Nimwombe tu Mheshimiwa Waziri, asikubali kuingia kwenye huu mtego na hili akusanye hela atoke kwenye asilimia moja ya pato la Taifa, Mheshimiwa Waziri ananisikiliza au anachati? Atoke kwenye hii nafasi aliyobananishwa na naamini Wizara yake ina wasomi, tunamwamini sana rafiki yangu, msomi mwenzangu Shemdoe, wakae watengeneze utaratibu mzuri, haya mambo ya dili dili waachane nayo, ili upate kipato kizuri tujifunze kwenye Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Madini ilikuwa inachangia asilimia moja kwa sababu wachimbaji wadogo walikuwa wanawaona kama wezi, kila wanapovumbua madini wanawapeleka polisi, wanapiga watu wanaweka wazungu wenye leseni. Tulishauriana nao humu ndani leo angalia tunavyochangia kwenye pato la Taifa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Sina tatizo na, Mheshimiwa Ulega, lakini wakati wa ku–wind up hapa akija na jibu la mawenge mawenge namdakia shilingi yake, ahsante sana. (Makofi)